BANIY QAYNUQAI-MAYAHUDI WA KWANZA KUDHIHIRISHA UADUI

Mayahudi wa kabila la Baniy Qayunqaa, ndio waliokuwa wa mwanzo kabisa kuwadhihirishia waislamu uadui.

Hii ni kwa sababu wao ndio waliokuwa mashujaa kuliko makabila yote ya kiyahudi na ndio walikuwa majirani wa karibu wa waislamu.

Hawa waliishi baina ya waislamu katika kitovu cha mji wa Madinah. Ama mayahudi wa kabila za Banin-nadhwiyr na Baniy Quraydhwah, hawa waliishi viungani na pembezoni mwa mji wa Madinah.

Ujirani na ushujaa huu ndio uliowafanya Baniy Qayunqaa kuwa maadui dhahiri wa mwanzo wa waislamu kuliko mayahudi wengine.

Na yahudi aliyekuwa shadidi mno katika kujihirisha uadui kwa waislamu kuliko wenzake, huyu hakuwa mwingine ila Ka’abu Ibn Al-Ashraf.

Huyu alikuwa ni miongoni mwa washairi na mabwana wakubwa wao. Huyu alianza kuwacheza shere waislamu, akamsingizia uongo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kuwahamasisha watu kumuua.

Kadhalika alijitia kuwaombolezea makurayshi watukufu waliouawa na waislamu ili kuwachochea makurayshi kulipa kisasi kwa waislamu.

Hakutosheka kuyafanya haya pale Madinah tu, bali alikwenda mpaka Makah kuwachochea watu kumuua Bwana Mtume. Ili kuwachochea zaidi watu na kuwapandisha mori, aliimba mashairi na kujitia kuwalilia watu wa kisima.

Hawa ni wale makurayshi waliouawa katika vita vya Badri, miongoni mwao akiwa ni Abuu Jahli.

Hivi ndivyo hali ya hewa ilivyosheheni uadui baina ya waislamu na mayahudi, nyoyo za watu zikajaa mifundo na chuki.

Jambo lo lote dogo la kipuuzi tu lilitosha kabisa kuwa ni sababu ya kuwasha moto baina ya makundi mawili haya yenye kukamiana.

Cheche zilizouwasha moto huu mkubwa, hazikuwa nyingine bali ni lile tukio la mwanamke wa kiislamu. Huyu alikwenda katika soko la Baniy Qayunqaa kwa ajili ya kujipatia mahitaji yake.

Akaliendea duka la sonara, hapo ndipo myahudi mmoja akamfanyia mwanamke huyu wa kiislamu kitendo cha kumdhalilisha na kumvunjia heshima.

Mmoja wa waislamu aliyekuwa mahala hapo na akashuhudia namna muislamu mwenzake anavyodhalilishwa, hakuweza kuvumilia kuliona tendo baya lile.

 Akamuendea yule myahudi aliyemdhalilisha mama wa kiislamu na kumuua. Kuona hivyo mayahudi wakamkusanyikia muislamu yule mmoja na kumuua kulipa kisasi cha myahudi mwenzao aliyeuliwa naye.

Hapa tena waislamu wakawa wanaitana kuja kupambana na mayahudi na mayahudi nao wakaitana kuja kukabiliana na waislamu.

Hali ya hewa ikachafuka kiasi cha kutaka kugeuzwa mahala hapo kuwa machinjioni, lau zisingekuwa hekima na busara za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuzizima cheche hizi.

Bwana Mtume akawaita viongozi wa mayahudi na kuwatahadharisha na kuwaonya juu ya matokeo ya dhulma waifanyayo na kuvunja kwao ahadi (mkataba) ya amani. Akawaambia:

 “Enyi kusanyiko la mayahudi, tahadharini na Allah isije ikakufikeni kama nakama (adhabu) iliyowafika makurayshi. Nakutakeni msilimu, kwani nyinyi mnajua fika kwamba mimi ni Mtume (wa kweli). Haya mnayapata ndani ya kitabu chenu na agano la Allah kwenu nyinyi”.

 Kusikia hivi, mayahudi wakamkunjia uso Bwana Mtume na kumwambia kwa ukali kabisa:”Ewe Muhammad wee! Hivi unadhania sisi ni kama hao jamaa zako (makurayshi wenzio)? Kusikughuri kupambana na watu wasio na ujuzi wa vita, ukapata fursa ya kuwashinda.

 Hakika sisi, wallah tukipigana na wewe utatutambua kwamba sisi ni watu kweli (wala sio kama jamaa zako)! Ibn Ishaaq-Allah amrehemu-anasema hawa ndio mayahudi wa mwanzo kuvunja mkataba wa amani na ujirani mwema waliotiliana saini na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

 

KUVAMIWA NA KUSHAMBULIWA BANIY QAYUNQAA.

Hali ya ujirani na mahusiano mema baina ya waislamu na mayahudi ikavunjika. Baniy Qayunqaa wakageuka na kuwa maadui wakubwa wa waislamu baada ya kuwa walikuwa marafiki wema siku za kisogoni.

Isitoshe wao ndio waliokuwa mstari wa mbele katika kufanya mambo na kusema maneno yanayopelekea kwa namna moja au nyingine kuvunjika kwa amani.

Wakatumia kila njia kuhakikisha kuwa amani iliyokuwepo baina yao na waislamu inatoweka kwa kuchochea kulipuka kwa vita ili wapate fursa ya kutoa chuki zao. Je, katika hali kama hii waislamu watakuwa na amani kwa upande huu wa mayahudi? Hapa ndipo Allah Mola Mwenyezi akamshushia Mtume wake:

“NA KAMA UKIOGOPA KHIANA KWA WATU (mliofanya nao ahadi) BASI WATUPIE (ahadi yao) KWA USAWA, HAKIKA ALLAH HAWAPENDI WAFANYAO KHIANA”. [8:58]

Naam, imekwisadhihiri khiana machoni pa mayahudi, kwani tayari wamekwishavunja ahadi walizoagana na Mtume wa Allah na wakaanza kuingilia mambo ya Mtume na maswahaba wake.

Wakatafuta sababu za kuwachokoza waislamu na kuwaudhi, wakawa sasa hawaaminiki kwa upande wa amani na ilhali wanajiranikiana na waislamu katika maskani na wanachanganyika nao katika kazi na shughuli mbalimbali.

Hawa wanajua mambo mengi ya ndani ya waislamu na kuzichomozea siri zao nyingi, kwa hivyo watu hawa ni watu hatari sana kwa waislamu.

Kwa hali hii, ikawa hapana budi ichukuliwe hatua mkataa (decisive) itakayowahakikishia amani na utulivu waislamu.

Hivi ndivyo alivyofanya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza na kuwatupia ahadi yao kama walivyotangulia wao kufanya hivyo.

Akawatangazia uadui waziwazi na kuwatahadharisha na khatari ya kukabiliwa na vita vikali kabisa.

Mayahudi walipoyakinisha kwamba Mtume hafanyi mzaha katika hili, wakajitia katika ngome zao ili kujilinda na mashambulizi yanayotegemewa kutoka kwa waislamu.

Kuona hivi Mtume wa Allah akaamua kuwazingira, akawazingira kwa kipindi kisichopungua siku kumi na tano.

Katika kipindi chote hicho alihakikisha kuwa hawapati chakula, maji, nguvu wala msaada wa aina yo yote ile kutoka nje.

Bwana Mtume alifanya hivi ili kuivunja nguvu yao na hatimaye wajisalimishe wenyewe bila ya kumwagika damu.

Hawa Baniy Qayunqaa walikuwa ni washirika na ndugu wa yamini wa Ubaadah Ibn Swaamit na Abdullah Ibn Ubayyi (wenyeji wa Madinah).

Mayahudi hawa walipodhihirisha uadui wao waliokuwa wameuficha, Ubaadah Ibn Swaamit akawakana na kuwakataa.

Ama Abdullah Ibn Ubayyi, yeye aliendelea kuwa mtiifu kwao na hakuwakana kama alivyofanya Ubaadah. Na alikuwa akisema: “Mimi ni mtu ninayechelea mageuzi ya mambo na wala sijiaminishi na zama”.

Kujitia ngomeni kwa mayahudi hakukuwasaidia cho chote, kwani hakuna ye yote aliyeweza kuwapa msaada katika kipindi chote hiki cha mazingiwa (blockade).

Wala ndugu zao (mayahudi wenziwao) wa kabila la Banin-Nadhwiyr na Baniy Quraydhwah hawakuweza kuja kuwaokoa.

Pengine hili la kutokusaidiwa hata na mayahudi wenziwao linathibitisha khiana yao na kwamba wao ndio waliofanya jeuri na dhulma.

Na wakatangaza vita kwa kuvunja kwao ahadi na maagano, wakaudhihirisha uadui na upinzani wao kwa Mtume na maswahaba wake.

Mazingiwa yaliporepa (yaliporefuka) na wakashindwa kupambana wao wenyewe na waislamu, ikawapata khofu kuu.

Wakamsihi Bwana Mtume awaruhusu kuondoka Madinah, wao, wake zao pamoja na watoto, nae Mtume na maswahaba wake wachukue mali na silaha zao zote.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawakubalia ombi lao hilo na akawapa muda wa siku tatu na akamuwakilisha Ubaadah Ibn Swaamit kusimamia utokaji na uondokaji wao.

 Wakaondoka na kwenda sehemu iitwayo ‘Adhri’aat’ katika nchi ya Shamu na waislamu wakaichukua ngawira mali na silaha zao zilizokuwa nyingi.

Ikumbukwe kwamba mayahudi hawa walikuwa ni masonara na walikuwa ni watu wenye mapenzi makubwa katika ulimbikizaji wa silaha.

Mtume wa Allah akahodhi khumsi (moja ya tano 1/5) ya ngawira hii kwa ajili ya Allah, Mtume wake, jamaa za Mtume, mayatima, masikini na wasafiri walioharibikiwa. Na sehemu iliyosalia, yaani nne ya tano (4/5) akaigawanya miongoni mwa maswahaba wake.

Kuvamiwa huku kwa Baniy Qayunqaa kulikuwa katikati ya mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi) wa mwaka wa pili wa Hijrah.

Bwana Mtume akampa ukhalifa (ugavana) wa mji huu wa mayahudi, Abuu Lubaabah Al-answaariy na bendera yake akampa ami yake Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib.

Hivi ndivyo Baniy Qayunqaa walivyotolewa Madinah kwa sababu ya uasi na jeuri yao sambamba na kuanza kwao uadui na uchokozi dhidi ya waislamu.

 

BANIY QAYNUQAI-MAYAHUDI WA KWANZA KUDHIHIRISHA UADUI

Mayahudi wa kabila la Baniy Qayunqaa, ndio waliokuwa wa mwanzo kabisa kuwadhihirishia waislamu uadui.

Hii ni kwa sababu wao ndio waliokuwa mashujaa kuliko makabila yote ya kiyahudi na ndio walikuwa majirani wa karibu wa waislamu.

Hawa waliishi baina ya waislamu katika kitovu cha mji wa Madinah. Ama mayahudi wa kabila za Banin-nadhwiyr na Baniy Quraydhwah, hawa waliishi viungani na pembezoni mwa mji wa Madinah.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *