1. Ni karaha kwa mwenye kutawadha kuacha suna yeyote miongoni mwa suna tulizozitaja chini ya anuani :SUNNA ZA UDHU.
Kwa sababu kuacha kuzitekeleza suna hizo kutampelekea mtu huyo kukosa thawabu, na muislamu wa kweli siku zote hupupia kuitekeleza ibada yake kwa ukamilifu na kwa namna ilivyofundishwa na mwenyewe Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie-.
2. Ni karaha kuyatumia maji kwa israfu (fujo) kama ambavyo ni karaha kujidhili katika kutumia maji, yaani kutumia kidogo mno yasiyokidhi haja ya udhu kwa ukamilifu.
Hayo yote ni kinyume na suna ya Bwana Mtume na Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia :
“…. NA WALA MSIPITE KIASI HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI” [7:31]
3. Ni karaha kutanguliza kuosha mkono/mguu wa kushoto kabla ya mkono/mguu wa kulia, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na alivyotenda Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie.
4. Ni karaha kukausha/kufuta viungo vya udhu kwa kutumia leso/taulo.
Ukaraha huo utaondoka kwa udhuru kama vile baridi kali, hapo itakuwa si karaha. Imepokelewa kwamba Mtume –Rehema na Amani zimshukie – aliletewa leso/taulo (ili ajifutie) basi hakuigusa (hakuitumia)” Bukhaariy.
5. Kuupiga uso kwa maji pia ni miongoni mwa mambo yaliyo karaha katika udhu. Kwa sababu kitendo hiki kinapingana na utukufu wa uso.
6. Ni karaha kuzidisha kuosha au kupakaza zaidi ya mara tatu au kupunguza. Alisema Mtume – Rehema na Amani zimshukie – baada ya kwisha kutawadha mara tatu tatu : “Hivi ndivyo (unavokuwa) udhu, basi atakayezidisha zaidi ya hivi au kupunguza huyo atakuwa amekosea na kudhulumu” Abuu Daawoud.
7. Ni karaha mtu kuoshwa viungo na mtu mwingine bila ya kuwa na udhuru ukubalikao kama ugonjwa.
Hili limefanywa kuwa ni karaha na sheria kwa sababu ndani yake mna chembechembeza kibri na ubwana, vitu ambavyo vinapingana na uja/utumwa kwa Mwenyezi Mungu.
8. Ni karaha kwa aliyefunga kuyapeleka ndani sana maji katika kusukutuwa na kupandisha maji puani.
Hii ni kwa sababu ya kuchelea kumponyoka maji na kufika kooni yakaingia ndani na hivyo kusababisha kufisidika/kuharibika swaumu yake. Amesema Mtume wa Allah –Rehema na Amani zimshukie –
“Na balighisha (yapeleke maji ndani sana) katika kupandisha maji puani, ila ukiwa umefunga (usibalighishe)” Abuu Daawoud.
TANBIIH: Ikiwa imekatazwa kubalighisha katika kupandisha maji puani kwa mfungaji, basi kubalighisha katika kusukutua ni bora zaidi kukatazwa.