YALIYO HARAMU KWA ASIYE NA UDHU

Ni haramu kisheria kwa mtu asiyekuwa na udhu kufanya mambo yafuatayo : –
Kuswali swala yeyote ile iwayo; ya faradhi, ya suna, au swala ya maiti, au sijida ya kusoma Qur-ani au sijda ya shukrani. Haya yote yametegemezwa kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :

“ENYI MLIOAMINI ! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU, …” [5:6].

Na kwa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

“Mwenyezi Mungu haikubali swala ya mmoja wenu atakapohuduthi mpaka atawadhe (tena)” Bukhaariy.

Na kwa hadithi nyingine: “Hana swala mtu asiyekuwa na udhu”.

Na kwa sababu twahara ya hadathi ni sharti miongoni mwa sharti za kusihi swala, haitosihi swala ila kwa kupatikana twahara ambayo ni udhu.

Kutufu/kuizunguka Al-Kaaba Tukufu, twawafu ya fardhi au ya sunna kwa sababu twawafu ni swala.

Hii ni kwa dalili ya riwaya iliyopokelewa na Imam Tirmidhiy katika kitabu chake cha hadithi (SUNAN TIRMIDHIY) kutoka kwa Ibn Abbaas –Allah awawie radhi – kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie – amesema : “Twawafu ni swala isipokuwa kwamba Allah mtukufu amehalalisha kuzungumza ndani yake. Basi yeyote atakayezungumza asizungumze ila lile la kheri”.

Kuugusa msahafu wote au baadhi yake. Hili ni kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu :

“HAPANA AKIGUSAYE ILA WALIOTAKASWA” [56:79].

Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anatufasiria kauli hii ya Mola Mtukufu anasema : “Asiiguse Qur-ani ila aliye twahara”

Na kwa sababu kuitukuza Qur-ani Tukufu ni wajibu miongoni mwa kuitukuza ni muislamu kuigusa il-hali ya twahara. Wamekongomana na kuwafikiana wanazuoni wa fani hii ya fiq-hi kwamba INAJUZU kwa mtu asiyekuwa na udhu kuisoma Qur-ani Tukufu bila ya KUIGUSA.

Kama alivoruhusiwa mtoto mdogo kuigusa bila ya udhu kwa lengo la kujifunza, kwa kuwa yeye si MTU MUKALLAF (anayelazimiwa na hukumu za sheria).

Pamoja na rukhsa hii bado ni bora azoweshwe kuigusa Qur-ani Tukufu akiwa na udhu ili kuipandikiza heshima na utukufu wa Qur-ani ndani ya moyo twahara wa chipukizi huyu. Akuwe akitofautisha Qur-ani na vitabu vingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *