Tumeeleza katika somo lililopita kwamba baba yake Bwana Mtume ni Mzee Abdallah Bin Abdul-Mutwalib na mama yake ni Bi Aaminah Bint Wahab.
Bwana Abdallah alikuwa ni miongoni mwa vijana bora wa mji wa Makkah na alikuwa mzuri wa umbo na tabia njema.
Bi Aaminah alitokana na kabila tukufu na alikuwa ni miongoni mwa mabinti wa makkah waliosifika kwa tabia njema na alijaaliwa na umbo na sura nzuri.
Baada ya Bwana Abdallah kumuoa Bi. Aaminah alisafiri pamoja na mkewe kuelekea Shaamu kwa ajili ya biashara,
Wakati anarudi Makkah akitokea Shaamu alishikwa na maradhi njiani, akaamua kwenda kujitibia Madinah ambako maradhi yalimzidia akafa na kuzikwa hapo hapo Madinah.
Baada ya mazishi mkewe alirudi Makkah hali ya kuwa ana huzuni ya kumpoteza mumewe mpenzi na wakati huo Bin. Aaminah alikuwa na mimba ya Bwana Mtume
Ama kisa cha kuchinjwa Bwana Abdallaha baba yake Mtume kilikuwa kama ifuatavyo:-
Bwana Abdallah alikuwa akipendwa sana na baba yake kuliko nduguze wengine. Ikatokezea kukauka chem chem ya maji ya ZamZam nyakati za Hijjah ndipo Mzee Abdul- Mutwalib akaweka nadhiri ya kumchinja mmojawapo wa wanawe kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mola wake maji yatakapozidi/yatakapoongezeka.
Maji yalipoongezeka ndipo ikamlazimu Bwana Abdallah kuitekeleza nadhiri aliyoiweka ya kumchinja mmojawapo wa wanawe. Sasa achinjwe nani?
Ikabidi ipigwe kura, na kila mara ikawa inamuangukia Bwana Abdallah baba yake Mtume.
Kwa kuwa mtoto huyu ndiye aliyekuwa kipenzi cha baba yake bali watu wote ndipo kiongozi mmoja wa dini akamshauri Mzee Abdul-Mutwalib apige kura baina ya mwanawe Abdallah na idadi fulani ya ngamia.
Kila mara kura itakapo muangukia Abdallah iliongezwa idadi ya ngamia mpaka kura iwaangukie ngamia.
Idadi ya ngamia ilipofika ngamia mia ndipo kura ikawaangukia ngamia wale, Mzee Abdul-Mutwalib akawachinja ngamia wale kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kwa kitendo hicho ikawa Bwana Abdallah ameokoka na kuchinjwa na ngamia wale wakawa ndio fidia yake.
Kisa hiki kinatukumbusha kisa kikongwe kilichojaa mafunzo mengi cha kutaka kuchinjwa Nabii Ismail Bin Ibrahim – Amani ya Allah iwashukie wakati Nabii Ibrahim alipooteshwa usingizini amchinje mwanawe Ismail.
Kwa kuwa ndoto za mitume huwa ni wahyi kwa Mwenyezi Mungu, Nabii ibrahim akaanza kuchukua hatua za kuitekeleza amri ya Mola wake, akamlaza mwanawe ili amchinje ndipo Mola mwingi wa huruma akamkomboa mja wake Ismail kwa kumleta kondoo wa peponi achinjwe badala ya Ismail kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani.
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume akisema:
“Mimi ni mtoto wa wachinjwa wawili “ Nao ni Babu Nabii Ismail, huyu ndiyo mchinjwa wa kwanza na wa pili ni baba yake Mzee Abdallah.