WACHUMBA KUZOEANA TABIA

Leo tena kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, jukwaa, lako la Nasaha za wiki linaendela kukuletea na kukuchambulia mila na desturi zinazopingana na kukhalifiana na sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Karibu unasihike pamoja nasi.

2. WACHUMBA KUZOEANA TABIA

Hii ni ada na desturi ambayo inaishi na kuchukua nafasi katika baadhi ya familia katika jamii zetu. Binti anapoposwa na kijana na kufungwa kile kinachoitwa “pamvu”, kitu ambacho uislamu haukitambui.

Pamvu ni kile kitu ambacho hupelekwa kwa wazazi wa binti ili kufunga mlango wa posa na kuonyesha kuwa tayari binti yao amekwishachumbiwa.

Baada ya kufungwa kwa pamvu, kijana wa kiume huwa na fursa ya kufika nyumbani kwao na binti na kupokelewa kwa mapana na marefu.

Akapikiwa, akala na kunywa kwa raha na furaha. Akawa na uhuru wa kukaa peke yake na binti faraghani wakazungumza na kucheka kwa furaha. Zaidi ya yuote hayo, kijana anaweza kumchukua binti na kwenda kutembea nae kokote apendako.

Haya yote hufanyika chini ya kivuli ya kile kinachoitwa “kuzoeana kitabia” kabla ya kuishi pamoja kaitka maisha ya ndoa. Desturi hii na yaliyomo ndani ya desturi hii hayakubaliki na hayana nafasi kabisa katika uislamu.

Haijuzu kwa mujibu wa sheria mchumba kuzungumza na mchumba wake hata kwa njia ya simu seuze kutokana na matembezi kukaa nae faraghani bila ya kuwepo baina yao maharimu wa mtoto wa kike kama vile Babu, baba au kaka.

Kisheria kijana wa kiume anaruhusiwa kumuangalia mtoto wa kike uso na mikono anapotaka kumposa bila ya kumgusa na hili hufanyika mbele ya wazazi wa pande zote mbili.

Hekima ya mkutano huu na kuonana huku ni kuwapa vijana hawa fursa ya kumuona yule atakayekuwa mwenza wake katika maisha na pia kuamua kukubali kuoa au kuolewa ama kukataa. Hili tu ndilo linaloruhusiwa na sheria.

Baada ya kuonana huku, wachumba hawa hawana ruksa ya kuzugumza au kuonana tena mpaka watakapooana kwa misingi na taratibu zote za kisheria ambapo binti sasa hutambulika kama mke wa mtu na kijana kama mume wa mtu.

Yaliyozuliwa na watu kinyume na utaratibu huu tuliowekewa na sheria ni HARAMU isiyokubalika na yenye adhabu kali mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na athari yake mbaya kwa jamii.

Uzoefu umeonyesha na kuthibitisha kuwa ada hii ya “kuzoeana kitabia” katika hatua ya uchumba imefanya ndoa nyingi zisifungwe.

Kijana wa kiume akishapata nafasi ya kukutana na binti na kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa, matokeo yake ni kumtia mimba mtoto wa kike. Baada ya mimba hupatikana mojawapo ya mambo mawili haya:

  1. Ama kijana ataukubali mzigo wake ule, akalea mimba na wakaja kufunga ndoa baadaye wakiwa na mtoto wa haramu/njeya ndoa.
  2. Au ataukana mzigo ule uwa si wake na hivyo kumuacha mtoto wa kike ahangaike na kuteseka pake yake naye akashika nia kwenda kuendeleza fisadi na uharibifu wake mahala pengine.

Sasa ili ili kuzuia haya yote yasitokee, ndio uislamu ukaamua kuufunga kabisa mlango huu wa fisadi na uharibifu kwa maslahi yetu wenyewe.

Tufuatane pamoja katika hadithi ifuatayo ya Bwana Mtume, ili tuone jinsi uislamu ulivyoharamisha mwanamume kumuangalia mwanamke ajnabia (wa kando na kando – yaani si maharim wa mwanamume yule):-

Imepokelewa na Umu Salamah – Allah amuwiye radhi – amesema: Nillikuwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – akiwa na Maimunah (mkewe), akaja/akaingia Abdullah Ibn Ummi Maktuum (kipofu).

Na hili lilikuwa baada ya kushuka aya za hijabu, akatuambia Mtume; “Jificheni nae,” tukamwambia; Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, yeye si kipofu ? Hatuoni na wala hatujui ? Mtume akatuambia; “Je! Na nyinyi ni vipofu, hamumuoni ?” Abuu Daawoud na Tirmidhiy.

Haya, ikiwa huyu ni kipofu haoni na bado Bwana Mtume anawaamrisha wakeze waondoke mbele yake, wasimuone kwa kuwa ni mwanamume.

Vipi leo, vijana wetu wa kike na wa kiume ambao wote wawilli si vipofu wanaona wakae pamoja wakitazamana na kuzungumza kwa tabasamu pevu na vicheko vya furaha.

Ruksa hii na uhalali huu wanaupata wapi na il-hali Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuonya;

“Asikae faragha mmoja wenu pamoja na mwanamke ila (atakapokuwa mwanamke huyo) pamoja na maharimu wake.” Bukhaary na Muslim. Bwana Mtume, anatukataza katika hadithi hii kukaa faraghani (yaani mwanamume na mwanamke peke yao tu) pamoja na mwanamke ambaye si maharimu yetu.

Mwanamke asiye maharimuni yule ambaye kisheria hakuna kizuizi wala kipingamizi chochote kwetu kumuoa.

Haya ni maelekezo, maagizo na amri ya Bwana Mtume ambayo sisi kama waislamu tunapaswa bali imetulazimu na kutuwajibikia kuifuata na kiutekeleza mara moja bila ya kuzitii na kuzifuata amri na maelekezo ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie.

Na ni vema ikatiwa akilini kuwa kumtii na kumfuata Bwana mtume ni amri ya mwenyezi mungu mtukufu, tusome na tutekeleze.

“………………NA ANACHOKUPENI MTUME (ANACHOKKUAMRISHENI BASI POKEENI), NA ANACHKUKATAZENI JIEPUSHENI NACHO …………………” (59:7)

Tusome tena kwa mazingatio na kasha tufuate:

“SEMA: IKIWA NYINYI MNAMPENDA ALLAH, BASI NIFUATENI; (HAPO) ALLAH ATAKUPENDENI NA KUKUGHUFIRIENI MADHAMBI YENU” (3: 31)

Aya hizi na nyinginezo ndizo zinazotulazimisha kumfuata na kumtii Bwana Mtume katika maelekezo, maamrisho au makatazo yote atakayotupa kwa maslahi na manufaa yetu wenyewe.

 Kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu mtukufu ametukamilishia dini hii kupitia kwa Mtume wake.

Dini hii haikusaza lolote lenye manufaa na faida kwetu katika maisha haya ya dunia na yale yajayo ya akhera ila imetueleza jambo hilo na namna ya kulitekeleza.

Kadhalika haikuacha lolote lile lenye madhara na kasoro kwetu ila imetuabainishia na kututahadharisha nalo na kutuonya tusilitende au kulifuata.

Sasa ikiwa dini hii imekamilika na kila jambo linalohusu nyanja mbalimbali za maisha yetu ya kila siku limekwisha bainishwa na kuwekewa utaratibu wake wa kulitekeleza au kulienda. Kwenda kinumbe na utaratibu huo, kunamaanisha:

  1. Dini hii haikukamilika kama anyavyosema Mwenyezi Mungu mtukufu
  2. Kumkadhibisha mwenyezi mungu na Mtume wake, jambo ambalo ni maasi.
  3. Sisi tunayo mamlaka na madaraka ya kujitungia sheria kinyume na sheria za Mwenyezi Mungu mtukufu.
  4. Tuna uamuzi na khiyari ya kufuata ama kutokufuata sheria/ hukumu za Mwenyezi Mungu mtukufu.
  5. Sheria na taratibu zetu tulizojipangia ni bora na zinafaa zaidi kuliko zile za mwenyezi mungu
  6. Kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Kwa ujumla kutokumfuata Bwana Mtume ni kumhalifu na kumpinga, jambo ambalo Mwenyezi Mungu mtukufu ametukataza tusome na tuzingatie:

“ …………….BASI WAJIHADHARI WALE WANAOKAIDI AMRI YAKE USIJE UKWAPATA MSIBA AU UKAWAFIKA ADHABU IUMIZAYO.” (24: 63)

Leo kwa sababu ya ukaidi na kukhalifu kwetu amri ya Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie- na tukaruhusu mila na desturi hii ya kuzoeana tabia iitawale jamii yetu, tayari tumeshafikwa na kupatwa na msiba.

Msiba huu si mwingine bali ni wimbi na janga la watoto wa haramu/nje ya ndoa na pengine hata hawa tuwaitao leo watoto wa mitaani ni natija ya kuendekeza na kufuata mila tamaduni n a desturi hizi mbaya. Taathira na athari na ada hizi potofu ziko wazi na bayana kwa kila mmoja wetu.

Haya sasa ndugu zanguni waislamu, tuamue ama kumfuata Bwana Mtume tupate salama au kutokumfuata na kuendeleza mila tamaduni na ada zetu wenyewe tufikwe na msiba na adhabu kali iumizayo.

Mwisho ni vema tukakumbuka na kukiri kuwa hizi ni hasaha za wiki, kunasihika au kutonasihika huo ni uamuzi wako wewe mwenyewe. 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *