VITENGUZI VYA UDHU

Haya ni yale mambo ambayo mojawapo miongoni mwake likimtokea/kumpata mtu mwenye udhu, litasababisha kubatilika kwa udhu wake huo na kuhesabika mbele ya sheria kuwa ni MUHDITH (hana udhu).

Kwa mantiki hii itamuwajibikia kutawadha tena ikiwa anataka kuyatenda yale ambayo kisheria haruhusiwi kuyatenda pasina udhu. Vitenguzi vya udhu ni vitano kama ifuatavyo :

1. Kila kilichotoka katika mojawapo wa njia mbili; ya mbele au ya nyuma.

    Ni sawasawa hicho kilichomtoka ni mkojo, mavi, damu au ushuzi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu :

     “…..AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI ….” [5:6],[4:43]

    Yaani ametoka kukidhi haja yake. Naye Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – amesema: 

    “Allah haikubali swala ya mmoja wenu atakapohuduthi (atakapotengukwa na udhu) mpaka atawadhe (tena)”

    Mtu mmoja wa Hadharamout (Mji katika Yemen-aliyekuwepo wakati Abuu Hurayrah akiipokea hadithi hii) akauliza : Hiyo hadathi (iliyotajwa katika hadithi) ni nini ?, Akajibu ni ushuzi.

    TANBIIH: Kisia/kadiria kwa haya yaliyotangulia kila kitokacho katika tupu ya mbele au nyuma, hata ni twahara kilichotoka.

    2. Kulala usingizi mzito ambao kuwa anakuwa hana hisia kabisa na akawa amelala pasina kuyaambatisha matako yake na ardhi, kiasi cha kuruhusu chochote kuweza kumtoka bila kuhisi khasa ushuzi.

    Ushahidi wa hili ni kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie

    “Atakayelala (akiamka) basi na akatawadhe”  Abuu Daawoud na wengineo.

    Ama ule usingizi mwepesi ambao mtu anakuwa anazo hisia zake na akawa amekaa mkao wa kuwambisha matako yake na ardhi, huu hautengui udhu kwa sababu atahisi kitakachomtoka.

    Ushahidi wa hili ni riwaya ya Anas ibn Maalik –Allah amuwie radhi – isemayo: ilikimiwa swala na il-hali Mtume –Rehema na Amani zimshukie – akinong’ona na mtu, akaendelea kunong’ona naye mpaka wakalala maswahaba wake, kisha (Mtume) akaja na kuwaswalisha. Muslim.

    Itabainika kutokana na riwaya hii kwamba Maswahaba walilala hali ya kuwa wamekaa mkao wa uwambishaji.

    Hii ni kwa sababu walikuwa msikitini wakingojea swala huku wakitumai kuwa Bwana Mtume atakata mazungumzo yake na kuja kuswalisha.

    3. Kuondokewa/kutokwa na akili kwa sababu ya uwendawazimu, kuzimia, kulewa (kwa namna yoyote ile iwayo) au kwa kutumia madawa ya kulevya. Ni mamoja ikiwa alitumia vitu hivi kwa kukusudia au bila ya kusudia, udhu utatenguka tu.

    Hii ni kwa sababu vitu hivi huiondosha akili ya binadamu na hivyo kumfanya akose hisia za kuweza kutambua kinachomtokea. Hii inakadiriwa na kulala.

    4. Mwanamume kumgusa mkewe au mwanamke wa kando pasina kizuizi, yaani wamegusana ngozi kwa ngozi, hapo utatenguka udhu wa wote wawili; mgusaji na mguswaji.

    Mwanamke wa kando, huyu ni kila mwanamke ambaye kisheria ni halali kumuoa, hakuna uharamu baina yao. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu

    “….AU MMEWAGUSA WANAWAKE…” [4:43]

    5. Kugusa utupu (uchi) wake au wa mtu mwingine hata kama ni mtoto mdogo au maiti kwa matumbo ya kiganja chake au matumbo ya vidole vyake pasina kizuizi. Dalili juu ya hili ni kauli ya Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie

    “Atakayeigusa dhakari yake, basi asiswali mpaka akatawadhe (tena)”  Tirmidhiy.

    One thought on “VITENGUZI VYA UDHU

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *