VITENGUZI VYA TAYAMAMU

Tayamamu hutenguka na kubatilika kwa kupatikana mambo yafuatayo:

  • Mambo yote yanayotenguka na udhu tuliyoyataja katika mlango wa udhu (rejea).
  • Kupata maji baada ya kuyakosa. Hii ni kwa sababu kutayamamu ni badala ya maji, kwa mantiki hii itakapopatikana asili (maji) hubatilika badala (tayamamu).

Haya ndiyo mafundisho ya Uislamu kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Abu Dharri –Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – amesema: “Hakika udongo (mchanga) ulio safi ni tahara ya muislamu hata kama hakupata maji kwa miaka kumi. Atakapoyapata maji basi na ajitwaharishe nayo kwani kufanya hivyo ndio bora” Abuu Daawoud. Hadithi hii inafahamisha kubatilika kwa tayamamu kwa kupatikana maji

TANBIHI:

1. Mtu akiyapata maji baada ya kumalizika kwa swala (baada ya kuswali), swala yake itakuwa ni sahihi na haimpasii wala kumuwajibikia kuikidhi swala hiyo. Kadhalika lau atayapata maji baada ya kuanza kuswali, basi na aikamilishe swala nayo itakuwa ni sahihi.

Lakini katika hali hii ni vema zaidi iwapo ataikata swala ili atawadhe na kuswali kwa udhu. Atafanya hivyo ikiwa muda upo wa kutosha kutawadha na kuswali ndani ya wakati yaani kabla ya kutoka wakati wa swala husika.

2. Uwezo wa kuyatumia maji. Hili ni kwa mtu aliyekuwa mgonjwa na akashindwa kutumia maji katika udhu au josho. Huyu akipona, hana tena ruhusa ya kutayammamu kwa sababu ya kuondoka jambo lililompa uhalali wa kutayamamu ambalo ni ugonjwa.

3. Kuritadi yaani kutoka katika Uislamu – tunamuomba Mola wetu Mtukufu atukinge na hilo.

TUJIFUNZE NA TUKUBALI:
Kuwa Uislamu hautekelezeki ila kwa kupitia mafundisho sahihi. Mafundisho hayo hayafahamiki ila kwa kusoma. Haya shime tusome kwa bidii ili tuweze kuutekeleza vema uislamu wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *