“Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini” Hadith Tukufu
Maji kwa kuzingatia sifa na hukumu zake yanagawanyika sehemu/mafungu matatu:-
1: MAJI TWAHUUR au MAJI MUTLAQ hili ndilo fungu la kwanza la maji. Haya ni maji yenye sifa mbili kuu:-
a/ Yenyewe ni twahara.
b/ Yana uwezo wa kutwaharisha.
Maji yenye sifa hizi ni kama vile maji ya mvua, bahari, maziwa, mito, chemchem na visima. Maji haya yatafaa kutumika katika twahara muda wa kubakia katika jumbile lake la asili bila ya kubadilika mojawapo ya sifa zake tatu ambazo ni:-
i/ rangi
ii/ Tamu (ladha) na
iii/ Harufu (riha)
Hukumu ya maji haya ni kwamba yanaondosha hadathi zote mbili; kubwa na ndogo, na najisi. Maji haya pia hutumika kwa kunywa, kufulia, kupikia, na shughuli nyingine za maisha ya kila siku ya mwanadamu.
2: MAJI TWAHARA: Haya ni maji ambayo yana sifa moja tu ya kuwa yenyewe ni twahara lakini hayana uwezo wa kutwaharisha. Haya ni maji twahara ambayo yamechanganyika na kitu kilicho twahara kama vile sabuni, sukari, zafarani, unga, asali au maziwa na kitu hiki kikaharibu moja wapo ya sifa zile tatu za maji yaani rangi, ladha au harufu. Kuharibika huku kwa mojawapo ya sifa za maji ndiko kunakoyanyang’anya maji vile uwezo na nguvu yake ya kutwaharisha.
Hukumu ya maji haya: yenyewe ni twahara na yanaweza kutumika katika matumizi mengine yote ya mwanadamu kama vile kunywa, kuoshea vyombo na kadhalika ila hayawezi kutumiwa katika suala zima la twahara kama vile kuondosha hadathi ndogo (kutawadha),hadathi kubwa (kukoga) na kuondosha najisi.
3: MAJI NAJISI: Haya ni maji yaliyonajisika kwa kuingia ndani yake najisi itakayoharibu mojawapo ya zile sifa tatu za maji.
Hukumu ya maji haya ni kutokufaa kutumika katika twahara na matumizi mengine ya kila siku ya mwanadamu.
vi/ MGAWANYIKO WA MAJI KWA KUZINGATIA WINGI NA UCHACHE
Tukiyaangalia maji kwa kuuzingatia wingi na uchache wake tutayakuta yamegawanyika sehemu/mafungu mawili:-
i/ maji mengi, na
ii/ Maji machache
i/ MAJI MENGI: Haya kwa mtazamo wa sheria ni yale yaliyofikia kullatein na zaidi yake. Kullatein ni miongoni mwa vipimo vilivyokuwa vikitumiwa na Waarabu zamani. Kwa vipimo tuvitumiavyo leo kullatein ni sawa na lita 216 za ujazo. Kwa vipimo vya ukubwa Kullatein ni sawa na dhiraa moja na robo upana, urefu na kina. Dhiraa moja ni sawa sawa na sentimeta 48 (48 cm)
HUKUMU YA MAJI MENGI: Maji yaliyofikia kullatein na kuendelea hayanajisiki kwa kuingia tu najisi ndani yake bali ya kuwa yamenajisika ikiwa najisi hiyo itaharibu mojawapo ya zile sifa tatu za maji.
ii/ MAJI MACHACHE: Maji yatahukumiwa kuwa ni machache ikiwa hayakufikia kiwango cha kullatein yaani yako chini ya lita 216 za ujazo ambazo ni karibu ya madebe 12 yaliyojaa.
HUKUMU YA MAJI MACHACHE: Maji haya yatanajisika kwa kuingiwa na najisi hata kama najisi hiyo haikuharibu mojawapo ya sifa za maji, na yatahukumiwa kwa mujibu wa sheria kuwa ni maji najisi na tayari tumekwisha itaja hukumu ya maji najisi huko nyuma.