1) MAANA YA ADHANA:
Adhana ni neno la Kiarabu lenye maana mbili; maana ya kilugha na maana ya kisheria (kifiq-hi). Kilugha neno adhana lina maana ya “tangazo” kama lilivyotumika ndani ya Qur-ani Tukufu:
“NA NI TANGAZO (adhana) LITOKALO KWA ALLAH NA MTUME WAKE, KUJUVYWA WATU SIKU YA HIJA KUBWA KWAMBA ALLAH YU MBALI NA WASHIRIKINA…..” (9:3)
“NA (tukamwambia): UTANGAZE (uadhini) KWA WATU HABARI ZA HIJA….” (22:27)
Ama maana ya adhana kisheria ni dhikri (utajo) maalum iliyowekwa na Uislamu kwa ajili ya kutangaza kuingia kwa wakati wa swala ya fardhi na kuwaita waislamu kuja kuswali.
1. HUKUMU YA ADHANA:
Adhana ni suna kwa swala ya sasa (ya wakati huu) na swala iliyofutu (inayoswaliwa nje ya wakati wake).
Kwa upande wa swala inayoswaliwa kwa jamaa adhana inakuwa ni SUNA KOKOTEZWA (Muakadah) kwa anjia ya kutoshelezeana.
Yaani akiadhini mmoja miongoni mwao atakuwa amewatoshelezea wengine wote na suna hii, kwa hivyo haitalazimu kutolewa adhana nyingine.
Ama kwa mtu anayeswali peke yake, yeye mwenyewe tu bila ya kuwa na wa pili yake, kwake huyu adhana itakuwa ni SUNA AINIYAH (yenye uzito wa fardhi).
Adhana ina umuhimu mkubwa na uzito wa pekee katika kudhihirisha alama za kuadhimisha dini ya Allah.
2. FADHILA ZA ADHANA:
Zimepokelewa hadithi kadhaa kutoka kwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – zinazofahamisha fadhila na thawabu adhimu zinazopatikana ndani ya adhana.
Miongoni mwa hadithi hizo ni kama zifuatavyo:
1. Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah amuwiye radhi kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – amesema:
“Lau watu wangelijua yaliyomo katika wito (adhana) na safu ya kwanza (ya swala ya jamaa) (yaani fadhila na thawabu adhimu zinazopatikana humo). Kisha wasipate (fursa hizo) ila kwa kupiga kura, basi wangelipiga kura.”
Bukhaariy & Muslim
2. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Said Al-khudriy- Allah amuwiye radhi – amesema: Amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie:
“Utapokuwa katika (kundi la) mbuzi na kondoo wako (malishoni) au (utapokuwa) kitongojini mwako, ukaadhini kwa sababu (ya kuingia wakati wa) swala. Basi inyanyue sauti yako kwa wito huo (adhana) kwani hakika haisikii sauti ya muadhini jini wala mwanadamu wala kitu cho chote ila (sauti hiyo) itamshuhudia (mtu huyo) siku ya kiyama.”
Bukhaariy
3. Amesema Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie:
“Bora ya waja wa Allah ni wale wachungao jua, nyota na vivuli (waadhini) kwa ajili ya dhikri ya Allah (swala).” Al-Haakim
3. DALILI NA USHAHIDI WA ADHANA:
Adhana inapatikana ndani ya Qur-ani Tukufu na suna ya Mtume. Katika Qur-ani adhana inapatikana katika kauli ya Allah:
“ENYI MLIOAMINI! KUKIADHINIWA KWA AJILI YA SWALA SIKU YA IJUMAA, NENDENI UPESI KUMTAJA ALLAH NA ACHENI BIASHARA….” (62:9) Na katika kauli ya Allah: “NA MANAPOITA KWENDEA SWALA (mnapoadhini) WANAIFANYIA MZAHA NA MCHEZO. HAYO NI KWA SABABU WAO NI WATU WASIO NA AKILI.” (5:58)
Katika suna ya Mtume, adhana inaelezewa na kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie:
“Unapoingia wakati wa swala, basi na akuadhinieni mmoja wenu na akuswalisheni aliye mkubwa wenu.” Bukhaariy & Muslim
Kutokana na nukuu hizi za kitabu (Qur-ani) na Sunah (hadithi) uma wa Kiislamu umekongamana juu ya kwamba adhana imeshariiwa kwa swala tano za fardhi ili kuwajulisha waislamu kuingia kwa wakati wa swala husika.