Hii ni mila na desturi iliyoenea na kufuatwa na makabila mengi khusasan hapa kwetu Tanzania. Unyago ni mila ya kumcheza mtoto wa kike wakati avunjapo ungo.
Wakati huo huandaliwa ngoma maalum ambayo huwashirikisha akina mama watu wazima.
Hawa kazi yao kubwa ni kile kinachoitwa “kumfunda” mwanamwali, yaani kumfahamisha kuwa sasa yeye amekuwa mwanamke na kumealeza nafasi yake kama mwanamke, majukumu yake na jinsi ya kuishi na mume.
Ngoma hii huchezwa mahala pa wazi, mahali ambapo hata mwanamume hupata fursa ya kuwaona wanawake, wake za watu wakikata viuno. Mahala hapa, mwanamwali huonyeshwa akiwa kavishwa khanga ya kiuno tu na baki ya mwili wake kuachwa wazi ikiwa ni pamoja na matiti yake.
Katika ngoma hii wanawake hunywa pombe ili kutoa aibu na haya wapate kukata viuno vizuri, na baadhi au wengi washirikio katika mila hii hujiita kuwa ni waislamu.
Waelewe uislamu hakuna mila kama hizi mbaya na kushikilia kuzifuata na kuziendeleza desturi hizi huku wakivaa vazi la uislamu, huko ni kuudhalilisha na kuutukanisha uislamu.
Mila na desturi hizi huzifai kwa kuwa zinapingana na sheria kamilifu ya Mwenyezi Mwenyezi Mungu, kwa hivyo tuziache mara moja pamoja na kuzizoea na kuzionea ladha kwetu. Mila hizi hazifai kwa sababu zifuatazo:
- Unyago huwashirikisha mwanaume na wanawake, kama tushuhudiavyo leo. Katika uislamu ni kosa kubwa mwanamume kuchanganyika na wanawake.
- Katika unyago huimbwa nyimbo za matusi, hili halikubaliki hata kiakili na kimaadili seuze sheria .
- Katika unyago watu hulewa eti kwa sababu ya kumsherekea mtoto wao. Uislamu umekataza ulevu kwa sababu yoyote ile iwayo, hata kama ni dawa kama wanavyodai hivyo baadhi ya watu.
- Mwanamwari hudhalilishwa na kunjiwa heshima yake kama mwanadamu kwa kuanikwa uchi mbele ya hadhara ya watu wakiwemo mwamume.
- Katika unyago hupatikana matumizi mabaya ya mali. Pesa ambazo zingetumika katika mambo mengiya maendeleo kwa maslahi ya jamii na familia husika, hutumika kununulia pombe, kuwalipa wapiga ngoma na kugharimia chakula cha wanangoma kwa kipind chote cha ngoma. Hii ndio israafu inakemewa na kukatazwa na uislamu.
Kwa ujumla, huzalikana na kupatikana katika desturi na mila hii ya unyago, mambo mengi ambayo yanakhalifiana na sheria.
Kwa mantiki hii kila aliyekuwa muislamu anpaswa kuziacha mara moja mila na desturi hizi ili awe muislamu kamili.
Uislamu haupingi wala kulikataa suala la kumfundisha mtoto wa kike/kiume nafasi yake yeye kama mwanamume/mwanamke na majukumu yake kama mke kwa mumewe au mume kwa mkewe. Aishi vipi na jamii, ailee vipi familia.
Uislamu unapinga na kukataa namna au njia na jinsi itoleavyo elimu hii. Uislamu umesheheni fani zote za elimu iwe na elimu ya kijamii, uchumi, afya, ulinzi na usalama, siasa na kadhalika, zote hizi zimo ndani ya uislamu, tusome tu tutakutana nazo.
Sasa kama elimu hii tunayo, kwa nini hatujifunzi na kuitoa kwa misingi yetu ya kiislamu?! Jamani , tuziache mila, desturi na ada hizi potofu na badala yake tushikamane na kuifuata mila na desturi sahihi za uislamu. Uislamu ndio mila baba yetu Nabii Ibrahimu- Rehema na Amani zimshukie, tusome:
“…..(Nayo dini hii) NI MILA YA BABA YENU IBRAHIMU….”[22:78]
Hivi ni kweli kuwa leo sisi tunaweza kuwa na mila na desturi bora kuliko mila ya Nabii Ibrahimu?! Kuacha kufuata mila ya Baba yetu Ibrahimu na kujiundia mila zetu wenyewe huo ni UPUMBAVU, tusome na tukubali:
“NA NANI ATAJITENGA NA MILA YA IBRAHIMU ISPOKUWA ANAYEITIA NAFSI YAKE KATIKA UPUMBAVU…”[2:130]