Wakati ni suala lenye umuhimu wa pekee katika maisha ya muislamu. Umuhimu huu unatokana na mtizamo wa Uislamu kwa wakati kuwa ndio maisha/uhai wenyewe.
Kwani hizi sekunde,dakika, saa, siku,juma,mwezi na hatimaye mwaka hazimaanishi ila umri wa mwanadamu na kumalizika kwake. Uislamu unaithamini na kuidhibiti kila dakika inayompitia mwanadamu na umemuwekea dhana ya kuhesabiwa juu ya dakika yake hiyo ambayo haiwakilishi ila uhai wake.
Huu ndio mtizamo na msimamo wa Uislamu kuhusiana na suala zima la wakati;mtizamo unaokinzana na mtizamo wa wale wanaodai kuwa ni waislamu,khususan waislamu wa leo. Waislamu wa leo wanashindana katika kuupoteza pasipo na faida wakati wao kwa njia mbalimbali.
Ushindani huu ndio uliozaa msemo shahiri utumikao leo, ambapo utamsikia mtu anasema: (Naenda kupoteza wakati). Msemo huu haumaanishi ila ni kuwa muhusika ana wakati (muda) kifaya(tosha) kuliko mahitaji yake, kiasi cha kutokujua autumieje huo muda wake wa ziada.
Hapo ndipo huamua kwenda kijiweni kwa wale vijana au kwenye baraza ya kahawa/karata/bao kwa wale wazee. Hivi kweli inamkinika kwa muislamu kuutumia hivi wakati wake na il-hali kitabu chake kitukufu ndicho kinachosema kwa ndimi za watu waovu watakaposema siku ya kiyama. Baada ya kupewa vitabu vya amali zao:
“NA MADAFTARI YATAWEKWA(mbele yao). UTAWAONA WABAYA WANAVYOOGOPA KWA SABABU YA YALE YALIYOMO (madaftarini) NA WATASEMA: OLE WETU! (Ee kuangamia kwetu leo!) NAMNA GANI MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYAYAMEHUDHURIA HAPO, NA MOLA WAO HAMDHULUMU YO YOTE”. [18:49]
Yatakayokuwamo ndani ya madaftari ya amali ya waja siku ya hesabu na malipo (kiyama) ni natija ya namna walivyoitumia neema ya wakati (uhai) waliopewa bure na Mola Muumba wao.Hapo ndipo unapodhihiri umuhimu wa wakati katika maisha ya muislamu bali mwanadamu.
Kumbuka ewe ndugu muislamu (Allah akuzindue) wakati ambapo wewe unauchezea na kuupoteza wakati (uhai) wako katika mambo yasiyokunufaisha bali kukudhuru.madola makuu (mataifa ya kikafiri) yanahakikisha kuwa yanaitumia vyema kila fursa ya dakika waipatayo kuitawala anga na bahari. Lengo kuu likiwa ni kukutawala wewe muislamu kijeshi, kiuchumi, kielimu, kiutamaduni,kifikra na hata ikiwezekana kiitikadi pia.
Hebu pekua kurasa za historia (tarekh) uone ni jinsi gani waislamu wa mwanzo walivyojua umuhimu wa wakati (uhai). Na namna walivyoupa thamani yake na wakati ukawathamini na kuwapa thamara (matunda) yake.
Miongoni mwa thamara hizo ni elimu yenye manufaa inayotunufaisha hata sisi leo,amali njema zilizowahakikishia utukufu na daraja za juu mbele ya Mola wao na ulimwengu mzima wa kiislamu muda wa kusalikia mbingu na ardhi. Jihadi yenye kukubaliwa na Allah iliyoueneza Uislamu mashariki na magharibi.
Ni kutokana na jihadi yao hiyo njema ndio na akina sisi tukapata bahati ya kuwa waislamu-Alhamdulillah! Ustaarabu uliowabakishia utu na ubinadamu wao hata wakawa ni kigezo kwa watu wa jamii nyingine na nembo yao ikawa ni ile dua iliyosajiliwa na Qur-ani:
“…MOLA WETU! TUPE MEMA DUNIANI NA (tupe) MEMA AKHERA, NA UTULINDE NA ADHABU YA MOTO”. [2:201]
Haya ni baadhi tu ya matunda waliyoyapata waislamu wa mwanzo kutokana na kuuthamini na kuutumia vema wakati.
QUR-ANI NA SUNAH (HADITHI) ZINAVYOUTHAMINI NA KUUSHUGHULIKIA WAKATI.
Kabla hatujaanza kuliangalia hili kwa pamoja, ni vema tukafahamu kwamba Uislamu unamtaka muislamu aushughulikie ulimwengu wake huu aishimo leo kama kwamba ataishi milele, hatokufa abadan.
Maana na tafsiri sahihi ya agizo hili la Uislamu ni kuwa muislamu ajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili aishi maisha mazuri na asiwe tegemezi na mzigo kwa jamii. Maisha ambayo yatamuhakikishia kupata mahitaji yake yote ya lazima; ale, anywe , alale mahala pazuri na apate elimu bora sambamba na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa dini yake.
Huu ni upande mmoja, kwa upande wa pili Uislamu unamuagiza muislamu kuishughulikia akhera yake, mahala ambako ndiko yaliko maisha yake ya milele, kama kwamba atakufa kesho. Tafsiri safi ya agizo hili ni kuwa muislamu anatakiwa asighurike na dunia ipitayo kiasi cha kuisahau akhera iliyo makazi yake ya milele.
Baada ya kukumbushana juu ya agizo hili la Uislamu; dini ya maumbile, hebu sasa na tuanze kuiangalia Qur-ani Tukufu inavyoutazama wakati na umuhimu wake, tusome na tuzingatie pamoja:
“NA AKAKUTIISHIENI JUA NA MWEZI, MAISHA YAO (yanafanya yaliyoamrishwa ya kuchomoza na kuchwa na mengineyo kwa ajili ya manufaa yenu) NA AKAKUTIISHIENI MCHANA NA USIKU NA AKAKUPENI KILA MLICHOMUOMBA (na msichomuomba). NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU…” [14:33-34]
Hapa Allah Mola Mtukufu anamkumbusha mwanadamu kuwa miongoni mwa neema zake nyingi alizomneemesha ni pamoja na neema ya jua na mwezi. Neema mbili hizi ndizo mihimili mikuu na chanzo cha kuhesabia wakati ambacho hutupatia usiku na mchana. Allah anazidi kutukumbusha juu ya neema hii ya wakati, hebu tumtegee sikio la usikivu:
“NAYE NDIYE ALIYEFANYA USIKU NA MCHANA UFUATANE KWA (nafuu ya yule) ANAYETAKA KUKUMBUKA AU ANAYETAKA KUSHUKURU (atatanabahi kwa kuja na kuondoka kwa mchana na usiku)”. [25:62]
Mfuatano wa mchana na usiku; yaani usiku ukaondoka na mahala pake pakachukuliwa na mchana na kinyume chake ni katika jumla ya neema za Allah zilizo kwa mwanadamu. Haukuwa usiku na mchana ila ni wakati ambao humpa mwanadamu fursa ya kufanya amali zitakazomdhaminia kheri na mafanikio ya ulimwengu huu na ule ujao.
Nafsi ya kufuatana kwa mchana na usiku hakupungui kuwa ni neema ambayo mwanadamu anawajibika kuishukuru. Kwani kila kimoja mbali ya kuwa kwake ni wakati (uhai) kina jukumu na manufa yake kwa mwanadamu ambayo mwenzake hawezi kuyatekeleza.
Lau ingelikuwa ni usiku tu milele bila ya mchana au ni mchana daima bila ya usiku, maisha yangelimwia uzito mwanadamu, bali yasingeliwezekana kamwe. Na hii ndio sehemu tu ya hekima na falsafa ya kauli tukufu ya Allah:
“SEMA: NIAMBIENI, KAMA ALLAH AKIUFANYA USIKU UKUKALIENI MOJA KWA MOJA MPAKA SIKU YA KIYAMA, NI MUNGU GANI ASIYEKUWA ALLAH ATAKAYEKULETEENI MWANGA? BASI JEE, HAMSIKII? SEMA: NIAMBIENI, KAMA ALLAH AKIUFANYA MCHANA KUKUKALIENI MOJA KWA MOJA MPAKA SIKU YA KIYAMA, NI MUNGU GANI ASIYEKUWA ALLAH ATAKAYEKULETEENI USIKU MNAOPUMUA HUMO? BASI JE, HAMUONI (ihsani za Allah)? NA KWA REHEMA ZAKE AMEKUFANYIENI USIKU NA MCHANA ILI MPUMUE HAPO USIKU NA MTAFUTE FADHILA ZAKE (hapo mchana) NA ILI MPATE KUSHUKURU”. [28:71-73]
Katika kuuonyesha umuhimu wa wakati Allah ameapa mianzoni mwa sura mbalimbali zilizoshuka Makkah kwa wakati au sehemu ya wakati, mithili ya kauli hizi:
“NAAPA KWA USIKU UFUNIKAPO (kila kitu) NA KWA MCHANA UANGAZAPO”. [89:1-2]
“NAAPA KWA MCHANA NA KWA USIKU UNAPOTANDA”. [93:1-2]
“NAAPA KWA ZAMA (zako ewe nabii Muhammad) KUWA BINADAMU YUKO KATIKA KHASARA”. [103:1-2]
Inajulikana kutokana na elimu ya tafsiri kwamba Allah Mteremshaji wa Qur-ani Tukufu anapoapa kwa cho chote miongoni mwa viumbe vyake. Hufanya hivyo ili kuvuta fikra na mtazamo wa waja wake kukielekea kitu hicho alichokiapia na wautanabahi utukufu, manufaa na athari ya kitu hicho katika maisha yao ya kila siku.
Suna ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie- haikubakia nyuma katika kusisitiza na kuonyesha thamani ya wakati. Na jinsi mwanadamu atakavyowajibika mbele ya Allah siku ya kiyama kuhusiana na neema hii ya wakati aliyopewa aliitumiaje.
Hata ikawa miongoni mwa maswali manne ya msingi atakayoulizwa mja siku hiyo ya hesabu, mawili yanahusika moja kwa moja na wakati. Imepokelewa kutoka kwa Muaadh Ibn Jabal-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume- Rehema na Amani zimshukie- amesema: “Hazitaondoka nyayo (miguu) za mja siku ya Kiyama (kuingia peponi/motoni)mpaka aulizwe mambo manne:
i. Umri wake ameumaliza katika mambo gani.
ii. Ujana wake ameuchakaza katika mambo gani.
iii. Mali yake ameichuma katika njia gani (za halali/haramu) na aliitumiaje.
iv. Na elimu yake ameifanyia nini”.
Bazzaar & Twabaraaniy
Hivi ndivyo atakavyoulizwa mwanadamu kuhusiana na umri wake kwa ujumla na khasa ujana ambao ni sehemu ya huo umri. Kwa nini ujana na sio utoto au uzee? Hili linatokana na umuhimu wa kipindi cha ujana katika umri mzima wa mwanadamu.
Kipindi hiki kina nafasi na thamani ya pekee katika uhai wote wa mwanadamu kwani hiki ndicho kipindi cha harakati na joto la maisha. Hiki ndicho kipindi cha mvuto na matamanio, kijana anaupenda ulimwengu nao unampenda.
Ni kipindi ambacho kijana anakuwa katika mtihani mkubwa wa kuyashinda majaribu na matamanio ya kimwili na kimali. Akifaulu kuvuka katika kipindi hiki ndio kafaulu katika maisha yote.
Ujana ni kipindi cha mpito cha nguvu/harakati kilicho baina ya vipindi viwili vya udhaifu. Kipindi cha utoto, kipindi cha kutojiweza na kipindi cha utu uzima (ukongwe), kipindi tegemezi. Qur-ani Tukufu inavielezea vipindi hivi,tuitegee sikio:
“ALLAH NDIYE ALIYEKUUMBENI KATIKA UDHAIFU (wa tumboni kwa mama na utoto baada ya kuzaliwa) NA BAADA YA UDHAIFU (huo) AKAFANYA NGUVU (za ujana), KISHA BAADA YA NGUVU (hizo) AKAUFANYA UDHAIFU NA UZEE…” [30:54]