UMUHIMU WA SIRA YA MTUME WA ALLAH KATIKA KUUFAHAMU UISLAMU
Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-tambua na ufahamu ya kwamba si lengo la kusoma Sira, Falsafa na Mafundisho yake, kujua tu matukio ya kihistoria au kupata mfululizo wa visa na matukio yenye kuleta ladha masikioni na kuburudisha. Hilo silo lengo, bali lengo hasa la kusoma Sira na yaliyomo ndani yake, ni muislamu kupata taswira sahihi ya UHALISIA WA UISLAMU katika mjumuisho wake unao patikana kupitia maisha ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.
Tunalo kusudia kusema na kutaka lifahamike ni kwamba kusoma Sira ya Mtume, hakukusudiwi kingine zaidi ya kuwa ni UTENDAJI WA KIUTUMIZI ambao muradi/mapendeleo yake ni kuufinyanga UHALISIA WA UISLAMU ulio kamili, kupitia kigezo chema; Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na tukipenda kuyagawa makusudiwa hayo ili yapate kuwa karibu na ufahamu wa msomaji wetu, kunamkinika kuyafupisha katika malengo yafuatayo:
- Kufahamu shakhsiya (haiba, silka na hulka) ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia hatua tofauti tofauti za maisha yake na hali/mazingira aliyo ishi ndani yake. Ili kuthibitisha ya kwamba Muhammad hakuwa tu mtu bora aliye pata utukufu kwa kaumu yake kupitia ubora huo, lakini yeye pia alikuwa ni Mtume wa Allah aliye pata msaada na uwezeshi wa Mungu kupitia wahyi (ufunuo) kutoka kwake.
- Kupata Muislamu mbele yake sura/picha/taswira ya ruwaza (kiigizo) njema katika kila hatua na kipengele cha kadhia/masuala/mambo yote ya maisha bora, ili ajitwalie na kujitengenezea kutokana na sura hiyo, desturi na njia atakayo ifuata na kupita hata ikamfikisha salama kwa Mola Muumba wake. Na wala hapana shaka kwamba popote mwanaadamu atakapo tafuta ruwaza njema katika kipengele miongoni mwa vipengele vya maisha, hakika ataipata ruwaza hiyo kwenye maisha ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Tena ataipata ruwaza hiyo kwa kiwango cha hali ya juu kabisa ya uwazi na ukamilifu na ni kwa ajili/sababu hiyo basi, Allah akamfanya Mtume wake kuwa kiigizo kwa wanaadamu wote, pale alipo tuambia: “HAKIKA NYINYI MNAYO RUWAZA NJEMA KWA MTUME WA ALLAH…”. Al-Ahzaab [33]:21
- Kupata Muislamu kutokana na kuisoma kwake Sira ya Mtume wa Allah, uweledi na maarifa yanayo muwezesha kukifahamu kitabu cha Allah (Qur’ani) na kuonja kiini cha makusudiwa yake. Kwa sababu nyingi miongoni mwa aya za Qur’ani zinafasiriwa na kuwekwa wazi na matukio yaliyo mtokea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika maisha yake na namna alivyo kabiliana nayo.
- Kupata Muislamu tafsiri ya kiamalia na ubainifu wa kiutendaji wa dini ya Allah na maneno teremshwa yake ambayo yaliteremshwa na Roho Muaminifu; Sayyidna Jibrilu-Amani imshukie-kwenye moyo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Naye Bwana Mtume akayafikisha maneno hayo (Qur’ani) kupitia kauli zake na akayatekeleza kwa matendo yake. Kwa hivyo basi, maisha yake yote; kauli zake na matendo yake, harakati zake na tuo zake katika hali ya kuridhia na hali ya kughadhibika, katika hali ya kuwa macho na hali ya kulala, katika hali ya uchangamfu na hali ya unyong’onyevu, ni ubainifu wa wazi wa maneno hayo. Maisha yake yote ni tafsiri ya kiamalia ya dini ya Allah na maneno yake. Imepokewa kutoka kwa Yaziid bin Baabanuus-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tuliingia kwa Bi. Aysha, tukasema: Ewe Mama wa Waumini! Nini zilikuwa tabia za Mtume wa Allah? Akajibu: Tabia zake zilikuwa ni Qur’ani. Mnaisoma Surat Muuminina? Akasema: Soma (Qad aflahal-Muuminuuna). Yaziid akasema: Basi nikasoma Qad aflahal-Muuminuuna – mpaka (akafika katika kauli yake Allah) lifuruujihim haafidhwuuna. Akasema (Bi. Aysha): Hizo ndizo zilizo kuwa tabia za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie”. Bukhaariy-308 [AL-ADABUL-MUFRAD]
- Kumuiga na kumfuata Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ni suala la wajibu kwa kila Muislamu, na ni dhahiri ya kwamba Muislamu hawezi kumfuata asiye mjua na hawezi kumjua Mtume ila kwa kupitia kuisoma Sira yake. Na kumuiga na kumfuata Mtume ni dalili/kielelezo cha mapenzi ya mja kwa Mola Mlezi wake na kwa kitendo chake hicho, mja atapata kupendwa na Allah. Hilo ndilo analo lisema Allah kupitia kauli yake tukufu: “Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allah, basi nifuateni mimi, mtapendwa na Allah na atakufutieni madhambi yenu. Na Allah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu”.Aali Imraan [03]:31
- Kunapatikana ndani ya Sira ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mawaidha, mazingatio na hekima/falsafa anazo waidhika nazo na kuzizingatia kila mwenye afya ya akili, awe ni kiongozi au muongozwa.
- Kufahamu vema miujiza ambayo Allah aliionyesha kupitia kwa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-hakupatikani ila kwa kupitia matukio mbali mbali ambayo ndani yake ilitokea miujiza hiyo. Na yote hayo hayafahamiki ila kwa kuisoma Sira. Na kuifahamu miujiza hiyo ni jambo linalo izidisha na kuiimarisha imani ya Muislamu.
- Kukusanyika kwa Muislamu kutokana na kuisoma kwake Sira ya Mtume wa Allah, kiwango kikubwa kabisa cha utamaduni na maarifa sahihi ya Uislamu. Yawe ni yale yanayo fungamana na Akida (Itikadi), hukumu au akhlaaq (tabia), kwa sababu ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba maisha ya Mtume ni sura yenye umbile linalo zagaza nuru ya mjumuisho wa misingi na hukumu za Uislamu.
- Kupata mwalimu na muhubiri wa Uislamu mfano hai wa njia za malezi na ufundishaji/ufikishaji wa ujumbe. Kwani Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa ni mwalimu mnasihi (mtoa nasaha) na mlezi bora ambaye hakuchoka kutafuta na kuvumbua njia zenye kufaa katika kufikia malezi na ufundishaji bora katika hatua tofauti tofauti za mahubiri na mafundisho yake.
Na hakika kitu muhimu kabisa kinacho ifanya Sira yake Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kuwa yenye kutosheleza malengo yote haya tuliyo yataja na mengine mengi tusiyo yataja. Ni kwamba maisha yake Bwana Mtume yamekienea na kukifikia kila kipengele cha maisha ya mwanaadamu yale ya kibinafsi sanjari na yale ya kijamii yanayo mpitia katika uhai wake, akiwa kama mtu binafsi (yeye mwenyewe) au nguvu tendaji (kiongozi) katika jamii yake.
Kwa ujumla, maisha ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-yanatupa sisi kama umma wa Kiislamu mifano iliyo tukuka kwa:
- Kijana mwenye nyenendo na tabia njema, aliye mfano na kioo kwa jamii yake.
- Kiongozi kwa ngazi zote na raia/watu wake, anaye ujua vilivyo wajibu wake kwa anao waongoza.
- Muhubiri anaye wahubiria watu kwa hekima na mawaidha mazuri, anaye waleta karibu watu kwa Mola Muumba wao.
- Mume bora kwa familia yake, anaye ilea vyema familia yake kiroho na kimwili.
- Baba bora, mlezi na kiongozi wa familia yake, anaye hangaikia mafanikio ya familia yake duniani na akhera.
- Kamanda mahiri wa jeshi, anaye ingia mwenyewe kwenye medani ya vita kuhakikisha jeshi lake linapata ushindi,
- Mwanasiasa mkweli na hodari katika uongozi, anaye piga vita vitendo vya rushwa katika jamii yake.
- Muislamu aliye kusanya usahihi na uadilifu baina ya wajibu wa kuabudu na kujitupa kwa Mola Mlezi wake na tangamano jema na ahali (watu wake wa nyumbani; mke, watoto na watumishi) na maswahaba wake.
Naam, hayo kwa uchache ndio malengo na makusudiwa ya kulisoma somo hili muhimu; Sira ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Somo ambalo kila Muislamu anawajibikiwa kulisoma, kulielewa, kulifahamu vema na kisha kuyatumia aliyo yapata katika usomaji wake huo.
Juma lijalo kwa uwezeshi wake Allah, tutaanza rasmi kujifunza na kuisoma Sira yake Bwana Mtume chini ya anuwani: “SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”. Mola wetu Mtukufu turuzuku ufahamu utakao tuwezesha kumjua, kumfahamu, kumpenda na kisha kumuiga na kumfuata Mtume wako aliye tuambia katika jumla ya maneno yake: “Nimeletwa ili kukamilisha tabia njema”. Na mahala pengine akasema: “Nimeletwa kuwa mwalimu”.
Mpaka juma lijalo tunasema: Maa Salaamah!