UBORA WA ELIMU NA FAIDA YA KUSOMA

UBORA WA ELIMU

Elimu ndio pambo tukufu na lenye thamani kushinda/kuliko mapambo yote anayojipamba nayo mwanadamu.

Elimu ndio mwangaza na taa pekee inayomuangazia mwanadamu katika maisha ya ulimwengu huu.

Elimu ndio chombo pekee anachoweza kukitumia mwanadamu katika kumtii Mola wake, kwani kutokana na elimu ndipo mwanadamu huweza kujua halali na haramu na akapambanua baina ya lenye kunufaisha na lenye kudhuru.

Elimu ndio wasila na sababu ya msingi ya mtu kuweza kupata utukufu. Lau si elimu mataifa yasingeweza kupata maendeleo yaliyonayo leo, maendeleo ambayo hukua siku hata siku kwa sababu ya elimu.

Lakini lazima tutambue kwamba elimu pekee bila ya amali/vitendo haina maana, haisaidii chochote, kwani elimu haiwi elimu ila kwa kutumiwa kama walivyosema wanazuoni wema: {Elimu bila ya matendo ni kama mti usiotoa matunda}.

Mwenye kutaka kupata elimu ya ziada, pamoja na kufanya juhudi ya kusoma basi ajilazimishe sana kumcha Mwenyezi Mungu katika dhahiri na siri. Amesema Mwenyezi Mungu:

“NA MCHENI MWENYEZI MUNGU NA MWENYEZI MUNGU ATAKUELIMISHENI; NA MWENYEZI MUNGU NI MJUZI WA KILA KITU”(2:282)

Katika kuonyesha ubora na utukufu wa elimu Mwenyezi Mungu anatuambia:

“SEMA, JE WANAWEZA KUWA SAWA WALE WANAOJUA NA WALE WASIOJUA?..”(39:09)

Ili kusisitiza na kuonyesha ubora wa elimu ndipo Bwana Mtume akatuambia:{Kutafuta elimu ni faradhi ya lazima kwa kila muislamu: mwanamume na mwanamke}

 

UBORA/FAIDA ZA KUSOMA

Kusoma kuna faida nyingi sana. Bila ya shaka, elimu ndio huzisafisha na kuzitakasa nafsi za wanadamu, ikazirekebisha tabia zao mbaya na kuwaongoza katika njia ya kheri.

Kusoma ni miongoni mwa amali tukufu ambazo mja anaweza kujikurubisha nazo kwa Mola wake, kwani bila ya elimu watu wasingeliyajua mambo ya dini wala ulimwengu wao, bali wangeliyafuata matashi na matamanio ya nafsi zao.

Kutokana na sababu hizi na nyinginezo ndio Mwenyezi Mungu akawaletea wanadamu mitume ili waje wawafundishe yaliyo na manufaa kwao katika dini yao na ulimwengu wao. Mwenyezi Mungu hakuwaacha mitume waitekeleze kazi aliyowapa ya kuwaelimisha waja wake bila ya muongozo, bali aliwapa muongozo akawaagiza:

“WAITE(watu) KATIKA NJIA YA MOLA WAKO KWA HIKIMA NA MAWAIDHA MEMA NA UJADILIANE NAO KWA NAMNA ILIYO BORA… “(16:125) katika jumla ya faida za kusoma ni kufuzu kwa kupata daraja kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ulimwenguni. Amesema Mola Mtukufu:

“MWENYEZI MUNGU ATAWAINUA WALE WALIOAMINI MIONGONI MWENU; NA WALIOPEWA ELIMU WATAPATA DARAJA ZAIDI” (58:11)

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *