TWAHARA

Hii ndio sharti ya kwanza ya kusihi swala:  Twahara nni nini, tayari umekwishajifunza katika sura ya kwanza, somo la kwanza, rejea huko na utaona.

Twahara ambayo ni sharti ya kusihi swala imegawanyika katika matapo yafuatayo:-

 

ii.  Twahara ya mwili kutokana na hadathi .  mtu mwenye hadathi haisihi swala yake. 

Ni mamoja ikiwa ni hadathi ndogo ambayo ni ukosefu wa udhu au ni hadathi kubwa kama vile janaba.  Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie katika hadithi sahihi “Haikubaliiwi swala bila ya twahara – Muslim.

 

ii.    Twahara ya mwili kutokana na najisi.  

Rejea sura ya kwanza, somo la pili ili ujikumbushe maana ya najisi na aina zake. 

Kabla ya kuvaana na ibada ya swala ni lazima mtu ahakikishe kuwa mwili wake ni twahara, hauna najisi ya aina yoyote ile. 

Haya ndio tunayoyafahamu kutokana na kauli ya Bwana Mtume – rehema na Amani zimshukie: 

“Jiepusheni na mkojo kwani hakika sehemu kubwa ya adhabu (zimpatazo mja) kaburini ni kwa sababu ya kutojikinga nao”

Mkojo hapa unakuwa ndio kigezo na mfano wa najisi nyingine zote ambazo Mtume hakuzitaja hapa katika hadithi hii. 

 Bwana mtume Rehema na Amani zimshukie – alimwambia Bi. Fatmah Bint Abiy Hubaysh – Allah amuwiye radhi; 

Itakapokuja hedhi basi acha kuswali.  Ikikoma, basi jikoshe damu (jitwaharishe na uanze) kuswali”  Bukhaariy na Muslim.

 

iii.  Twahara  ya nguo kutokana na najisi. 

Haitoshi tu mwili kuwa na twahara usio na  najisi bali hapana budi nguo anazozivaa mwenye kutoka kuswali, pia ziwe ni twahara, zisiwe na najisi ya aina yoyote ile. 

Hivyo ndivyo tunavyoambiwa na Mwenyezi mungu Mtukufu kupitia kauli yake :

 NA NGUO ZAKO UZITWAHARISHE (74:4)   Haisihi swala ya mtu aliyeswali huku akiwa kavaa nguo yenye najisi isiyosameheka kisheria hata kama mwili wake utakuwa ni twahara.  

Imepokelewa kutoka kwa Abu- Hurayrah – Allah amuwiye radhi – Kwamba Bi., Khaulah Bint Yassar – Allah amuwiye radhi alimuendea Mtume na kumwambia :

 Ewe Mtume wa Allah mimi sina ila nguo  moja tu, nami ninapata hedhi katika nguo hiyo, basi nifanyeje?   (Mtume) akamwambia

“Utakapotwaharika ifue (itwaharishe) (pia) na iswalie |” Akauliza (tena)  Kama (athari ya) damu haikutoka?  (Mtume) akamjibu

 “ Kunakutosha kukosa damu, na wala athari ya damu haikudhuru :” Abuu Dawood.

iv.  Twahara ya mahala pa kuswalia.   

Ni lazima kwa mwenye kutaka kuswali ahakikishe  mahala anapotaka kupatumia kwa ajili ya utekelezaji wa ibada yake hiyo ya  swala ni twahara, hapana najisi yoyote ile.  

Sharti hili tunaliegemeza katika riwaya iliyopokelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwiye radhi amesema   “Alisimama mkazi mmoja wa majangwani akakojoa msikitini (msikiti wa Mtume) watu (mwaswahaba) wakamuinukia ili wamtie adabu”.  Mtume – rehema na Amani zimshukie akawaambia

 “ Muacheni (amaliza haja zake) na (kisha) mumwagie mkojo wake ndoo ya maji, kwani hakika si vinginevyo mmetumizwa kuwa wawepesishaji (wa mambo) na wala hamkutumwa kuwa wafanya uzito/ugumu – Bukhaariy.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *