Tujiandae na ramadhan

HUJACHELEWA, ANZA LEO KUJIANDAA KUUPOKEA MWEZI WA RAMADHANI NA KUIPATILIZA FURSA HIYO YA MWAKA HATA MWAKA

Sifa zote njema na takasifu ni zake Allah; Mola Mlezi wa viumbe vyote ambaye amesema katika kitabu chake kitukufu, alicho mteremshia Mtume wake Mtukufu: “BASI KUMBUSHA, KAMA KUKUMBUSHA KUNAFAA. ATAKUMBUKA MWENYE KUOGOPA. NA ATAJITENGA MBALI NAYO MPOTOVU”. Ewe Mola Muumba wetu! Mrehemu Bwana wetu Muhammad aliye Mbora wa wakumbushaji wote, Aali, Swahaba na wapenzi wake wote wenye kumfuata mpaka utakapo wakutanisha naye peponi. Aaamin!

Ama baadu,

Mpendwa ndugu yetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Mpendwa mfungaji mtarajiwa-Allah asitunyime fursa hiyo na aturehemu-tunakusihi ukubali na utambue ya kwamba jukwaa hili halipungui kuwa ni neema ambayo sote tunalazimika kumshukuru Allah kwa kutukirimu neema hii. Hivyo basi ni wajibu wa kila mmoja wetu kuitumia vema neema hii, kwa kuwa tayari kuyapokea na kuyatendea amali yale yote anayo kumbushwa kwa ajili ya maslahi na manufaa yake yeye mwenyewe katika dini, dunia na akhera yake. Naam, karibu katika jukwaa letu la juma hili, ambalo anuani yake inasomeka:

  • Allah amekwisha ikunjua mikono yake tayari kukupokea mja wake, mkimbilie naye atakupokea:

Ndugu mfungaji mtarajiwa-Allah akurehemu-zikiwa zimebakia siku chache mno kabla ya kuwasili kwa mgeni mtukufu tunaye mtazamia. Hebu sawirisha pamoja nami ndani ya akili yako, taswira ya mzazi aliye mkunjulia mwanawe mikono yake iliyojazwa mapenzi na huruma, tayari kumpokea na kumkumbatia mwanawe ambaye hawajakutana kwa muda mrefu. Unaiona furaha ya moyoni ya mzazi kwa mwanawe huyo inavyo onekana machoni mwake na kudhihirishwa na viungo vingine, kupitia namna atakavyo mkumbatia na kumbusu na hata kumbeba. Kupitia maneno matamu atakayo mwambia huku akimpapasa mwili wake mpapaso wa huba iliyo jaa shauku na huruma na huenda hata akabubujikwa na machozi ya furaha.

Naam, ikiwa umenielewa katika mfano huo, basi Allah Mtukufu huwa zaidi ya hivyo kwa mja wake pale anapo mpendelea mja wake, akamletea fursa ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ndani ya mwezi wa Ramadhani, Allah huikunjua mikono yake tayari kumpokea, kumuhurumia na kumsamehe mja wake aliye mjia akiwa na mzigo ulio mlemea wa madhambi. Ipatilize fursa hiyo na mkimbilie Mola Muumba wako akupokee mja wake huku ukiitia akilini mwako, moyoni mwako na mwilini mwako kauli yake Allah pale alipo sema kumwambia Mtume wake atuambie sisi waja wake: “Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Allah. Hakika Allah husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na nyenyekeeni kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa. Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui”. Az-zumar [39]:53-55

Na kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao, humkumbuka Allah na wakamuomba msamaha kwa dhambi zao – na ni nani anaye futa dhambi isipo kuwa Allah? – na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua. Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao”. Aali Imraan [03]:135-136

Ewe ndugu mfungaji mtarajiwa-Allah akurehemu-mkimbilie Mola wako mzima mzima; kwa kila kitu chako, mkimbilie kwa nguvu zako, mkimbilie kwa akili yako, mkimbilie kwa moyo wako, mkimbilie kwa roho yako, mkimbilie kwa imani yako, mkimbilie kwa mali yako na … na … Jitupe kwake, nyenyekea na jisalimishe kwake, ukifanya hivyo naye atakujia na kukupokea, hivyo ndivyo anavyo sema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika Hadithi Al-Qudsiy: “Atakaye jikurubisha kwangu kwa shubiri moja, nami nitamkurubia kwa dhiraa moja. Na atakaye jikurubisha kwangu kwa dhiraa moja, nami nitamkurubia kwa pima moja. Na atakaye nijia akitembea, Mimi nitamjia wangu wangu”.

Ewe ndugu mfungaji mtarajiwa-Allah akurehemu-usiipoteze fursa hii ambayo hujui kama utaipata tena mwakani, Mola wako amekuchagua na amekupa fursa ambayo Yeye haimnufaishi kwa chochote, amekunjua mikono yake tayari kukupokea, basi nawe mkimbilie kwa:

  1. Kumdhukuru faraghani, jifungie chumbani mwako, ukiwa peke yako baina yako na Mola wako, muabudu, zungumza naye na mlilie kwa madhambi uliyo yatenda na mbembeleze akusamehe. Ukifanya hivyo utakuwa umejijengea ngome madhubuti itakayo kukinga na madhambi na machafu na utaupata upamoja wake. Atakuwa nawe popote ulipo na kwa lolote ulitendalo. Mdhukuru Mola wako huku ukiijaza damuni mwako kauli yake tukufu: “Basi nidhukuruni (nikumbukeni kwa kuniabudu na kuniomba), nami nitakudhukuruni na nishukuruni wala msinikufuru”. Al-Baqarah [02]:152

Mdhukuru sana Mola wako hata uingie katika kundi la watu wenye akili kubwa: “Ambao humdhukuru Allah wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na huleta fikra ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wakasema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Sub-haanaka, Umetakasika! Basi (tunakuomba) utukinge na adhabu ya moto”. Aali Imraan [03]:191

Mdhukuru Mola wako kwa wingi asubuhi na jioni ili upate rehema yake: “Enyi mlio amini! Mdhukuruni Allah kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni (msabihini) asubuhi na jioni. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu waumini”. Al-Ahzaab [33]:41-43

  1. Kufanya toba ya kweli, mkimbilie Mola wako aliye kukunjulia mikono yake tayari kukupokea ndani ya Ramadhani, muendee ukiwa na toba ya kweli kwani ni Yeye ndiye aliye tuambia: “… na nyote tubuni kwa Allah, enyi waumini ili mpate kufanikiwa”. An-nuur [24]:31

Na ni Yeye ndiye aliye sema: “ Enyi mlio amini! Tubuni kwa Allah toba iliyo ya kweli. Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika pepo zipitazo mito kati yake…”. At-tahriim [66]:08

Ewe ndugu mfungaji mtarajiwa-Allah akurehemu-hatukusudii kwa kufanya toba ya kwamba wewe uombe tu msamaha kutokana na dhambi ulizo zitenda na wala hatukusudii wewe kumuendea Allah ndani ya Ramadhani ukiwa na moyo safi, la. Bali tunalo likusudia na kulilenga ni wewe kuyajua hayo madhambi kwa dhati yake hasa na kwa uwezeshi wake Mola tutakutajia baadhi ya hayo madhambi ambayo unapaswa kuyaletea toba kuanzia hivi sasa kabla hujafikiwa na mgeni mtukufu. Ukaendelea na toba hiyo ndani ya Ramadhani na hata baada ya Ramadhani na hilo likawa ni zoezi la maisha yako yote mpaka pale utakapo kutana na Mola wako nawe ukiwa miongoni mwa wale waja wema ambao wataambiwa wakati wa kutolewa roho: “Ewe nafsi iliyo tua! Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. Basi ingia miongoni mwa waja wangu. Na ingia katika pepo yangu”. Al-Fajri [89]:27-30

Na wale ambao: “… Allah yu radhi nao, na wao waradhi naye…”. Al-Bayyinah [98]:08

Naam, ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-pambana na nafsi yako na jitahidi kurejea kwa Mola wako, tubu kutokana na dhambi ya:

  • Unafiki: Hili ni gonjwa kubwa na hatari sana hasa hasa katika wakati wetu huu, jitahidi mno kujinasua kutokana na gonjwa baya hilo ambalo huenda limejenga kambi ndani yako. Ni jambo mumkini kwamba huweza kukusanyika ndani ya mtu Imani, unafiki na ukafiri pamoja, akawa ana fungu katika Imani, sehemu katika unafiki na kitu katika ukafiri, na huenda mwenyewe akawa anajua au hajui. Basi ukitokezea una jambo katika hayo, la mwanzo kabisa unalo paswa kulifanya ni kujikurubisha na kumuendea Allah na kumuomba toba ya madhambi hayo. Na katika jumla ya mambo ambayo yanahesabika kuwa ni unafiki, ni pamoja na:
  1. Kupuuzia swala (kunyong’onyea/kuswali kivivu):

Allah Mtukufu anasema: “Hakika wanafiki wanamkhadaa Allah, na hali ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kuswali huinuka kwa unyong’onyo, na wanajionyesha kwa watu tu (riyaa), wala hawamdhukuru Allah ila kidogo tu”. An-nisaa [04]:142

Naam, sote sisi tunapaswa kumuendea Allah kabla ya kuingia kwa mwezi wa Ramadhani kwa kufanya toba ya kujinasua kutokana na dhambi ya kupuuzia swala na hususan swala za jamaa misikitini. Huenda tunaswali, lakini tunaswali majumbani mwetu au kazini kwetu na ilhali hatuna sababu ya kisheria inayo tuzuia kuhudhuria jamaa misikitini.

Na hali kadhalika tulete toba ya dhambi ya kulala hata tukapitwa na swala ya Alfajiri, tujinasue na dhambi hiyo ili tusije kuangukia kwenye pote la wanafiki. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Hakika swala nzito mno kwa wanafiki, ni swala ya Ishaa na swala ya Alfajiri. Na lau watu wangelijua yanayo patikana humo (kwenye swala mbili hizo katika ujira na thawabu), basi wangeli ziendea hata kwa kutambaa”. Sunan Ibnu Maajah

Hali kadhalika kila mmoja wetu anatakiwa kuleta toba na kujinasua na dhambi ya kutomdhukuru Allah kwa wingi, wengi miongoni mwetu hatumdhukuru Allah ila ndani ya swala tu. Hivyo si sawa, muislamu anatakiwa kumdhukuru Allah katika hali zake zote na kila wakati; alale kwa kumdhukuru Allah, aamke na kumdhukuru Allah, atembee kwa kumdhukuru Allah, afanye kazi na ilhali anamdhukuru Allah, na … na … Ukijiona humdhukuru Allah ila ndani ya swala tu, basi tambua hiyo ni dhambi inayo hitaji toba, na hali hiyo haipungui kuwa ni mojawapo ya alama za unafiki. Haya haraka mkimbilie Mola wako na umuombe toba ili upate kuingia ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ukiwa umeshajinasua na hilo.

  1. Toba ya kusema uwongo: Kusema uwongo limekuwa ni jambo la mazoea linalo onekana kuwa halina neno kwa wengi miongoni mwetu, hapana hiyo ni dhambi inayo hitajia toba. Muislamu hapaswi ila kusema kweli hata katika mazingira magumu, jiepushe kabisa kusema uwongo huku ukitambua ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “… Hakika uwongo unapelekea kwenye uovu na hakika huo uovu unapelekea motoni”.

Na katika jumla ya yanayo hesabika kuwa ni uwongo, ni kutokutekeleza ahadi uliyo itoa wewe mwenyewe kwa mwenzako. Hapana, usivunje ahadi uliyo muahidi mtu pasina kulazimishwa, tekeleza ulicho ahidi. Na pia epuka kujionyesha mwema au mtu mzuri kwa kumuahidi mtu kitu ambacho wewe mwenyewe unajua fika huna uwezo wa kukitekeleza, usijikalifishe ukajitumbukiza kwenye dhambi ya uwongo, kwani: “Allah haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo…”. Al-Baqarah [02]:286 Ikiwa hivyo ndivyo kwa Allah, kwa nini basi wewe ujikalifishe kwa kuahidi usilo liweza, ukapata dhambi bure na ukajitia kwenye unafiki?!

Ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-kutoa ahadi nyingi usizoweza kuzitekeleza, hilo halipungui kuwa ni sehemu ya unafiki, tena ni katika jumla ya alama za kutupwa mkono mja na Mola wako, pulika.

  1. Kufanya khiana: Kuaminiwa, ukapewa amana kisha wewe ukafanya khiana; ukamdhulumu au ukamkana mwenye amana pale atakapo kuja kuchukua amana yake. Kufanya hivyo ni unafiki na hakupungui kuwa ni dhambi inayo taka toba, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Alama za mtu mnafiki ni tatu; anapo zungumza husema uwongo, anapo ahidi huvunja ahadi na anapo aminiwa hufanya khiana”.

Na katika upokezi wa Imamu Muslim-Allah amrehemu: “… hata kama ataswali na kufunga na akadai kwamba yeye ni muislamu”.

Allah Mtukufu anasema: “Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Allah na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua”. Al-Anfaal [08]:27

  1. Tubu kutokana na maafa ya ulimi: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Haitanyooka imani ya mja mpaka uwe mnyoofu moyo wake na wala hautakuwa mnyoofu moyo wake mpaka unyooke ulimi wake”.

Kwa kuizingatia kauli hii ya Bwana Mtume, tunapaswa kuanzia sasa na kuendelea kutubu kwa kupunguza kama si kuacha kabisa mazungumzo yasiyo ya lazima. Kwani muislamu sio mtu wa kusema sema hovyo bali hupima kwanza na kuangalia nini cha kusema, akiseme wapi na amwambie nani na nini athari ya maneno hayo, pulika. Muislamu hasemi semi kwa sababu anaisoma kauli yake Allah kuhusiana na waja wa Allah walio waumini: “Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi”. Al-Muuminuun [23]:03

Hebu acha kuongea sana, kuanzia sasa punguza kuongea na simu ila kwa dharura, epuka kukaa vijiweni kupiga soga, jiepushe na kufanya mzaha ulio pitiliza ambao pengine ukasababisha mzozo au ugomvi baina yenu. Fanya hivyo ili ukiingia ndani ya mwezi wa Ramadhani, uwe umeshakuwa na mazoea hayo na upate kuitumia vema fursa hiyo.

Hatukuambii usizungumze, usiongee na simu, la hasha. Bali tunalo kusudia kukuambia ni kwamba uwe kati na kati; fanya mzaha, cheka na ucheze na wenzako kwa kuchunga mipaka kama alivyo kuwa akifanya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na akisema: “Hakika mimi hufanya mzaha na wala sisemi ila haki (kweli)”.

Ndugu mwana jukwaa na mfungaji mtarajiwa-Allah akurehemu-kwa unyenyekevu mkubwa sote kwa pamoja tumuombe Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale walio andikiwa kuidiriki Ramadhani ya mwaka huu. Atuwezeshe kutenda amali njema ndani yake kwa namna itakayo mridhi na kuwa ndio sababu ya kutakabaliwa kwa amali zetu hizo, aturuzuku ukweli na ikhlasi katika kauli na matendo yetu. Na mwisho tuseme ya kwamba yale tuliyo patia katika yote tuliyo yasema, basi hilo linatokana na uwezeshi wake Allah peke yake na wala si kwa uhodari wala elimu yetu. Na pale tulipo teleza na kukosea, basi hayo ni katika mapungufu yetu sisi wanaadamu wenzenu, tuombeeni Mungu atusamehe na atuwezeshe kusema na kutenda yale yaliyo ndiyo, yaliyo sawa.

Panapo majaaliwa yake Allah tukutane juma lijalo, hapa hapa katika jukwaa letu la Ramadhani ya mwaka 1442H/2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *