SWALI LA WIKI (JUMA LA 86)

SWALI: Nimepata kusikia kwenye mojawapo na darsa za misikitini ya kwamba mtu akikosa maji anatakiwa kutayamamu. Naomba kujua namna ya huko kutayamamu.

JIBU: Uliyo yasikia ni sahihi kabisa, mtu akiwa mahala ambapo hapana maji au akiwa na maradhi ambayo huzidi pindi atakapo tumia maji au atachelewa kupona. Basi ameruhusiwa kutumia mchanga katika twahara badala ya udhu.

Ruhusa hiyo amepewa muislamu na Allah Mwenyewe katika kauli yake ambayo pia amefundisha namna ya huko kutayamamu, anasema Yeye aliye Mtukufu:“… NA MKIWA WAGONJWA, AU MMO SAFARINI, AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI, AU MMEWAGUSA WANAWAKE – NA MSIPATE MAJI, BASI UKUSUDIENI MCHANGA SAFI, MPAKE NYUSO ZENU NA MIKONO YENU…”. An-Nisaa [04]:43

Na imepokewa kutoka kwa Abdurahman Ibnu Abzaaa-Allah amuwiye radhi-amesema: Alikuja mtu mmoja kwa Umar bin Al-Khatwaab, akasema: Mimi nimepatwa na janaba na sijapata maji. Akasema Ammaar bin Yaasir kumwambia Umar bin Al-Khatwaab: Hivi wewe hukumbuki ya kwamba mimi na wewe tulikuwa safarini. Ama wewe hukuswali, lakini mimi nilijigaragaza mchangani na nikaswali. Nikamwambia Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Hakika si vinginevyo, ilikuwa inakutosha wewe kufanya hivi”. Mtume wa Allah akaipiga ardhi kwa vitanga vyake, kisha akapuliza ndani yake, halafu akapangusa kwavyo uso wake na mikono yake”. Bukhaariy [338], Muslim [368], Nasaai [311,318], Tirmidhiy [144], Ibnu Maajah [569] na Ahmad [04/265]-Allah awarehemu.

Allah ndiye Mjuzi mno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *