SWALI: Je, mwanamke analazimika kutoa huduma binafsi kwa mumewe mithili ya kumpikia, kumfulia na baki ya majukumu mengine ya nyumbani?
JIBU: Jumuhuri ya Wanazuoni wakiwemo wale wa Kishafi wamefuata madhehebu ya kwamba mke hakalifishwi kutoa huduma binafsi kwa mume wake au nyumba yake kufuatia kifungo cha ndoa.
Yaani halazimishwi na sharia kupika chakula, kufua nguo, kusafisha nyumba na mfano wa mambo hayo. Hivyo ni kwa sababu kifungo cha ndoa sio kifungo cha utumishi wa mke kumtumikia mume wake na wala hilo sio lengo la ndoa.
Bali ndoa ni kifungo kinacho maanisha ushirika katika kutimiza na kufikia starehe na kukidhi matamanio ya kijinsia baina ya wanandoa. Ushirika ambao unahitaji kila mmoja kujitoa kwa mwandani wake kimwili, kifikra, kiakili na kiroho.
Na kinacho ingia katika madhumuni ya ushirika huo ni unyonyeshaji na ulezi wa watoto tu, ambao ni zao na matunda ya ushirika huo. Kumpa utulivu mume na kunyonyesha mtoto wake, na kushirikiana na mume wake katika malezi ya mtoto wao huyo, hayo ndio mambo aliyo kalifishwa mwanamke na sharia.
Ama mambo na shughuli nyingine za nyumba, sharia haikumbebesha jukumu hilo kwa sababu/kufuatia kufungwa kwa kifungo cha ndoa.
Lakini angalia, ikiwa imezoeleka katika jamii yao ya kwamba mwanamke ndiye anaye beba jukumu la masuala yote ya nyumba; kupika, kufua, usafi na kadhalika. Basi hayo yatamlazimu kwa njia na mlango huo wa ada na wala sio kisharia na pia amepewa khiari ya kuutekeleza au kutoutekeleza wajibu huo na mume hakupewa mamlaka ya kumlazimisha.
Allah ndiye Mjuzi mno.