SWALI: Mke amefiwa na mume wake, je akae muda gani katika kumuhuzunikia marehemu mume wake?
JIBU: Kisheria, muda ambao ni wajibu mke akae kwa ajili ya kumuhuzunikia marehemu mume wake, ni miezi minne na siku kumi, kama alivyo sema Allah Mtukufu: “NA WALE MIONGONI MWENU WANAO KUFA NA WAKAACHA WAKE, HAWA WAKE WANGOJE PEKE YAO MIEZI MINE NA SIKU KUMI. NA WANAPO TIMIZA EDA YAO BASI HAPANA UBAYA KWAO KWA WANAO JIFANYIA KWA MUJIBU WA ADA…”. Al-Baqarah [02]:234
Na mambo ambayo mke analazimika kujifunga nayo ndani ya kipindi hiki, ni pamoja na:
- Kutokuolewa na kutojitia kwenye sababu zinazo pelekea kuolewa kama kujipamba, na
- Kutokutoka kwenye nyumba ya marehemu mume wake ila kwa haja kubwa.
Ama hili la kujilazimisha kuvaa nguo nyeusi eti kwa ajili ya kuonyesha msiba/kufiwa, kutokuzungumza na wanamume na kutojitazama kwenye kioo. Hayo ni mambo ambayo hayapo katika sharia yanayo vumishwa na wanawake majahili miongoni mwao, yote hayo hayana asili katika dini.
Allah ndiye Mjuzi mno.