SWALI: Leo ulimwenguni kote kumekuwa na miito ya kuwataka watu kuchangia damu, na watu wanaitika na kuchangia hiyo damu na wengine kufikia hata kujitolea viungo vyao vya mwili. Sheria inasemaje kuhusiana na suala hilo?
JIBU: Kwanza muulizaji na wasomaji wote, tunapaswa kufahamu ya kwamba lililo asili katika vitu vyote ni UHALALI, kisha ndipo hutolewa vilivyo harimishwa kutoka kwenye uenevu/ujumla wa vitu hivyo kwa njia ya kuvuliwa. Yaani kwa mujibu wa nukuu za Qur-ani(nassi) na dalili(Hadithi, Qiyaasi au Ijmaai), zinazo thibitisha hukumu ya uharamu wa jambo/kitu hicho.
Na kitendo cha mtu kujitolea damu akawekewa mtu mwingine kwa maridhiano ya pande zote mbili; pasina kulazimishwa mchangiaji, haikuja na wala haikupokewa nukuu au dalili inayo liharimisha hilo.
Bali kitendo hicho kinaingia chini ya uvungu wa matendo ya kheri na huduma za kibinaadamu ambazo Allah ameziwekea sharia kwa neno lake: “…na saidianeni katika wema na uchaMngu na wala msisaidiane katika dhambi na uadui…”. Al-Maaidah [05]:02
Na mfano wa uchangiaji damu, ni sawa sawa na mtu kujitolea figo yake ili ipandikizwe kwa mtu mwingine anaye sumbuliwa na matatizo ya figo. Kwani lililo asili katika jambo hilo ni kujuzu/kufaa/kuruhusiwa, lakini pia ni kitendo cha utu mkubwa.
Lakini hilo lifanyike baada tu ya kuthibitishwa na daktari mahiri wa fani hiyo ya kwamba kujitolea kwake figo au kiungo chake kingine, hakutaiathiri afya yake au kuyahatarisha maisha yake. Na kwamba baada ya kutolewa kwa kiungo hicho ataendelea kuishi kawaida.
Allah ndiye Mjuzi mno.