SWALI: Allah ameturuzuku mtoto wa kike, mke wangu anataka kumuita Jenifa, lakini mimi nimemkatalia na nikampa jina Fatma. Je, Uislamu unasemaje katika suala zima la majina?
JIBU: Unalo litaka Uislamu ni wazazi kuwachagulia watoto wao majina mazuri, yanayo kubalika na wala haukushurutisha majina maalumu ila tu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amependekeza baadhi ya majina. Lakini wazazi wanawapa watoto wao majina ya watu wa nyumba ya Mtume (Aali Beit) kwa ajili ya kutabaruku nao na kuonyesha mahaba yao kwa kizazi cha Bwana Mtume. Na hali kadhalika wanawapa majina ya Mitume wa Allah, maswahaba, mawalii, wanazuoni na masheikh zao kwa lengo hilo hilo la kutabaruku nao.
Lakini atakaye ukhalifu utaratibu huo, hapati dhambi muda wa kuwa jina atakalompa mwanawe linakubalika, halina maana mbaya na wala halishabihiani na majina ya makafiri.
Allah ndiye Mjuzi mno.