SWALI LA WIKI (JUMA LA 61)

SWALI: Mwanamke yumo katika hedhi, je ni halali kwake kumdhukuru Allah kwa kuleta mfano Tahalili (Laa ilaaha illal-laah), Tahmiidi (Al-hamdulillaah), Tasbihi (Sub-haanallaah) na Takbiiri (Allaahu Akbaru)?

JIBU: Hedhi na nifasi ni katika jumla ya nyudhuru za kisheria ambazo zikimtokea mwanamke haiswihi swaumu wala swala yake hata kama atafunga au kuswali. Imepokewa kutoka kwa Muaadhah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Nilimuuliza Aisha-Allah amuwiye radhi: Ana jambo gani mwenye hedhi anakidhi (analipa) swaumu na wala hakidhi swala? Akajibu: Tulikuwa tukipatwa na hali hiyo tulipo kuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-basi tukiamrishwa kukidhi swaumu na wala hatukuamrishwa kukidhi swala”.

Angalia, mwanamke muislamu atakapo tokewa na hedhi au nifasi naye akiwa katika swaumu ya Ramadhani au nyingineyo, ni wajibu afungue (ale) tangu wakati ule wa kuanza kutoka kwa damu. Na wala hapati thawabu na si uchaMngu, iwapo atakaidi na kuendelea kufunga. Ama kwa upande wa swala, haitakuwa wajibu kwake katika kipindi chote cha hedhi au nifasi yake na wala hatalipa kwa ushahidi wa hadithi tuliyo tangulia kuinukuu. Sharia imemfanyia hivyo ili kumfanyia takhfifu kutokana na kujirudia kwa hedhi kila mwezi na kama hivyo nifasi nayo hujirudia kila anapo jifungua. Na wala hakuna ubaya na wala si dhambi yeye kumdhukuru Allah akiwa katika hali hiyo, bali ni halali kwake kufanya dhikri wakati wowote; usiku au mchana. Lakini ni HARAMU kugusa/kushika msahafu.

Allah ndiye Mjuzi mno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *