SWALI LA WIKI

SWALI: Imekua ni ada na mazoea ya miaka mingi katika baadhi ya jamii, anapo fariki mmoja wao, ndugu na jamaa hukusanyika kwenye nyumba ya msiba, kwa ajili ya kuwafariji na kuwapa pole (Ta’azia) wafiwa. Naomba kujua hukumu ya sheria katika jambo hilo na Allah atakupeni jazaa iliyo njema.

JIBU: Kuwafanyia Ta’azia wafiwa kwa kwenda kukaa nao, kuwafariji na kuwapa pole ya kuondokewa na mpendwa wao, kwa lengo la kuwapunguzia makiwa, jambo hilo ni Sunna iliyo kokotezwa (Sunna Muakadda). Tunalichukulia hilo kuwa ni katika maslahi mema yenye kuendana na zama/wakati na mazingira ya sasa.

Ama watu kushughulika na kusoma Qur-ani kwa nia ya kumuombea marehemu na huku watu wakiingia na kutoka na wengine kuzungumza na huku watu wakipewa kahawa, huko kutakuwa ni kukidharau na kukivunjia heshima kitabu chake Allah. Lakini hilo halikinzani na ile hoja iliyo tiwa nguvu na wengi miongoni mwa Wanazuoni wa Fiq-hi, ya kwamba thawabu za kisomo cha Qur-ani humfikia maiti kwa fadhila na ukarimu wake Allah, pale zitakapo tolewa hidaya kwake kupitia dua inayo somwa baada ya kuhitimishwa Qur-ani.

Ama kile chakula kinacho andaliwa na wafiwa kwa ajili ya wanandugu na watu wasio wahitaji, kikaliwa na kusazwa hata kutupwa jaani, hilo ni bidaa ambayo tunapaswa kujiepusha nayo na hasa hasa ikiwa chakula hicho kimetokana na mali iliyo achwa na marehemu.

Allah ndiye Mjuzi mno.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *