Kuibuka (kuanzishwa) na kukua kwa mji wa Makka.
Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-fahamu na uelewe ya kwamba, Historia ya mji wa Makka; kuibuka, kujengwa na kukua kwake haiandikiki na wala haielezeki bila ya kutajwa Mtume wa Allah; baba yetu Ibrahim na mwanawe Ismail-Amani iwashukie. Haya sasa, tufuatane pamoja tuiangalie tarekhe (historia) fupi ya maisha ya Nabii Ibrahim-Amani imshukie-ili tupate kujua namna anavyo fungamana na tarekhe ya mji mtukufu wa Makka.
Kwa Jina la Allah tunaanza hali ya kuutegemea msaada wake kwa kutambua ya kwamba mwanaadamu na kiumbe yeyote awaye hana aliwezalo ila tu ni kwa msaada na uwezeshi wake Mola:
Nabii Ibrahim-Amani imshukie-alihamia Shamu akitokea Iraq, kisha tena akaondoka Shamu na kuhamia Misri. Na katika misafara na hijra zake hizo alikuwa akibeba, kuambatana na kuusambaza ujumbe wa Tauhid (kuwalingania na kuwahubiria watu kumpwekesha katika ibada Allah pasina kumshirikisha na chochote katika viumbe wake). Hilo linatajwa na kushuhudiwa na kauli yake Mola: “Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Allah, mwongofu wala hakuwa miongoni mwa washirikina”. An-Nahli [16]:120
Na katika safari zake hizo alikuwa akiambatana na mkewe aitwaye Sarah; mama yetu huyu alikuwa mzuri wa sura, umbo na tabia. Na ilikuwa ni katika ada, mazoea na kawaida ya wafalme wa Misri wa zama hizo, kujitwalia kila mwanamke mzuri anaye tokezea kwenye ufalme wao. Na Allah akataka kuikomesha ada mbaya hiyo kupitia kwa Mama yetu Sarah, yakajiri yaliyo jiri, mfalme akauona uwezo na nguvu ya Allah iliyo jitokeza kwa Mama Sarah. Moyo wake ukaingiwa na khofu, akaiacha dhamira yake mbaya kwa Mama yetu huyo na badala yake akamzawadia kijakazi wa kumtumikia, ambaye ndiye Bi. Haajira; mama yake Nabii Ismail-Amani imshukie.
Na kwa kuwa Bi. Sarah alikuwa ni tasa na Nabii Ibrahim-Amani imshukie-alikuwa ameingia kwenye umri wa uzee, kichwa chote kimekuwa cheupe kwa mvi. Bi. Sarah akaona ni vema ampe hiba mume wake, akamtoa kijakazi wake awe suria kwake, huenda Allah akamruzuku kutokana naye kizazi chema. Na mapenzi na matashi yake Allah yakawafiki Bi. Haajira amzalie Nabii Ibrahim mtoto wake wa kwanza, akamuita Ismail-Amani iwashukie.
Baada ya Bi. Haajira kujifungua mwanawe Ismail, maumbile yakamshinda Mama yetu Sarah akapatwa na wivu ulio pindukia kiasi cha kufikia kuapa kumkatakata vipande Bi. Haajira. Kwa kuchelea kufikwa na yaliyo apwa juu yake, Bi. Haajira akajitengenezea guo kama mtandio mkubwa wenye mkia mpana unao buruza, akajifunga kiunoni, akambeba mwanawe na kukimbia ili kuyasalimisha maisha yake na yale ya mtoto wake. Wakati akichapua mwendo alikuwa akiliburuza lile guo ili kufuta athari ya nyayo zake kwa ajili ya kumpoteza Mama Sarah asipate kujua alipo elekea yeye na mumewe. Wakaenda hata Nabii Ibrahim akamfikisha na mwanawe Ismail naye akinyonya, akawaweka mahala ilipo jengwa Al-Ka’aba. Ikumbukwe wakati huo Makka hapakuwa na watu wanao ishi hapo, bali ilikuwa ni jangwa tupu na kame lisilo na maji. Akamuachia kijaruba kilicho kuwa na tende kiasi na guduria la maji, kisha akamuaga tayari kuanza safari ya kurejea Misri kwa mkewe Sarah.
Bi. Haajira akamfuata kama mtu anaye msindikiza mgeni, akamwambia: “Ewe Ibrahim! Unakwenda wapi na kutuacha kwenye jangwa hili lisilo na chochote, tena bila hata mwenza wa kutuliwaza?”. Akayakariri maneno yake hayo mara kadhaa na Nabii Ibrahim hageuki nyuma na wala hamjibishi, hatimaye Bi. Haajira akamuuliza: “Je, ni Allah ndiye aliyekuamrisha kufanya hivi?”. Akamjibu: “Ndio”. Bi. Haajira akamwambia: “Kama ni hivyo, basi (Allah) hatatutupa mkono (hatatuacha tuangamie)”. Kwisha kusema hivyo akarejea pale alipo wekwa na mume wake. Nabii Ibrahim-Amani imshukie-akaondoka hata alipo fika mahala asipo weza kuonekana na mkewe, akaelekea upande ule wa nyumba ya Allah (Al-Ka’aba), akaomba akisema: “Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu. Ewe Mola wetu Mlezi! Ili washike swala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na waruzuku matunda, ili wapate kukushukuru”. Ibrahim [14]:37
Hakikupita ila kitambo kidogo tu tangu kuondoka kwa Nabii Irahim, Bi. Haajira akaishiwa maji na kikampata kiu kikali yeye na mwanawe Ismail, moyo wake ukaungua kumuona mwanawe akitweta kutokana na ukali wa kiu kilicho mshika. Akaanza kuhangaika kuyasaka maji, akaenda hata akasimama kwenye jabali lililo kuwa karibu, nalo ndilo jabali “Swafaa”, akalielekea jangwa kujaribu kuangalia labda atamuona yeyote apitaye, huenda akawa na akiba ya maji, akawasaidia. Alipo kata tamaa ya kumuona mtu, akashuka kutoka pale jabalini alipo kuwa amesimama, hata alipo fika chini akapanya kidogo nguo yake ili apate kuchapua mwendo. Akaenda mpaka akafika kwenye jabali “Marwah”, akasimama juu yake ili kuona kama atabahatisha kumuona mtu akipita eneo hilo, lakini wapi hakuweza kumuona yeyote. Akaenda baina ya majabali hayo mawili mara saba – na hiyo ndio Sa’ayi inayo fanywa na mahujaji kama alivyo sema Mtume wa Allah (Rehema na Amani zimshukie).
Na mwishoni mwa ile mara ya saba, akatokewa na malaika Jibrilu-Amani imshukie-akaanza kutafuta mahala pa kisima cha Zamzam mpaka yakachimbuka maji. Bi. Haajira akawa anayawekea kitu kama ukingo ili kuyazuia yasisambae, kisha akayachota na kuyatia kwenye guduria lake. Kule kuyachota kukayafanya yazidi kufurika na katika hili Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Allah amrehemu mama yake Ismail, lau angeliiacha Zamzam”. Au alisema: “Lau asingechota maji kwenye Zamzam, basi leo Zamzam ingelikuwa ni mbubujiko mkubwa”. [Rejea FAT-HUL BAARIY 13/140
Bi. Haajira akanywa maji yale hata akakata kiu na kwa baraka ya maji hayo, akapata maziwa ya kutosha kumnyonyesha mwanawe. Malaika Jibrilu akamwambia: “Usichelee kutupwa na kuachwa pweke, hakika (mahala) hapa ni Nyumba ya Allah itakayo jengwa na mtoto huyu na baba yake na hakika Allah hawatupi mkono watu wake”. Na wakati ambapo Bi. Haajira akiwa jangwani hapo na mwanawe peke yao, wakiwa na maji ya Zamzam tu bila ya chakula, wakapita hapo watu wa kabila la Jurhum kutokea Yemen, kabila litokanalo na ukoo wa Qahtwaani. Walipo kuta maji hapo, na kutokana na shida kubwa ya maji jangwani, wakamuomba wapige kambi hapo, akawakubalia lakini kwa sharti la kutokuwa na haki ya umiliki wa maji hayo, wakakubali. Wakaenda kuwachukua wenzao, wake na watoto wao walio kuwa wamewaacha mahala wakati wao wakihangaika kutafuta maji, wakaja nao hapo. Wakafanya maskani hapo, na mtoto Ismail akakua miongoni mwao, akajifunza lugha ya Kiarabu kutoka kwao. Wakapendezwa naye hata alipo kuwa kijana barobaro, wakamuozesha mmoja wa banati zao.
Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-kwa juma hili tutamatie hapa huku tukizidi kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo ili tupate kuendelea na kisa hiki kitakacho tufundisha na kutuwekea wazi tarekhe ya kuibuka na kukua kwa mji mtukufu wa Makka.