Haya ni mambo ambayo mwenye kuswali anatakiwa kuyatenda kabla hajaingia ndani ya swala, haya hayazidi mambo matatu ambayo ni:
(i) Adhana
(ii) Iqaamah.
Inshaalah, tutazielezea adhana na Iqaamah kwa ufafanuzi wa kutosha katika somo la pili.
(iii) Kuweka sitara mbele.
Ni suna kwa mwenye kuswali kuweka kitu mbele yake kitakachokuwa ni sitara baina yake na wale wapitao mbele yake.
Sitara hii inaweza kuwa ni ukuta au nguzo ya msikiti, akaswali karibu na ukuta au nyuma ya nguzo.
Au anaweza kuweka fimbo mble yake au kitu kingine mithili ya hivyo. Kama hakupata sitara kabisa, basi anaweza kuchora/kupiga mstari.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar- Allah awaridhie kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa anapotoka siku ya Eid (kwa ajili ya swala) huamrisha (uletwe) mkuki wake na huwekwe mbele yake, naye huswali kwa kuuelekea na il-hali watu (wakiswali) nyuma yake. Na hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya awapo safarini.
Bukhaariy na Muslim.
Na ni bora sitara ikawa karibu na mahala pake pa kusujudia. Hili linatokana na riwaya iliyopokelewa kutoka kwa sahli Ibn Sa’ad – Allah amuwiye radhi – amesema:
Ulikuwa (Umbali) wa baina ya muswala (mahala pa kusujudia) wa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie na ukuta wa msikiti ni (kama) mapito ya mbuzi (nafasi awezayo kupita mbuzi). Bukhaariy na Muslim.