SOMO LA TATU – HALI YA BARA ARABU WAKATI WA KUPEWA UTUME MUHAMMAD – Rehema na Amani zimshukie.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Naam, kwa mara nyingine tena, Mola wetu Mtukufu anatukutanisha katika darasa letu la Sira, ili litusaidie kumjua Mtume wetu na dini yetu kwa ujumla. Juma lililo pita tulimaliza kujifunza kuhusiana na utukufu wa mji wa Makka. Juma hili kupitia uwezeshi wake Allah, tutaanza kuiangalia hali ya Bara Arabu ilivyo kuwa kipindi ambacho analetwa Mtume wa Allah kuja kushika hatamu za uwongozi wa ulimwengu. Haya karibu darasani:

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-ni bora na ni kheri kwako ukafahamu ya kwamba jamii ya wanaadamu iliishi katika kiza cha jahiliya mnamo kipindi cha karne mbili; karne ya sita na saba Miladia. Kwani kipindi hicho kilitawaliwa mno na itikadi ya kuabudu sanamu, ushirikina, ukabila, utabaka, ubaguzi na machafu ya kijamii na kisiasa. Na ni ndani ya kipindi hicho ndimo ambamo iliharibiwa na kukengeushwa sehemu kubwa ya fikra tengenea; zilizo salimika na mapungufu. Fikra zote; zile zilizo letwa na kuachwa na Mitume walio tangulia au zile zilizo achwa na wenye hekima, waonao mbali ambao umbile lao limesimama juu ya haki. Na kweli hakika hii imeelezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia kauli yake: “Hakika Allah aliwaangalia wakaazi wa ardhini, akawachukia (kutokana na matendo yao maovu) wote; Waarabu miongoni mwao na wasio Waarabu ila masalia ya Ahli (watu wa) Kitaab (walio shikamana na dini yao ya haki pasina kuitia mikono)”. Muslim [04/2197]-Allah amrehemu.

Katika masomo yanayo fuatia, tutaeleza kwa mukhtasari hali ya Bara Arabu katika kipindi hicho ili tupate kuuona umuhimu wa risala (ujumbe wa kitume) wa Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Na misingi na vipimo vya utu vilivyomo kwenye risala hiyo ambavyo vilikuwa, vinaendelea na vitaendelea kuwa injini na sababu ya msingi katika ujenzi wa utu wa mwanaadamu.

Kwa msaada na uwezeshi wake Mola, tuanze kuangalia:

  1. Hali ya Kisiasa.
  2. Dola ya Yemen:

Hakika miongoni mwa jamii kongwe za watu zilizo julikana kuishi katika nchi ya Yemen katika Waarabu, ni Waarabu wanao julikana katika Istilahi za Kihistoria kwa jina la “Aariba”. Hao wanatokana na kaumu ya Sabai ambao wametajwa ndani ya Qur-ani Tukufu na sura nzima (34) ikaitwa kwa jina lao. Mola anasema: “Hakika ilikuwapo ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao, bustani mbili kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Allah, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu”. Sabai [34]:15

Kuchanua kwa ustaarabu wao na kuimarika kwa utawala na nguvu zao kulidumu kwa karne kumi na moja. Mnamo mwaka wa mia tatu Miladia, ufalme/utawala wao ulishindwa na kabila la Himyari. Baada ya hapo Dola ya Yemen ikaanza kuporomoka na makabila ya Qahtwaani yakaanza kutapanyika na kuhamia kwenye nchi tofauti tofauti.

Yakafululiza kwao machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kisicho pungua miaka mia mbili na sabini, hicho ni kipindi cha kabla ya kuingia kwa Uislamu kwenye taifa la Yemen. Machafuko na vita hivyo vikapelekea kudhoofisha nguvu zao na kutoa mwanya kwa mataifa ya kigeni kuingia na kuikalia Yemen kimabavu. Warumi wakaingia Aden na kwa msaada wao Wahabeshi wakaikalia Yemen kwa mara ya kwanza mwaka 340 Miladia, wakaitumia fursa ya ushindani na upinzani ulio kuwepo baina ya makabila ya Hamdani na Himyari. Ukaliaji huo wa kimabavu wa Wahabeshi uliendelea mpaka mwaka 378 Miladia, kisha Yemen ikajipatia uhuru wake. Lakini Allah akawapelekea mafuriko makubwa mnamo mwaka 450/451 Miladia, yakalivunja bwawa la Ma’arab ambalo Allah alilifanya kuwa chanzo cha neema na hali njema kwao. [Rejea AT-TAARIIKH cha Al-Ya’aquubiy 01/205] 

Yote hayo yaliwakumba kwa sababu ya ufisadi, kufuru na kuikengeuka kwao dini ya haki na hiyo ndio kawaida na ada yake Mola katika hayo. Mafuriko hayo ndio yanayo tajwa na kauli yake Allah: “Lakini wakaacha, tukawapelekea mafuriko makubwa, na tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda makali machungu na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi kwani tunamuadhibu isipokuwa anaye kufuru?”. Sabai [34]:16-17 

Na mnamo mwaka 523 Miladia, mfalme wao aitwaye Dhu Nawaas alianzisha mashambulizi dhidi ya Waumini na Wafuasi wa Nabii Isa (Wakristo wa Najiraan) ili kuwatoa kwenye dini yao, walipo kataa, akawachimbia mahandaki, ukawashwa humo moto na wakatumbukizwa humo. Hao ndio ambao khabari yao imetajwa na Allah katika Qur-ani Tukufu: “Wameangamizwa watu wa mahandaki. Yenye moto wenye kuni nyingi. Walipo kuwa wamekaa hapo. Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia waumini. Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Allah, Mwenye nguvu, Msifiwa”. Al-Buruuj [85]:04-08

Mashambulizi hayo yakawa ndio sababu ya Warumi kuwachochea na kuwashawishi Wahabeshi kuikalia tena Yemen kwa mara ya pili mnamo mwaka 525 Miladia chini ya uongozi wa Aryaatw. Huyu akawa ndiye mtawala wa Yemen mpaka pale alipo uawa na Abraha; mmojawapo wa makamanda wa jeshi lake. Abraha akatwaa hatamu za utawala baada ya kupata baraka za mfalme wa Uhabeshi. Baada ya kutwaa madaraka, Abraha akafanya jaribio la kuivunja Al-Ka’aba iliyoko Makka, lakini Allah akalizima jaribio lake hilo kwa nguvu zake zisizo shindwa. Jaribio hilo ndilo linalo simuliwa na Qur-ani Tukufu, tusome pamoja: “Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo? Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika? Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi. Wakiwatupia mawe ya udongo wa motoni. Akawafanya kama majani yaliyo liwa!”. Al-Fiil [105]:01-05 

Wayemeni wakaomba msaada kwa Wafursi (Waajemi), wakawasaidia kuwafurusha Wahabeshi nchini mwao mnamo mwaka 575 Miladia. Wakafanikiwa kuwaondosha Wahabeshi chini ya ukamanda wa Ma’ad Yakrib bin Seif bin Dhi Yazini wa kabila la Himyari, wakamtawaza kuwa mfalme wao. Mfalme huyu akalibakisha kundi la Wahabeshi kwa ajili ya kumtumikia, wakapanga njama wakamuua, kifo chake kikawa sababu ya kukatika kwa silsila ya ufalme katika ukoo wake.

Kufuatia hali hiyo, Kisraa; mfalme wa Fursi (Uajemi) akamtawaza Mfursi kuwa gavana wa mji wa Sanaa na Yemen akaifanya kuwa jimbo lililo chini ya Fursi linalo pokea amri na maelekezo mengine ya kiutawala kutoka kwake. Na gavana wa mwisho mfursi kuitawala Yemen alikuwa ni Baadhaan, huyu alisilimu na kwa kusilimu kwake ukakoma utawala wa Fursi katika nchi ya Yemen. [Rejea AT-TAARIIKH cha Al-Ya’aquubiy 01/200]

Kusilimu kwa Baadhan kulikuwa ni katika mwezi wa Jumaadal-Uula (Mfunguo Nane), mwaka wa saba wa Hijra, sawa na mwaka 627 Miladia. [Rejea AT-TWABAQAATUL-KUBRAA cha Ibn Sa’ad 01/260]

Naam, ndugu mwana darasa-Allah akurehemu-tunatumai kuwa unafuatana pamoja nasi na kwamba tayari umeshaanza kupata pepeso juu ya hali ya Bara Arabu ilivyo kuwa kabla ya kuletwa kwa Mtume wa mwisho; Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Tumuombe Allah atukutanishe juma lijalo, tupate kuelimishana namna ilivyo kuwa hali ya Bara Arabu. Maa Salaam!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *