SOMO LA TANO – MUHAMMAD; MTUME WA MWISHO-Rehema na Amani zimshukie-Na uhusiano/mafungamano ya ujumbe (Da’awa) wake na jumbe za mbinguni zilizo tangulia.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-kwa auni na uwezeshi wake Mola, tumekutana tena juma hili katika darsa zetu za Sira yake Bwana Mtume, leo tutaanza kujifunza uhusiano/mafungamano ya Risala ya Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na Risala za kabla yake.

Tunasema hali ya kumtaraji Allah atuongoze kusomeshana yale yaliyo ndiyo, yale yatakayo tunufaisha sote na kutusogeza karibu zaidi na Bwana Mtume ili tuweze kumuiga na kumfuata:

Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-ndiye Mtume wa mwisho, na tunaposema hivyo tunamaanisha ya kwamba hakuna tena mtume mwingine atakaye letwa baada yake. Kwani huko nyuma ilikuwa ni utaratibu na mpango wa kiMungu, mtume kufuatiwa na mtume mwingine.

Utaratibu na mpango huo wa kiMungu ukakoma na kutamatia kwa kuja Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-ndipo pakasemwa kwamba yeye ni mtume wa mwisho, kwa maana ya kuletwa kwa watu duniani. Na ni kwa ajili hiyo basi ndio akawa Mtume wa mataifa yote na watu wote ulimwenguni kote.

Na kuwa kwake Mtume wa mwisho, hilo ni jambo ambalo wamekongamana kwalo Wanazuoni wote wa Kiislamu, tena ni kadhia ambayo kujulikanwa kwake ni dharura katika dini.

Bwana Mtume amesema: “Mfano wangu mimi na Mitume wa kabla yangu (walio nitangulia), ni kama mfano wa mtu aliye jenga jengo vizuri na akalipamba ila sehemu ya tofali moja tu katika mojawapo ya pembe zake. Watu wakawa wakiizunguka (nyumba hiyo) na kupendezwa nayo na wakisema: Laiti lingeliwekwa tofali hilo (mahala hapo palipo wazi)? Basi mimi ndiye hilo tofali na mimi ndiye mwisho wa Mitume”. Bukhaariy na Muslim-Allah awarehemu.

Ama risala/ujumbe wake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na mafungamano/mahusiano yake na risala za Mitume walio mtangulia, yamesimama na kujengwa juu ya msingi wa kuthibitisha na kutimiza/kukamilisha, kama linavyo julishwa na kufahamishwa hilo na hadithi tuliyo inukuu hapo juu.

Ubainifu na ufafanuzi wa maelezo hayo, ni kwamba risala ya kila mtume inajengwa juu ya misingi miwili mikuu:

  1. Msingi wa kwanza ni Akida (Itikadi), na
  2. Msingi wa pili ni Sharia na Akhlaaki (Tabia na Maadili).

Ama tukianza na kuielezea Akida, madhumuni/malengo yake hayakutofautiana tangu kwa Mtume wa kwanza; Baba yetu Adam-Amani imshukie-mpaka kwa Mtume wa mwisho; Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Hakika si jenginelo, hiyo Akida ni:

  • Imani inayo elezea umoja na upweke wa Allah na kutakata/kuepukana kwake na kila sifa/jambo lisilo chukuzana na utukufu wake,
  • Imani ya uwepo wa siku ya mwisho (ambamo watu wote watakufa, kisha wafufuliwe na kusimamishwa mbele ya Allah kwa ajili ya kuhisabiwa na),
  • Imani ya hesabu (kuhisabiwa waja kwa matendo yao na kisha kulipwa jazaa sawiya), na
  • Imani ya uwepo wa Pepo (jazaa ya watu wema) na Moto (jazaa ya watu waovu).

Akawa kila Mtume aliye letwa anawalingania na kuwahubiria kaumu (watu) yake kuyaamini mambo hayo. Na alikuwa kila mmoja miongoni mwao anakuja kuisadikisha risala ya mtangulizi wake na kutoa bishara ya Mtume mfuatizi wake (atakaye kuja baada yake).

Naam, kama hivyo basi kulifuatana na kufululiza kutumwa na kuletwa kwao kwa watu na mataifa tofauti tofauti, ili wote waithibitishe “kwelihakika” moja waliyo amrishwa kuifikisha kwa waja wa Allah. Na kuwafanya watu wainyenyekee na kuikubali, na kwelihakika hiyo si nyengineyo ila ni kumuambudu Allah Mtukufu peke yake, pasina kumshirikisha na yeyote/chochote katika viumbe wake.

Na hilo ndilo linalo bainishwa na Allah kupitia kauli yake iliyomo ndani ya kitabu chake kitukufu: “Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na tuliyo wausia Ibraahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini na wala msifarikiane kwayo…”. As-shuuraa [42]:13

Bali ni jambo lisilo sawirika kutofautiana risala/jumbe za Mitume walio wakweli katika suala la Akida, kwa sababu kadhia ya Akida ni katika aina ya kupokea na kufikisha khabari. Na upokeaji na ufikishaji wa khabari ya jambo fulani, hakumkiniki kutofautiana baina ya mfikisha khabari mmoja na mwenzake, kama tutakadiria ukweli katika khabari ya kila mmoja wa wawili hao.

Kwa mantiki hiyo basi, ni jambo lisilo ingia akilini kutumwa/kuletwa mmoja wa mitume awafikishie watu khabari ya kwamba Allah ni mmoja katika watatu (Ametakata na hayo wayasemayo).

Kisha akatumwa/akaletwa mtume mwingine baada yake awafikishie ya kwamba Allah ni Mmoja; hana mshirika. Kisha baada ya kufikisha khabari hiyo, kila mmoja kati ya mitume wawili hao walio fikisha khabari inayo tofautiana awe ni mkweli katika khabari hiyo aliyo ifikisha kutoka kwa Allah ambaye ndiye chanzo cha khabari. Jambo hilo ni muhali kimantiki, chanzo kimoja kutoa khabari tofauti kwa mlengwa yule yule, hilo halimkiniki abadan.

Naam, hilo ni kwa upande wa Akida. Ama kwa upande wa Sharia, ambao ni ule uratibu/uwekaji wa hukumu ambazo kunatarajiwa kwazo kutungamana, kupangika na kusimama sawa kwa maisha ya jamii na yale ya fardi (mtu mmoja mmoja).

Lililo la lazima ni kuwa hiyo sheria ifuate na iendane na maendeleo na mahitaji ya zama husika na utofauti wa watu na mataifa yao. Utofauti wa zama, watu na maendeleo ni mambo yenye athari katika kutanuka na kutofautiana kwa sheria baina ya mataifa.

Inakuwa hivyo kwa sababu asili na chimbuko la uratibu na uwekwaji wa sheria umejengwa juu ya msingi wa yanayo pelekea maslahi ya waja katika dunia na akhera yao kupitia sheria hiyo.

Naam, hivyo ni kwamba uletwaji wa mitume wote walio tangulia ulikuwa ni makhsusi kwa umma/kaumu/taifa maalumu na wala haukuwa enevu kwa jamii yote ya wanaadamu. Kwa ajili hiyo basi, zikawa hukumu za kisharia zimefungika katika wigo finyu kulingana na mahitaji na hali ya umma/kaumu/taifa husika.

Kwa mfano, alitumwa na kuletwa Mtume Musa-Amani imshukie-kwa wana wa Israili na mazingira munasaba kwa hali ya Wana wa Israili wa zama hizo, yalikuwa yanahitajia na kupelekea sharia yao kuwa ngumu/nzito iliyo jengwa juu ya msingi wa maamuzi (mtu hana khiyari ila kufuata tu) na sio rukhsa (mtu ana khiyari ya kutenda au kutokutenda).

Na zilipo pita zama nyingi na akatumwa kwao Mtume Isa-Amani imshukie-yeye akawaletea sheria rahisi kutekelezeka na nyepesi zaidi kuliko ile aliyo tumwa kuwaletea Nabii Musa-Amani imshukie-hapo kabla.

Liangalie hilo kwenye kauli yake Allah kwa ulimi wa Nabii Isa naye akizungumza na Wana wa Israili: “Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikubainishieni baadhi ya yale mliyo harimishiwa…”. Aali Imraan [03]:50

Katika maneno yake hayo, Nabii Isa-Amani imshukie-anawabainishia Wana wa Israili ya kwamba yeye katika mambo yanayo fungamana na Akida, ni mwenye kuyasadikisha na wala si kuyatengua yale yaliyomo ndani ya Taurati miongoni mwa hukumu.

Na tena ni mwenye kuyathibitisha hayo na kuhuisha ulinganiaji (uhubiriaji) wa hayo. Ama kwa upande wa uratibu wa sheria na hukumu za halali na haramu, amepewa jukumu la kufanya mabadiliko kidogo na kuweka wepesi fulani, na kuzifuta baadhi ya hukumu zilizo kuwa ukiwawiya ugumu utekelezaji wake.

Kwa uchache, haya ndio tuliyo jaaliwa na Allah Mtukufu katika kusomeshana kwetu Sira ya Bwana Mtume kupitia darsa letu hili, kwa juma hili.

Tunataraji kwamba tunafuatana pamoja, tumuombe Allah azibariki juhudi zetu hizi ili zipate kutunufaisha leo hapa duniani kabla ya kesho kule akhera tutakapo kutana na kipenzi chetu; Mtume Muhammad kwenye makaazi ya milele. Tukutane juma lijalo kwa mapenzi yake Mola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *