SOMO LA TANO-KUTAYAMMAMU

i) WEPESI WA UISLAMU NA MAANA YA KUTAYAMAMU

Tumekwishajua kutokana na maelezo ya masomo yaliyopita kwamba udhu ni sharti ya kusihi kwa swala, tawafu (ibada ya kuizunguka Al -kaabu), kuushika na kuuchuka/kuubeba msahafu.

Kadhalika tumefahamu kuwa udhu hupatikana kwa kutumia maji katika viungo makhsusi. Sote tunakubaliana na hakika/ukweli kuwa mwanadamu kama viumbe hai wengine ni viumbe mwenye tabia ya kubadilika kutoka hali moja kwenda katika hali nyingine iliyo tofauti na ile ya mwanzo au kutoka katika mazingira hadi mengine.

Sasa kwa kuizingatia kanuni/sheria na tabia hii ya kimazingira, inawezekana kabisa ikamtokea mwanadamu hali au mazingira ambayo atashindwa kuyatumia maji kwa ajili ya udhu au josho.

Anaweza akayakosa maji katika maeneo aliyomo wakati ule, au maji yakawa yanapatikana maeneo ya mbali sana na ikamuwia taabu kuyafikia, au akawa na maradhi ambayo yanamzuilia kutumia maji katika hali na mazingira kama haya, muislamu afanye nini na ilhali imemlazimu kuitekeleza ibada ya swala na ni maalum kuwa ibada hii haitekelezeki bila ya kuwa na udhu.

Sasa je, aache kuswali kwa sababu ya kukosa au kushindwa kuyatumia maji ? Au ayatumie maji hata kama yanamdhuru ili apate udhu utakaomuwezesha kuswali ? La, hasha ! Hapo sasa ndio inaonekana kazi ya msingi miongoni mwa misingi ya fiq-hi ya kiislamu usemao: “HAPANA KUDHURU (MTU) WALA KUJIDHURU MWENYEWE.”

Kutokana na msingi huu tumeelewa kuwa kumbe hakuna katika Uislamu kujitia katika madhara kwa sababu ya kuutekeleza Uislamu. Msingi huu si dhana tu iliyosimikwa na kuwekwa na wanazuoni bali unaitegemea kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“…WALA MSIJITIE KWA MIKONO YENU KATIKA MAANGAMIZO …” [2:195].

Kupitia msingi huu ndipo unapojitokeza na kuonekana wepesi wa dini na mfumo huu sahihi wa maisha unaokwenda sambamba na hali, tabia na mazingira ya mwanadamu.

Katika hali na mazingira kama hayo ndio uislamu ukamuwekea mwanadamu huyu sheria ya kutayamamu kwa kutumia mchanga tahara badala ya kutumia maji katika udhu au josho.

Uislamu umetoa ruhusa hiyo ili kumpa fursa mwanadamu huyu ya kuitekeleza ibada bila ya tabu au madhara na kuziba mwanya wa kuacha kutekeleza ibada kwa kisingizio cha kukosa maji au maradhi yanayozuia utumiaji wa maji. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu:
“…ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI NA WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO …” [2:185]

Tusome tena ili tuzidi kuuona wepesi wa Uislamu
“….HAPENDI ALLAH KUKUTIENI KATIKA TAABU ..” [ 5:6]
“… WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI .” [22: 78]

Baada ya kuona ni jinsi gani uislamu ulivyomuwekea muislamu mazingira mepesi katika kuutekeleza uislamu. Hebu sasa tujaribu kuiangalia tayamamu kwa ujumla, tukianzia na maana ya kutayamamu.

Tayamamu ni neno la Kiarabu ambalo tumezoea kulitamka kama “kutayamamu”.

Neno hili lina maana mbili zifuatazo:
Maana ya kilugha: Katika lugha ya Kiarabu neno tayamamu lina maana ya kukusudia.

Maana ya kisheria: Kutayamamu ni kupakaza vumbi la mchanga twahara katika uso na mikono kwa utaratibu maalum uambatano na nia.

(ii) HUKUMU NA DALILI YA KUTAYAMAMU

Kutayamamu ni WAJIBU/FARDHI kwa mtu katika hali mbili:1: Wakati atakapoyakosa maji ya kutawadhia.2: Wakati atakaposhindwa kuyatumia maji kwa sababu zilizobainishwa na sheria.Kutayamamu kumethibiti katika Qur-ani Tukufu, Sunnah na Ijmaa.

Dalili ya kutayamamu katika Qur-ani ni kauli tukufu ya Mwenyezi Mungu: “………… NA MKIWA WAGONJWA AU MMO SAFARINI, AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI AU MMEINGILIANA NA WANAWAKE NA HAMKUPATA MAJI, BASI KUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI (twahara) NA KUUPAKA NYUSO ZENU NA MIKONO YENU …” [5:6].

Tayamamu katika Sunnah imo katika kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema : “….na tumejaaliwa (tumefanyiwa) ardhi yote kuwa ni msikiti (mahala pa kuswalia) na mchanga (udongo) wake umefanywa kwetu ni twahara (utwahirishayo) tutakapokuwa hatukupata maji”. Muslim.

Ama Ijmaa, wanazuoni wote wamekogomana na kukubaliana kuwa tayamamu imefanywa kuwa ni sheria, itumike badala ya ya udhu na josho katika hali na mazingira maalum yaliyobainishwa na sheria.Hiyo ndiyo tayamamu ndani ya Qur-ani, Sunnah na Ijmaa.

(iii) FALSAFA NA HEKIMA YA KUTAYAMAMU

Kutayamamu kumefanywa kuwa ni sheria miongoni mwa sheria za uislamu ili kumfanya muislamu aweze kuitekeleza ibada katika hali na mazingira mbalimbali yanayomzunguka.

Apate wepesi katika kulitekeleza lengo la kuumbwa kwake ambalo ni ibada kwa maana halisi ya neno hilo. Tayamamu ni hadiya na zawadi ya Mola kwa umati Muhammad, sheria hii haikuwepo katika nyumati zilizoutangulia uma huu.

Haya yanathibitishwa na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie: “Nimepewa (mambo) matano, hakupata kupewa mtume yeyote kabla yangu; Nimenusuriwa na khofu kitambo cha mwezi mzima, na nimefanyiwa ardhi kuwa ni msikiti na twahara, basi popote pale mtu katika umati wangu itakapomdiriki swala na aswali. Na nimehalalishwa ngawira na hazikuhalalishwa kwa heyote kabla yangu, na nimepewa shafaa (uombezi kwa watu). Mtume alikuwa akipelekwa kwa watu wake tu na mimi nimepelekwa kwa watu wote.” Bukhaariy na Muslim.

Itakuwazikia kutokana na hadithi hii ya Bwana Mtume kuwa kutayamamu ni fursa maalumu ya upendeleo uliyopewa muislamu na Mola wako ili kukuwepesishia utekelezaji wa ibada zako.

(iv) NAMNA YA KUTAYAMAMU

Kwa kuwa tayari tumeshathibitisha kwamba tayamamu ni sheria katika uislamu, sheria hii haikuachwa ielee angani na kumpa fursa kila mtu aitekeleze kwa mujibu wa matakwa na matashi yake.

Sheria hii imewekewa utaratibu maalumu wa kuitekeleza na mwenyewe Mwenyezi Mungu na kubainisha na Bwana Mutume kiutendaji. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia ndani ya Qur-ani: “………. BASI KUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI (twahara) NA KUUPAKA NYUSO ZENU NA MIKONO YENU….…..” (5:6).

Haya ni maelekezo na maelezo ya jumla kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia tutayamamu kwa kutumia mchanga, tuzipakaze nyuso na mikono yetu. Swali linajitokeza tupakaze vipi, namna ya upakaji inakuwa je ?

Hapa sasa ndipo inapoonekana nafasi na umuhimu wa Bwana Mtume na kwamba bila yeye dini hii haieleweki na wala haitekelezeki. Yeye ndiye aliyetoa maelezo na kuonyesha namna ya kutayamamu mbele ya maswahaba ili kuitekeleza kiutendaji aya hiyo na kuufundisha uma jinsi ya kuitekeleza sheria hii ya tayamamu.

Sasa basi ili tayamamu ya mtu ikubalike kisheria ikiwa ni pamoja na ibada atakayoifanaya kwa tayamamu hiyo ni lazima ahakikishe kuwa anatayamamu kwa mujibu wa utendaji na maelekezo ya Bwana Mtume.

Ifuatayo ndiyo namna ya kutayamamu kama alivyofundisha Bwana Mtume:-Kwanza kabisa andaa mafungu/marundo mawili ya mchanga ulio twahara. Halafu elekea Qibla, sema; BISMILLAAH, piga mikono yako juu ya fungu moja la mchanga huku ukisema moyoni mwako NAWAYTUS – TIBAAHATI FARDHWIS – SWALAA Kung’uta mchanga kidogo na upakaze uso wako kwa mikono yote miwili vumbi lililobakia katika vitanga hivyo kama unavyouosha uso katika udhu. Halafu piga tena kwa vitanga vyako katika lile fungu la pili la mchanga, kung’uta mikono yako kidogo. Kisha upakaze mkono wa kulia kwa mkono wa kushoto na upakaze ule wa kushoto kwa mkono wa kulia. Zingatia kupakaza vumbi ni mara moja moja tu na sio mara tatu kama ilivyo katika kutawadha.

TUJIFUNZE NA TUKUBALI: kuwa tayamamu ni miongoni mwa sheria ambazo zinazothibitisha kuwa uislamu ni dini na mfumo sahihi wa maisha unaokwenda sambamba na kukubaliana na umbile la mwanadamu.

Sheria na hukumu zote za dini hii zimezingatia mambo mawili makuu:-Umbile la mwanadamu, na Mazingira yake.

Kwa mantiki hii sheria na hukumu zote za uislamu zinatekelezeka bila ya matatizo yoyote. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu, “UELEKEZE USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWA SAWA, NDILO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU. (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu) HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIYO DINI ILIYO HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI” [30: 30].

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *