SOMO LA TANO –01 MUHAMMAD; MTUME WA MWISHO-Rehema na Amani zimshukie-Na uhusiano/mafungamano ya ujumbe (da’awa) wake na jumbe za mbinguni zilizo tangulia.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-ni juma jingine tena, kwa auni na uwezeshi wake Mola, tumekutana katika darsa zetu za Sira yake Bwana Mtume, leo tunaendelea kuangalia uhusiano/mafungamano ya Risala ya Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na Risala za kabla yake.

Tunasema hali ya kumtaraji Allah atuongoze kusomeshana yale yaliyo ndiyo, yale yatakayo tunufaisha sote na kutusogeza karibu zaidi na Bwana Mtume ili tuweze kumuiga na kumfuata:

Naam, ili tupate kwenda sawa katika darsa ya leo, tukumbushane pale tulipo ishia juma lililo pita:

Katika maneno yake hayo, Nabii Isa-Amani imshukie-anawabainishia Wana wa Israili ya kwamba yeye katika mambo yanayo fungamana na Akida, ni mwenye kuyasadikisha na wala si kuyatengua yale yaliyomo ndani ya Taurati miongoni mwa hukumu.

Na tena ni mwenye kuyathibitisha hayo na kuhuisha ulinganiaji (uhubiriaji) wa hayo. Ama kwa upande wa uratibu wa sheria na hukumu za halali na haramu, amepewa jukumu la kufanya mabadiliko kidogo na kuweka wepesi fulani, na kuzifuta baadhi ya hukumu zilizo kuwa ukiwawiya ugumu utekelezaji wake.

Na kwa kujengea juu ya maelezo hayo, tutafahamikiwa ya kwamba risala/ujumbe/da’awa ya kila Mtume inakusanya mambo mawili; Akida na Sheria.

Ama tukiitazama hiyo Akida, basi kazi/dhima yake si nyingine zaidi ya kuithibitisha Akida hiyo hiyo ambayo walitumwa kuileta mitume walio tangulia. Kuithibitisha pasina tofauti yoyote au mabadiliko, bali inabakia vile vile katika uasili wake, ni kitu ambacho Mitume wanapokezana kijiti katika mbio zile zile.

Ama uratibu/uwekwaji wa sharia, basi hakika kila sharia ya Mtume wa zama zilizopo inaifuta ile sharia iliyo tangulia ila ile sharia inayo tiliwa nguvu na hii ya sasa, au ile hukumu ambayo imenyamaziwa na sharia ya sasa.

Na hilo linasemwa na wale wasemao: Sharia ya wa kabla yetu, hiyo ni sharia yetu pale ambapo haikupokewa inayo khalifiana nayo (katika Sharia yetu).

Kupitia maelezo yote yaliyo tangulia tangu katika darsa lililo pita, inatuwazikia na kutubainikia ya kwamba, hakika ya hali ilivyo hakuna dini nyingi za mbinguni lakini kilichopo ni sheria nyingi za mbinguni.

Ambazo hizo, iliyo tangulia inafutwa hukumu yake na hii ya sasa mpaka ilipo letwa sheria ya mwisho ya mbinguni. Ambayo hekima ya Allah imehukumia mfikishaji na mletaji wa sheria hiyo awe ni mtume wa mwisho; Muhammad-Rehema na Amani zimshukie.

Ama tukikubali au tukikataa, dini ya haki ni moja tu ambayo mitume wote wametumwa kuilingania na kuwaamrisha watu kuipokea na kuifuata, tangu Mtume wa mwanzo; baba yetu Adam-Amani imshukie-mpaka Mtume wa mwisho; Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Na dini hiyo si nyingine ila ni Uislamu.

Wametumwa kuihubiri na kuileta dini hiyo Ibraahim, Ismail na Ya’akuub-Amani iwashukie. Allah Mtukufu anasema: “Na nani atajitenga na mila ya Ibraahim isipokuwa anaye itia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini sisi tulimteua yeye katika dunia, na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema. Na Mola wake Mlezi alipo mwambia: Silimu, nyenyekea! Alinena: Nimesilimu, nimenyenyekea kwa Mola wa walimwengu wote. Na Ibraahim akawausia wanawe, na pia Ya’akuub: Nyinyi wanangu! Hakika Allah amekuteulieni dini hii, basi msife ila nanyi mmekuwa Waislamu, wanyenyekevu”. Al-Baqarah [02]:130-132

Na kwa dini hiyo hiyo, alitumwa Musa-Amani imshukie-kwa Wana wa Israil. Allah Mtukufu anasema kuhusiana na wachawi wa Firauni: “Wakasema: Sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. Nawe hukuudhika nasi ila kwa kuwa tumeziamini aya (ishara) za Mola Mlezi wetu zilipo tujia. Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie uvumilivu na utufishe hali ni Waislamu”. Al-A’araaf [07]:125-126

Na Isa-Amani imshukie-naye ametumwa kuleta na kuihubiri dini hiyo hiyo. Allah Ataadhamiaye anasema: “Na alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri, alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Allah? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Allah. Tumemuamini Allah, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu”. Aali Imraan [03]:52

Pengine mtu anaweza kusema: Ikiwa hivyo ndivyo basi, kwa nini wale wanao jinasibisha na Nabii Musa-Amani imshukie-wanafuata Akida maalumu inayo tofautiana na Akida ya Tauhidi iliyo letwa na Mitume wote? Na ni kwa nini wale wanao jinasibisha kwa Nabii Isa-Amani imshukie-wanaiamini Akida nyingine maalumu?

Jibu la swali hilo, ni yale aliyo yasema Allah Atukukiaye ndani ya kitabu chake kitukufu: “Bila ya shaka Dini mbele ya Allah ni Uislamu. Na walio pewa kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao…”. Aali Imraan [03]:19

Na aliyo yasema ndani ya Surat As-shuuraa [42]:13 baada ya neno lake: “Amekuamrisheni dini ile ile aliyo muusia Nuhu na aliyo kufunulia wewe…”. “Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka pangeli hukumiwa baina yao. Na hakika walio rithishwa kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo wahangaisha”. As-shuuraa [42]:14

Kwa hivyo basi, litakiwalo kufahamika na kueleweka ni kwamba Mitume wote walitumwa kuleta kwa wanaadamu wote Uislamu ambao ndio dini inayo tambulika na kukubalika mbele za Allah. Na watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo) wote wanajua fika ya kwamba dini ni moja kama wanavyo jua ya kwamba mitume hawakuja kwa jingine isipo kuwa kusadikishana; mfuatizi kumsadikisha mtangulizi wake katika dini aliyo ileta.

Na wala hawakuja kutofautiana katika Akida zisizo fanana, lakini wao watu wa Kitabu ndio walio khitalafiana na kufarikiana na wakawazulia Mitume wao wasiyo yasema wala kuyafundisha.

Pamoja na kujua kwao kwamba hayo si katika mafundisho ya mitume wao, lakini walifundishana na kurithishana hivyo hivyo kwa sababu ya chuki zilizopo miongoni mwao, kama alivyo sema Allah Atukukiaye.

Darsa letu la leo linakomelea hapa huku tukitaraji kwa msaada wake Mola utakuwa tayari umesha ujua japo kwa kiwango kidogo uhusiano/mafungamano ya Risala ya Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na Risala za kabla yake.

Kujua ambako kunazidi kukujaza yakini juu ya dini yako ya Uislamu, iliyo letwa na kufundishwa na Mitume wote-Amani iwashukie. Hadi juma lijalo tunasema: Maa Salaama!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *