“KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”
Shukrani zote ni stahiki na milki yake Allah Mtukufu, aliye uumba ulimwengu kwa utashi, uwezo, malengo, mpangilio na makadirio yake maalumu na akaiumba Akhera kwa ajili ya hisabu na jazaa. Sala na salamu zimuendee mbora wa walio oa na kuishi na wake kwa wema. Ziwaendee kadhalika Aali, Sahaba na umati wake wote.
Ndugu mdau wa jukwaa letu hili la kila juma-Allah akurehemu. Kwa mara nyingine tena, Mola wetu Mtukufu anatukutanisha katika ukumbi na jukwaa letu hili ili kutupa fursa ya kuendelea kukumbushana kuhusiana na Familia ya Kiislamu. Tumuombe Mola wetu Mkarimu kwa ukarimu na neema zake atujaalie kuwa miongoni mwa wale ambao wanapo kumbushwa, haraka hukumbuka na wakayafuata makumbusho.
Juma hili katika jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu, tutaendelea kuongozwa na somo lenye anuani isemayo:
- Malengo/Makusudio ya ndoa:
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma lililo pita kwa auni na msaada wake Allah tulianza kuangalia na kujifunza malengo makuu ya ndoa ambayo tulisema ya kwamba tukiyajumuisha pamoja yanaangukia katika mafungu makuu matatu. Na tayari juma lililo pita tumekwisha kujifunza lengo msingi la ndoa, ambalo tulisema ni kupata watoto. Leo kwa uwezeshi wake Mola tutaliangalia lengo la pili la ndoa ambalo ni:
- Kujikinga/kujihifadhi na haramu:
Katika jumla ya mambo ambayo yasiyo na shaka ndani yake, ni kwamba miongoni mwa malengo makuu ya ndoa, ni mtu kupata kinga itakayo mkinga na kumuhifadhi dhidi ya zinaa na baki ya machafu mengine yanayo tendwa na tupu. Na wala si tu kukidhi na kushibisha matamanio ya kimwili. Ni kweli na ni sahihi kabisa, kwamba kukidhi matamanio ndio sababu ya kujikinga/kujihifadhi na haramu; zinaa na jamaa zake. Lakini huko kujikinga na zinaa hakuthibiti na wala hakutimii ila tu kwa kupatikana kusudio na nia, kwa hivyo basi hakusihi kuyatenganisha mambo hayo mawili; kukidhi matamanio na kusudio/nia ya kujikinga na haramu. Hivyo ni kwa sababu mwanaadamu atakapo ielekeza hima yake yote kwenye kukidhi matamanio ya mwili na akafanya tendo la ndoa mara baada ya mara na wala lisiwe kusudio na nia yake katika tendo hilo ni kuikinga nafsi yake kutokana na uchafu wa zinaa. Huyo atakuwa na tofauti gani na hayawani wengine ambao wao hufanya tu tendo la ndoa kila wanapo jisikia kufanya hivyo na ambao kwao hakuna ndoa na wala hawaitambui kamwe zinaa?!
Kwa minajili hiyo basi, ni lazima kila mmoja; mume na mke awe na lengo tukufu wakati akiliendea tendo la ndoa na mwenza wake, na lengo hilo lisiwe lingine zaidi ya kuyashibisha matamanio kwa njia ya halali ili kupata kinga dhidi ya haramu. Na hilo ndilo analo tuongozea kwalo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia wito wake kwa vijana, pale alipo sema: “Enyi kongamano la vijana! Atakaye imudu ndoa, basi na aoe, kwani huko kuoa kunalifumba mno jicho (kutizama haramu) na kunaihifadhi mno tupu (kuepukana na zinaa). Na asiyekuwa na uwezo (wa kuoa), basi na ajilazimishe kufunga, kwani huko kufunga ni kinga kwake yeye”. Bukhaariy [5065], Muslim [1400], Nasaa [2046], Tirmidhiy [1081], Ibn Maajah [1845] & Ahmad [424]-Allah awarehemu.
Maana ya kauli hii ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa vijana, anawaambia: Enyi vijana! Yeyote miongoni mwenu anayeweza kumuingilia mwanamke na akawa na uwezo wa kumudu majukumu na gharama za ndoa, basi huyo na aoe. Kwani huko kuoa kunalifumba mno jicho na kulizuia kuangalia yaliyo ya haramu na kunailinda na kuihifadhi tupu kuepukana na zinaa. Na kama anaweza kujamii lakini hamudu majukumu na gharama za ndoa, basi na ajilazimishe kufunga, kwa sababu huko kufunga kunayavunja vunja makali ya matamanio na kumpelekea kutokumuasi Allah kupitia mlango wa zinaa.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-lililo wazi katika Hadithi hii ni kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ameiratibia na kuiandamizia ndoa mambo mawili ambayo yanamsaidia mwanandoa; mume na mke, mambo hayo ni:
- Kufumba jicho, kuliepusha kutazama/kuangalia/kukodolea macho wanawake ambao Allah amemuharimishia, na
- Kuilinda/kuihifadhi tupu dhidi ya zinaa na machafu mengine kama liwati na ndugu zake.
Maana na ufafanuzi huu tulio uelezea ndio unao tajwa na Hadithi hii iliyo pokewa na Jaabir bin Abdillah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Mmoja wenu atakapo pendezwa (vutiwa) na mwanamke na akaingia moyoni mwake, basi haraka na amuendee na kumuingilia mke wake, kwani kufanya hivyo kutayaondosha (matamanio) yaliyo ingia ndani ya nafsi (moyo) yake”.
Ama wale wanao ingia kwenye ndoa na hima na makusudio yao ya kuoa/kuolewa yakiwa ni matamanio ya kujamiiana tu na si kingine, basi hao kujamiiana hakutawazidishia ila matamanio juu ya matamanio, na hao ndio ambao hawatosheki na mke/mume wake wa halali. Bali hao ndio wanao thubutu kutoka nje ya ndoa zao/kuchepuka.
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]
“Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74
Ewe Mola wa haki! Ewe ambaye unaye samehe madhambi yote! Tunakuomba utusamehe madhambi yetu na ya familia zetu, uzitwahirishe nyoyo zetu na za familia zetu, uzihifadhi tupu zetu na zile za familia zetu, uzifanye njema tabia zetu na zile za familia zetu na uzijaze nyoyo zetu sote nuru na hekima. Hakika Wewe ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. Yaa Allah tutakabalie dua!
Kwa juma hili haya ndio tuliyo wafikiwa na Allah kukumbushana, tulilo patia katika hayo ni kwa taufiki yake Allah Mola Muwezeshi na tulilo kosea miongoni mwayo linatokana na mapungufu ya kibinaadamu, kwani ukamilifu ni wake Allah pekee. Tumuombe Mola wetu Mkarimu azidi kututunukia neema ya uhai, uzima na ufahamu ili juma lijalo kwa uweza wake tuendelee kuzinduana na kukumbushana yale yanayo husiana na Familia ya Kiislamu.
Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “Na asiye weza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia. Na Allah ni Mjuzi wa Imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada…”. An-Nisaa [04]:25
Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.