SOMO LA PILI .04

 Hadhi, nafasi na daraja ya mji wa Makka katika Uislamu

SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-juma lililo pita tulijifunza na kuangalia mchango na ushiriki wa Waislamu wale wa mwanzo katika ujenzi wa nyumba kongwe ya ibada (Al-Ka’aba) na ambayo ndiyo chimbuko la mji wa Makka. Leo kwa msaada wake Mola, tuiangalie nafasi, hadhi na daraja ya mji wa Makka katika Uislamu.

Kwa jina lake Allah ambaye amezifanya bora baadhi ya sehemu juu ya sehemu nyingine, akaufanya mji wa Makka kuwa mtukufu na bora kuliko miji na sehemu zote za duniani. Tunasema hali ya kutaraji msaada wake:

Katika jumla ya mambo yanayo upa hadhi na daraja mji wa Makka:

  • Ni ule uwepo wa nyumba kongwe na ya mwanzo ya ibada ndani ya mji huo, kama anavyo litaja hilo Allah Mtukufu: “Hakika nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka (Makka), iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. Ndani yake zimo ishara zilizo wazi – makaamu (masimamio) ya Ibraahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani…”. Aali Imraan[03]:96-97
  • Hiyo ni nyumba ambayo huwakusanya watu wengi kwa wakati mmoja kila mwaka kwa ajili ya ibada, mkusanyiko ambao haupatikani mfano wake mahala pengine popote duniani. Hapo kwenye nyumba hiyo, watu huona raha, hupata amani na ladha ya kumuabudu Mola Muumba wao. Na nyumba kongwe hiyo huwakumbusha juu ya Mitume wa Allah na wakawaiga katika matendo yao mema mazuri, tusome: “Na kumbukeni tulipo ifanya ile nyumba (ya Al-Ka’aba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipo kuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kuswalia…”. Al-Baqarah[02]:125
  • Ndio mji ambao ni mahala pa amani, mji unao jiwa na kheri na riziki kutoka kila mahala zinazo letwa hapo ili kuijibu dua iliyo ombwa na Baba wa Mitume; Nabii Ibrahim-Amani imshukie. Hilo linaelezwa na Mwenyewe Mola ndani ya kitabu chake kitukufu: “Na alipo sema Ibrahim: Ewe Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Allah na siku ya mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya moto, napo ni pahala pabaya mno pa kurejea”. Al-Baqarah[02]:126
  • Allah ameuteua mji huo kuwa ndio mahala pa mazawa ya Mtume wake wa mwisho na ndio mahala pa kutumilizwa kwake (kupewa utume). Ni ndani ya mji huo basi, ndimo ilimo anza kushuka Qur’ani; kitabu cha mwisho, na ndani yake mji huo ndimo yalimo anza mahubiri ya kheri na haki na kuenea ulimwenguni kote. Allah Mtukufu anasema: “Na namna hivi tumekufunulia Qur’ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa miji (Makka) na walio pembezoni mwake…”. As-shuuraa [42]:07
  • Allah amewajibisha kwa kila mtu mwenye uwezo kutoka pande zote za ulimwengu, kwenda huko, tena waingie kwenye mji huo kwa unyenyekevu, adabu na udhalili kwa Mola Mwenyezi. Tena wakiwa vichwa wazi na wakiwa wamevua mavazi ya watu wa Dunia. Hayo ndio mapendeleo ya kauli yake Allah Mtukufu pale alipo sema: “…na kwa ajili ya Allah kumewawajibikia watu kuhiji kwenye nyumba hiyo, kwa yule awezaye njia ya kwendea. Na atakaye kanusha, basi Allah si Muhitaji kwa walimwengu”. Aali Imraan [03]:97
  • Kwenda kwenye mji huo, kunafuta na kupomosha dhambi za mja. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakaye kuja kwenye nyumba hiyo (Al-Ka’aba) na asiseme maneno machafu wala kutenda matendo machafu, atarejea (kwake akiwa msafi) kama (ile siku) aliyo zaliwa na mama yake”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
  • Ni mji mtakatifu wa Allah, tusome: “Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu, aliye ufanya mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea”. An-namli [27]:91
  • Ni mji ambao haitakikani humo kumwagwa damu wala kuwindwa mnyama, wala kukatwa mti, wala kung’olewa mimea na wala hakiokotwi kitu ila tu kwa ajili ya kukitangaza. Hayo yamebainishwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika hadithi iliyo pokewa na Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-pale alipo sema: “Allah ameifanya Makka kuwa mji mtukufu, na haukumuhalalikia yeyote kabla yangu wala baada yangu, nimehalalishiwa mimi muda katika mchana. Haing’olewi mimea yake, wala haikatwi miti yake, wala hawakurupushwi wanyama wake na wala hakiokotwi kitu chake ila kwa atakaye kitangaza…”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
  • Huwa mara dufu ujira na thawabu za amali inayo tendwa humo, kwani swala moja inayo swaliwa kwenye msikiti mtukufu kiujira ni sawa na swala laki moja zinazo swaliwa kwenye misikiti mingine.
  • Limo kwenye mji huo Hajarul-Aswad – jiwe jeusi kutoka peponi ambalo kulibusu kumefanywa kuwa sharia na wala hakuna mahala pengine popote katika uso wa ardhi ambapo ni sharia kupabusu zaidi ya jiwe hilo tu.
  • Ndio mji ambao umehifadhiwa na Allah dhidi ya Masihi Dajjaali, basi hataweza kuingia humo. Imepokewa na Anas bin Maalik-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba yeye amesema: “Hapana mji wowote ila ataukanyaga Dajjaali, isipokuwa Makka na Madina kwani hapana njia yake yoyote ila itakuwa na malaika walio panga safu kuilinda. Kisha Madina itawatetemesha watu wake mitetemo mitatu, basi Allah atamtoa humo kila kafiri na mnafiki”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Kwa kauli jumla, tukubali au tusikubali, mji wa Makka una daraja na hadhi kubwa sana si tu kwetu sisi wanaadamu bali hata mbele za Allah na Mtume wake. Allah ameuchagua uwe ndio mji wake mtakatifu na umo humo msikiti mtukufu kuliko misikiti yote ya dunia nzima, msikiti ambao waislamu wote huuelekea kila siku mara tano, kwa kuswali na kumuabudu Mola wao. Na atakaye swali bila ya kuelekea huko, swala yake ni batili, haikubaliki.

Hapa tulipo fikia, ndio tamati ya darasa letu la juma hili. Tumuombe Allah; Mola Mlezi wetu asitunyime baraka na fadhila za mji mtukufu wa Makka na wala asitufishe ila nasi tumehiji kwenye nyumba yake kongwe. Aturuzuku kwa fadhila zake mahaba ya Mtume mzaliwa wa mji huo na atuwezeshe kumfuata kikweli. Sote tuseme: Aaamin!

Na tukutane juma lijalo kwa uwezo na matashi yake Mola. Maa Salaam!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *