SOMO LA PILI NO .03

Mchango wa Ibn Zubeir na watu wengine katika ujenzi wa Al-Ka’aba.

SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

  1. Mchango wa Ibn Zubeir na watu wengine katika ujenzi wa Al-Ka’aba.

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-juma lililo pita tulijifunza awamu ilizo pitia Al-Ka’aba katika ujenzi wake, leo tena tunaendelea na somo hilo lakini kwa kuangalia mchango na ushiriki wa Waislamu wa mwanzo katika ujenzi huo. Kwa jina lake Allah tunasema hali ya kutaraji msaada wake:

Pale ambapo Swahaba Ibn Zubeir-Allah amuwiye radhi-alipo pendekeza na kuamua kujengwa upya kwa Al-Ka’aba, Waislamu walimuitika na wakalibomoa jengo lote la Al-Ka’aba tayari kwa ujenzi mpya. Wakasimamisha nguzo kuizunguka Al-Ka’aba, halafu wakaanza kazi ya ujenzi na wakazidisha urefu na upana kuliko lilivyo kuwa kabla ya kubomolewa. Na wakaliwekea milango miwili; mlango upande wa Mashariki na mwingine upande wa Magharibi. Mlango mmoja ukiwa ni kwa ajili ya kuingilia ndani na mwingine wa kutokea nje.

Ujenzi huo mpya ulifanywa kwa kuitegemea kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-iliyo pokewa na Imamu Bukhaariy na Muslim-Allah awarehemu: “Ewe Aisha! Lau si kuwa watu wako ndio wametoka kwenye jahiliya hivi karibuni, basi ningeliamrisha ibomolewe Al-Ka’aba, kisha nikayatia humo yale yaliyo tolewa. Na ningeifanya sawa na ardhi, na nikaiwekea mlango wa Mashariki na mlango wa Magharibi na nikaifikisha kwenye misingi ya Ibrahim”. [Rejea AL-BIDAAYAH WAN-NIHAAYAH cha Ibn Kathiir 01/320]Au maneno yenye maana sawa na haya.

Ametaja Al-Azraqiy-Allah amrehemu-katika kitabu AKHBAARU MAKKAH [01/64]: Ya kwamba Mtume Ibrahim-Amani imshukie-aliufanya urefu wa jengo la Al-Ka’aba kwenda juu kuwa dhiraa tisa na urefu wake wa chini kuwa dhiraa thelathini na mbili na upana dhiraa ishirini na mbili. Na jengo halikuwa na paa (halikuezekwa).

Na amesimulia Imamu Suhailiy-Allah amrehemu: Ya kwamba urefu wa jengo la Al-Ka’aba wakati wa Nabii Ismail-Amani imshukie-ulikuwa ni dhiraa tisa. Wakati Makuraishi walipo lijenga kabla ya Uislamu wakaongeza dhiraa tisa nyingine, kwa hivyo urefu wake ukawa ni dhiraa kumi na nane. Mlango wakauinua ukawa juu, ikawa mtu hawezi kuingia ndani ila kwa ngazi. Kisha tena alipo lijenga jengo hilo Ibn Zubeir, naye akaongezea urefu wake kwa dhiraa tisa, jumla urefu wake ukawa dhiraa ishirini na saba…”. AR-RAUDHWU AL-UNFU [01/221]

Msikiti mtukufu haukuwa na uzio na ulikuwa umezungukwa na nyumba kwa pande zake zote. Na wakati ambapo Sayyidna Umar bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-alipo ona msikiti umekuwa finyu kutokana na wingi wa Mahujaji na Wafanya ziara, alinunua nyumba zinazo uzunguka msikiti kwa makubaliano na wamiliki wake. Akaupanua msikiti na akauwekea uzio wenye urefu wa kimo cha mtu na akauzungushia taa. [Rejea AR-RAUDHWUL AL-UNFU 01/224]

Na katika awamu ya Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-alipo ona ya kwamba msikiti umekuwa finyu kutoka na idadi kubwa ya Mahujaji na wafanyao Umrah, naye akanunua nyumba nyingine. Akaupanua msikiti na eneo linalo uzunguka. Al-Azraqiy [02/69]

Na kama hivyo ndivyo alivyo fanya Ibn Zubeir. Al-Azraqiy [02/69-70]

Kisha tena ndio makhalifa na maamiri wa zama hizo, wakaendelea kufanya upanuzi wa eneo la Haram mpaka katika zama zetu hizi ambamo tumeshuhudia upanuzi na maboresho makubwa mno ya sehemu za ibada unao fanywa na Serikali ya Saudi Arabia. Allah awajaze kheri wote walio shughulika na kazi tukufu ya ujenzi wa Al-Ka’aba na upanuzi wa msikiti mtukufu na eneo lake.

  1. Makaamu Ibraahim-Amani imshukie.

Ndugu msomaji wetu-Allah akurehemu-neno hili “Maqaamu” ni neno lenye asili ya Kiarabu ambalo limetajwa na Mola katika kitabu chake kitukufu pale alipo tuagiza: “Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Al-Ka’aba) iwe pahala pa kukusanyikia na pahala pa amani. Na Maqaamu Ibraahim(mahala alipokuwa akisimama) pafanyeni pawe pa kusalia…”. Al-Baqarah [02]:125

Na akasema: “Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyo Bakka (Makka), iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. Ndani yake zimo ishara zilizo wazi – Maqaamu Ibraahim(masimamio ya Ibraahim)…”. Aali Imraan [03]:96-97

Kupitia aya mbili hizo tulizo zinukuu, inatubainikia ya kwamba kumbe “Makaamu Ibraahim” ni: Lile jiwe ambalo alikuwa akisimama juu yake Nabii Ibraahim-Amani imshukie-wakati wa ujenzi wa Al-Ka’aba pale jengo lilipo inuka juu kuliko urefu wa kimo chake. Na nyayo zake ziliacha athari/alama juu ya jiwe hilo na athari hiyo iliendelea kubakia na kuonekana mpaka mwanzoni mwanzoni mwa Uislamu. Kisha ikafutika kutokana na kuguswa na mikono ya watu kwa ajili ya kutabaruku.

Na imepokewa ya kwamba Makaamu ilikuwa imeshikana na ukuta wa Al-Ka’aba tangu zamani mpaka katika zama za ukhalifa wa Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi. Yeye ndiye aliye itenganisha kidogo Makaamu na Al-Ka’aba ili kutoa mwanya kwa wenye kutufu na wenye kuswalia kwenye Makaamu na maswahaba wakaliwafiki na kulikubali hilo lililo tendwa na Al-Faarouq Umar. [Rejea FADHWAAILUS-SWAHAABA cha Ahmad 01/324, AKHBAARU MAKKA 02/33 & AL-MUSWANNAFU 05/48]

Na huku kuwafikiwa Sayyidna Umar na maswahaba si jambo geni, kwani yeye alikwisha wafikiwa na Allah kwa kauli yake alipo mwambia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Waonaje, lau tungeli pafanya Maqaamu Ibraahim kuwa ni mahala pa kuswalia”. Allah Ataadhamiaye akateremsha aya inayo somwa mpaka siku ya Kiyama: “…Na Maqaamu Ibraahim(mahala alipokuwa akisimama) pafanyeni pawe pa kuswalia…”. Al-Bukhaariy [01/504] & Ahmad [01/23]-Allah awarehemu.

Si vibaya bali inafaa tukadokezea hapa ya kwamba Nabii Ibraahim-Amani imshukie-pia ndiye aliye ujenga msikiti wa Al-Aqswaa; mmojawapo wa ile misikiti mitatu mitukufu iliyo tajwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na ipo kauli nyingine inayo sema ya kwamba Nabii Yaaquub-Amani imshukie-ndiye aliye weka misingi ya msikiti wa Al-Aqswaa.

Ndugu msomaji wetu-Allah akurehemu-darasa leo juma hili linaishia hapa na kwa uwezo wake Mola tunataraji umesha uona mchango wa Waislamu wenzetu wa mwanzo katika ujenzi wa nyumba tukufu ya Allah; Al-Ka’aba na kwamba utakuwa umejifunza kitu katika hilo. Kwamba na wewe pia mahala ulipo na kwa kile ulicho nacho; akili (elimu), nguvu au mali ni wajibu wako kushiriki katika kuuendeleza Uislamu kupitia ujenzi wa misikiti, madrasa na miradi mbali mbali itakayo dhamini ustawi wa Uislamu.

Tumuombe Allah atukutanishe tena juma lijalo, hadi wakati huo tunasema: Maa Salaamah!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *