“KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”
Shukrani zote ni stahiki na milki yake Allah Mtukufu, aliye uumba ulimwengu kwa utashi, uwezo, malengo, mpangilio na makadirio yake maalumu na akaiumba Akhera kwa ajili ya hisabu na jazaa. Sala na salamu zimuendee mbora wa walio lea na kujenga familia bora ya kupigiwa mfano. Ziwaendee kadhalika Aali na Sahaba walio jifunza ulezi katika Madrasati Muhammadiyya hata jamii yao ikawa ndio jamii bora ya kuigwa na kufuatwa na ziuendee pia umati wake wote.
Ndugu mpenzi na mdau wa jukwaa letu-Allah akurehemu. Tuna kila sababu ya kumuhimidi na kumshukuru Mola wetu Mkarimu kwa kutujaalia kukutana tena katika jukwaa letu hili, lengo mama likiwa ni kukumbushana yale ambayo ndani yake yamo manufaa na kheri yetu yenyewe.
Naam, baada ya kuizungumzia Familia kwa kiasi tulicho jaaliwa katika juma lililo pita na tukajua tunamaanisha nini pale tunapo izungumzia familia. Sasa basi, kwa kuwa Familia ya Kiislamu hupatikana na huasisiwa kupitia ndoa sahihi na si vinginevyo. Kuanzia juma hili na kuendelea, kwa msaada wake Mola wetu aliye tufundisha kwa msaada wa kalamu, tutaanza kuiangalia na kuizungumzia ndoa ambayo hiyo ndio kiwanda cha kuzalisha familia ambayo nayo huanzisha jamii na kisha kupatikana kwa Taifa.
- Utangulizi:
Cha mwanzo kabisa kutajwa wakati tunapo izungumzia familia, ni ndoa; kile kifungo kitakatifu ambacho Qur-ani imekichukulia kuwa ni katika jumla ya neema za Allah alizo waneemesha waja wake, tena ni miongoni mwa shuhuda zinazo onyesha uwezo wake Mola Muumba na utukufu wake. Hilo ndilo analo likusudia Allah Yeye aliye Mtukufu kupitia kauli yake tukufu: “Na katika ishara (aya) zake amekuumbieni wake zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri”. Ar-Ruum [30]:21
Ndugu mwana familia wa jukwaa hili-Allah akurehemu-hebu sote kwa pamoja tuyatafakari maneno yake haya Mola ambayo yanaitaja ndoa. Sote tunapaswa kufahamu na kujua ya kwamba, Qur-ani Tukufu hailitumii neno “aya” – ambalo Kiswahili tunalitafsiri kwa maana ya ishara/alama, ila katika mambo makubwa, mambo matukufu. Inafanya hivyo ili upate kujulikana na kuonekana utukufu, ukubwa na hekima ya Muumbaji. Hivyo tunaruhusika kabisa kusema ya kwamba ndoa ni katika jumla ya alama zinazo onyesha utukufu, ukubwa na hekima yake Mola katika uumbaji wake, kwa hivyo basi ndoa ni tendo tukufu na kubwa mno mbele zake Mola, wazazi na jamii kwa ujumla.
Naam, baada ya utangulizi huo mfupi unao itaja ndoa, ili tupate kwenda sawa kuanzia sasa na kuendelea, ni vema sote tukajiuliza:
- Nini ndoa:
Kiislamu na kwa mtazamo wa sharia, ndoa kwa maneno sahali; yenye kueleweka na kila mmoja; mwenye elimu na asiye nayo, ni kifungo ambacho kwa kufungwa kwake, kinamuhalalishia mwanandoa kuchanganyika na kustarehe na mwenza wake kimwili, ili kushibisha kiu ya kimaumbile iliyomo ndani yao.
Na kifungo cha ndoa, ndio bora ya vifungo vyote vilivyopata kufungwa na mwanaadamu kwa sababu hicho hakifungamani na mali wala maslahi bali kinafungamana na mtu mwenyewe na kinawaunganisha watu wawili kwa kamba ya mapenzi na huruma. Na pia ni kwa kuwa kifungo hicho ni sababu ya kupatikana kwa kizazi na kuhifadhi tupu kutokana na uchafu wa zinaa. Na ndoa ndio tendo pekee ambalo mwanaadamu hashirikiani na hayawani wengine, kwani kwao hao hayawani kuna tendo la ndoa na wala hakuna ndoa na ndio maana kwao hakuna nasaba kama ilivyo kwa jamii ya wanaadamu.
- Mahimizo ya ndoa ndani ya Qur-ani na Sunna:
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu na akuongoze kufahamu ya kwamba ndoa ni tendo na jambo tukufu ambalo limehimizwa na kusisitizwa na Qur-ani Tukufu kama ambavyo halikusahauliwa na Sunna. Haya sasa, kwa uzingativu na umakini mkubwa tuzisome aya zifuatazo na kisha tutafakari kwa pamoja. Allah aliye Mtukufu anasema:
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Allah ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Allah ni Mwenye kuwaangalieni”. An-Nisaa [04]:01
“…basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivyo ndio kutapelekea msikithirishe wana”. An-Nisaa [04]:03
“Na asiye weza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia. Na Allah ni Mjuzi wa Imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada…”. An-Nisaa [04]:25
“Na Allah amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Allah?” An-Nahli [16]:72
“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri”. Ar-Ruum [30]:21
“Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allah ni huyo aliye mchaMngu zaidi katika nyinyi. Hakika Allah ni Mwenye kujua, Mwenye khabari”. Al-Hujuraat [49]:13
“Na waozeni wajeni miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allah atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Allah ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua”. An-Nour [24]:32
Amesema kweli Mola wetu aliye viumba viwili viwili. Tukizitafakari aya hizi tulizo zinukuu, tutafahamikiwa ya kwamba zinabainisha na kueleza kuwa mwanamume na mwanamke, wawili hao ndio msingi wa:
- Uumbwaji; Allah ameijaza dunia kwa wanaume na wanawake wengi kutokana nao,
- Familia kupitia kuzaana kwao, na
- Jamii yote ya wanaadamu inayo undwa kutokana mjumuiko wa familia kadhaa.
Ni kwa ajili/sababu hizo, ndio Uislamu; Dini na mfumo kamili wa maisha ukaipangia na kuiwekea familia mpango/utaratibu wa kisharia wa muundo, mjengo na uendeshaji wake. Familia ambayo msingi/chimbuko lake kama linavyo tajwa na aya hizo hapo juu, ni watu wawili; mke na mume.
Ndoa ni umbile alilo umbiwa mwanaadamu, limo ndani yake; ndani ya mwili, akili na mawazo yake. Umbile ambalo Allah amelitia ndani ya waja wake wote; wanamume na wanawake na hilo linafahamika kupitia kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Basi uelekeze uso wako sawa sawa kwenye Dini – ndio umbile la Allah alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Allah. Hiyo ndio dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui”. Ar-Roum [30]:30
Kwa ukweli huu basi, haiingii akilini mtu mwanamume kuishi bila ya mwanamke na hali kadhalika mwanamke kuishi bila ya mwanamume na ni kwa ajili hiyo basi ndio sharia ya Kiislamu ikawafikiana na kurandana na umbile hilo la mwanaadamu, ikaukataa useja na ikakataza uruhubani. Na hapo ndipo Allah Mtukufu akasema: “…basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane…”. An-Nisaa [04]:03
Kwa kauli hiyo yake Yeye aliye Mtukufu, inatufahamikia ya kwamba wanawake ni kipendwa cha wanamume na kinyume chake na ni kwa sababu hiyo basi, ndio Uislamu ukahukumu mwanamume aungane na mwanamke kupitia tendo tukufu la ndoa ili kuunda familia inayo funikwa na mapenzi na huruma.
Na ili kuilinda nasaba ya mwanaadamu isipotee na apate kujulikana familia na ukoo wake na kuihifadhi familia kuchanganyika, Uislamu ukaiharimisha zinaa ili familia na jamii ipatikane kupitia ndoa. Allah ambaye aliye na utukufu akatuonya na kututahadharisha, akasema: “Wala msiukaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya”. Al-Israa [17]:32
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tutambue ya kwamba zinaa ni katika kundi la zile dhambi kubwa, ni haramu kuitenda dhambi hiyo kwa wale Waislamu ambao Qur-ani Tukufu imewasifia kwa kauli yake Mola wetu Mtukufu: “Na wale wasio muomba mungu mwengine pamoja na Allah, wala hawaiuwi nafsi aliyo iharimisha Allah isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara”. Al-Furqaan [25]:68
Na kutokana na ubaya wa dhambi hiyo, Allah akateremsha hukumu kwa anaye itenda na akamuwajibishia kupata adhabu kali ambayo haimtofautishi mwanamke na mwanamume, akasema Yeye aliye Mtukufu: “Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allah na siku ya mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini”. An-Nour [24]:02
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ukiwa umefuatana nasi tangu mwanzo wa jukwaa la juma hili mpaka hapa tulipo fikia, basi hutashindwa kujua na kufahamu ya kwamba ndoa ni jambo muhimu mno na tukufu kabisa katika dini. Na kwamba mwanaadamu anaihitajia ndoa kama anavyo kihitajia chakula na maji, hiyo ni kwa sababu matamanio yakizidi na yasikabiliwe na uchaMngu, yataendea kwenye kufanya uchafu na kutenda dhambi kubwa. Sasa ili kulizuia hilo, ni lazima mtu aoe/aolewe ili kupata mahala halali pa kuyaweka matamanio yake ya kimaumbile.
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]
“Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74
Ewe Mola wa haki! Ewe ambaye unaye samehe madhambi yote! Tunakuomba utusamehe madhambi yetu, uzitwahirishe nyoyo zetu, uzihifadhi tupu zetu, uzifanye njema tabia zetu, zibariki ndoa zetu na uzijaze nyoyo zetu nuru na hekima. Hakika Wewe ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. Yaa Allah tutakabalie dua!
Kwa juma hili haya ndio tuliyo wafikiwa na Allah kukumbushana kuhusiana na ndoa, tulilo patia katika hayo ni kwa taufiki yake Allah Mola Muwezeshi na tulilo kosea miongoni mwayo linatokana na mapungufu ya kibinaadamu, kwani ukamilifu ni wake Allah pekee. Tumuombe Mola wetu Mkarimu azidi kututunukia neema ya uhai, uzima na ufahamu ili juma lijalo kwa uweza wake tuendelee kuizungumzia ndoa ambayo ndio mwanzo na msingi wa familia.
Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “Na Allah amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri…”. An-Nahli [16]:72
Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.