SOMO LA PILI (Iinaendelea) – NDOA

NDOA

KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”

Sifa njema zote ni haki yake Allah; Mola wa viumbe vyote. Yeye pekee ndiye wa kuabudiwa na kuombwa. Ambaye Yeye ndiye aliye tuambia: “Na katika ishara (aya) zake amekuumbieni wake zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanao fikiri”. Rehema na Amani zishuke juu ya Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, maswahaba wake na kila aliye itika mwito wake na kufuata maagizo yake mpaka siku ya Kiyama.

Kwa ukarimu na mapenzi yake Mola, tunajumuika tena pamoja katika jukwaa letu hili, linalo tujumuisha kila juma, huku sote tukiwa na lengo moja ambalo si jingine zaidi ya kukumbushana na kuelezana yale yote yanayo ihusu familia ya Kiislamu ambayo hiyo ndio inayo tupeleka kwenye jamii bora na kisha umma bora wa Kiislamu.

Leo tunaendelea na somo letu tulilo lianza juma lililo pita, ambalo linaongozwa na anuani isomekayo:

  1. Mahimizo ya ndoa ndani ya Qur-ani na Sunna:

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tumeanza kuishi na somo hilo hapo juu katika juma lililo pita, na kwa uwezo wake Mola Yeye aliye Mtukufu tulisoma na kujifunza mahimizo ya ndoa ndani ya Qur-ani na tunataraji ya kwamba umeuona umuhimu huo chini ya kivuli cha maneno hayo matukufu. Juma hili bado tutaendelea na somo hilo hilo kwa kuuangalia upande wa Sunna (Hadithi) unasemaje kuhusiana na umuhimu wa ndoa ambayo hiyo ndio tofali la mwanzo katika ujenzi wa familia na hatimaye jamii na kisha umma wa Kiislamu.

Naam, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ambaye yeye ndiye mfasiri mkuu wa Qur-ani, anatuelezea umuhimu wa ndoa katika hadithi zake nyingi, katika darasa letu juma hili sisi tutatosheka na chache miongoni mwa hizo. Haya sasa na tufuatane pamoja kwa utuvu na umakini mkubwa ili tupate kuuona umuhimu wa ndoa kupitia kauli hizo za mume bora aliye kiigizo chema kwa kila mwana familia-Rehema na Amani zimshukie.

  • Imepokewa kutoka kwa Alqamah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilikuwa nikitembea pamoja na Abdullah bin Masoud-Allah amuwiye radhi-katika kitongoji cha Minaa, akakutana na Uthmaan-Allah amuwiye radhi-akasimama akizungumza nae, Uthmaan akamwambia (Ibn Masoud): Ewe babie Abdurahman! Ehee! Tukuozeshe binti kijana, huenda akakukumbusha yaliyo pita katika zama (za ujana) zako. Anasema (mpokezi wa hadithi; Alqamah): Abdullah akajibu: Usemayo wewe alikwisha tuambia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Enyi kongamano la vijana! Atakaye imudu ndoa, basi na aoe, kwani huko kuoa kunalifumba mno jicho (kutizama haramu) na kunaihifadhi mno tupu (kuepukana na zinaa). Na asiyekuwa na uwezo (wa kuoa), basi na ajilazimishe kufunga, kwani huko kufunga ni kinga kwake yeye”. Bukhaariy [5065], Muslim [1400], Nasaa [2046], Tirmidhiy [1081], Ibn Maajah [1845] & Ahmad [424]-Allah awarehemu.
  • Imepokewa kutoka kwa Said bin Jubeir-Allah amuwiye radhi-amesema: Niliulizwa na Ibn Abbas-Allah awawiye radhi: Je, umeshaoa? Nikamjibu: Hapana, sijaoa. Akaniambia: Basi oa, kwani watu bora wa umma huu ni wale wenye wake wengi”. Bukhaariy [5069] & Ahmad [01/231]-Allah
  • Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Amrou-Allah awawiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Dunia ni starehe na bora kabisa ya starehe za dunia ni mwanamke mwema”. Muslim [1467], Nasaai [32323], Ibn Maajah [1855] & Ahmad [02/168]-Allah awarehemu.
  • Imepokewa kwamba aliuliza Umar-Allah awawiye radhi: Ewe Mtume wa Allah! Tujipotelee mali gani? (Mtume) akamjibu: “Na ajipotelee mmoja wenu moyo wenye kushukuru, na ulimi wenye kudhukuru (kumtaja Allah kwa wingi) na mke muumini atakaye msaidia mmoja wenu katika suala la akhera”. Tirmidhiy [3094], Ibn Maajah [1856] & Ahmad [05/282]-Allah awarehemu.
  • Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Masoud-Allah awawiye radhi-amesema: Tulikuwa tunapigana vita pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na (wakati huo vitani) hatuna wake. Tukajiambia: Kwa nini hatujihasi? Akatukataza kufanya hivyo, na baada ya hapo akaturuhusu tuoe mke kwa kumpa (mahari ya) nguo, kisha akasoma: “Enyi mlio amini! Msiharamishe vizuri alivyo kuhalalishieni Allah…”. [05:87] Bukhaariy [06/139]-Allah amrehemu.
  • Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Walikuja watu watatu nyumbani kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuulizia kuhusiana na ibada yake. Na walipo ambiwa (Ibada anayo fanya), kama kwamba wakaiona ni ndogo (chache), wakasema: Tu wapi sisi na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-yeye amekwisha samehewa dhambi alizo zitenda na atakazo zitenda, mmoja wao akasema: Ama mimi, nitaswali usiku kucha maisha yote. Na mwingine akasema: Na mimi nitafunga mwaka mzima na wala sitakula. Na mwingine akasema: Na mimi najitenga na wanawake sitaoa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawafuata, akawaambia: “Nyinyi ndio mlio sema maneno kadha na kadha?! Ama wallah, hakika mimi ni mwenye kumuogopa na kumcha Allah kuliko nyinyi, lakini mimi ninaswali na ninalala, ninafunga na ninafungua na ninaoa wanawake. Basi atakaye ichukia sunna yangu (kuoa), huyo si katika mimi”.

Maelezo: Analo likusudia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kauli yake “Basi atakaye ichukia sunna yangu” – yaani atakaye upuuzia mwenendo wangu na akaenda kinyume na haya niyafanyayo mimi; kuoa na kuishi na wanawake na kupata watoto, “huyo si katika mimi” – yaani si miongoni mwa watu wanao fuata mila/dini ya maumbile, yenye wepesi katika utekelezaji wake. Imekuwa hivyo kwa sababu yeye amejiwekea uzito kwa jambo ambalo hajaamrishwa na akajitwika mashaka na taabu.

Na pia pamesemwa na Wanazuoni katika kuitolea ufafanuzi kauli hiyo ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ya kwamba muradi/mapendeleo/makusudio yake ni kwamba: Yule atakaye ukhalifu (kwenda kinyume na) muongozo na njia yake na huku akiona ya kwamba ibada anayo ifanya yeye ni bora zaidi kuliko ile inayo fanywa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Hapo sasa, kwa maono hayo, neno lake Bwana Mtume “huyo si katika mimi”, litamaanisha – huyo si katika watu wa mila (dini) yangu, kwa sababu kuitakidi hivyo kwamba unaweza kumshinda Mtume wa Allah katika ibada, jambo hilo linampeleka mtu kwenye ukafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kama tutaitafakari vema hadithi hiyo tuliyo inukuu hapo juu, basi bila ya shaka hatutashindwa kufahamu hakuna mwanaadamu anaye weza kumshinda uchaMngu Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Lakini pamoja na uchaMngu wake huo, hakujitoa katika matakwa na mahitaji ya kimaumbile kama mwanaadamu, akawa anampa Mola wake haki yake kwa kumuabudu. Na hali kadhalika anaupa mwili wake haki yake kwa kupumzika, akalala na akachanganyika na wake zake. Na akawatahadharisha Waislamu kutokuiacha Sunna hiyo au kujiweka kando nayo na akasema asiye fuata njia na mwenendo wa Waislamu, basi huyo si katika wao, sio mwenzao kwani hakuna useja katika Uislamu. Na kuwa mseja si tu ni kwenda kinyume na mwendo wa Mtume Muhammad bali ni kuwakhalifu Mitume wote wa Allah-Rehema na Amani iwashukie.

  • Imepokewa kutoka kwa Qataadah-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza useja, kisha Qataadah akaisoma (kauli yake Mola): “Na hakika sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake na dhuriya (watoto)…”

Kutokana na umuhimu wa ndoa na kwa kuwa ni tendo la kimaumbile ambalo mwanaadamu hawezi kuliepuka, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akipupia maswahaba wake wote wawe kwenye ndoa; waoe/waolewe. Na alikuwa akimuuliza mtu kama ameoa na kama hajaoa, basi humuhimiza kuoa.

  • Imepokewa kutoka kwa Abu Dharri-Allah amuwiye radhi-amesema: Aliingia kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mtu mmoja aitwaye Ukaafu bin Bishri wa kabila la Tamim, Mtume akamuuliza: Ewe Ukaafu! Una mke? Akajibu: Sina. (Mtume) akamwambia: (Huna mke) na wewe una uwezo na afya? Akasema: Na mimi nina uwezo na ni mzima. (Mtume) akamwambia: Kwa hivyo basi, wewe ni katika ndugu za shetani. Lau ungelikuwa kwa Manaswara (Wakristo) ungelikuwa mmoja wa makuhani wao. Hakika sunna yetu sisi ni ndoa. Waovu wenu ni wale walio waseja katika nyinyi na walio dhalili katika maiti wenu, ni wale walio kufa bila ya kuoa….”.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]

Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74

Ewe Mola wa haki! Kwa fadhila na rehema zako, zifungamanishe familia zetu na twaa yako na utujaalie kuwa wajenzi wa familia bora, zitakazo zalisha jamii bora, itakayo jenga umma bora. Yaa Allah tutakabalie dua!

Jukwaa letu juma hili linaishia hapa ili kutoa nafasi kwa kila mwenye siha ya akili kuyazingatia haya tuliyo elezana kuhusiana na familia ya Kiislamu na kisha kutafakari namna gani atachangia katika kupatikana kwa umma bora wa Kiislamu kupitia malezi bora ya familia yake.

Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Allah ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Allah ni Mwenye kuwaangalieni”. An-Nisaa [04]:01

Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.

One thought on “SOMO LA PILI (Iinaendelea) – NDOA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *