“KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”
Sifa njema zote ni haki yake Allah; Mola wa viumbe vyote. Yeye pekee ndiye wa kuabudiwa na kuombwa. Rehema na Amani zishuke juu ya Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, maswahaba wake na kila aliye itika mwito wake na kufuata maagizo yake mpaka siku ya Kiyama.
Ndugu mpenzi na mfuatiliaji wa jukwaa letu-Allah akurehemu. Tuna kila sababu ya kumuhimidi na kumshukuru Mola wetu Mkarimu kwa kutujaalia kukutana tena katika jukwaa letu hili, lengo mama likiwa ni kukumbushana yale ambayo ndani yake yamo manufaa na kheri yetu yenyewe.
Juma hili tena katika jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu, bado tunaendelea kuongozwa na somo lenye anuani isemayo:
- Malengo/Makusudio ya ndoa:
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma lililo pita kwa auni na msaada wake Allah tuliendelea kuangalia na kujifunza malengo makuu ya ndoa ambayo tulisema ya kwamba tukiyajumuisha pamoja yanaangukia katika mafungu makuu matatu. Na tayari juma lililo pita tumekwisha kujifunza malengo mawili ya ndoa, ambayo tulisema la kwanza ni kupata watoto na la pili ni kujikinga/kujihifadhi na haramu. Leo kwa uwezeshi wake Mola tutaliangalia lengo la tatu la ndoa ambalo ni:
- Kusaidiana katika harakati za kimaisha:
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-elewa na ufahamu ya kwamba lengo kuu la tatu la kufanywa ndoa kuwa ni jambo la kisheria katika Uislamu, ni kuwajengea watu mfumo na namna bora ya kusaidiana katika harakati za maisha ya kila siku. Kusaidiana ambako kutamfikisha mwanaadamu katika lengo la kuumbwa kwake, apate kuwa mtawala na kiongozi katika dunia hii ili aweze kumakinika katika kumuabudu Mola Muumba wake. Na kusaidiana huko kunapatikana kwa njia ya kuanzisha na kujenga familia.
Kusaidiana katika majukumu ya maisha baina ya mke na mume, kunatokana na kusukumwa na ile huruma na mapenzi yaliyo tiwa ndani yao, kwani bila huruma na mapenzi ni muhali mtu kumsaidia mwenziwe, tusome: “…Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu…”. Ar-Ruum [30]:21
Lengo hili la tatu; kusaidiana katika harakati za kimaisha, lina faida nyingi ambapo kila moja miongoni mwa hizo inamkinika kuwa na hekima/falsafa inayo jitegemea, na katika jumla ya faida hizo ni pamoja na:
- Mke kubeba sehemu ya majukumu ya maisha:
Katika ndoa, mke humsaidia mume wake katika kubeba sehemu ya majukumu ya maisha ili kumuwezesha mume kupata nafasi ya kuyashughulikia majukumu mengine. Wakati mke anashughulika na majukumu ya nyumba; kwa kuwaangalia na kuwalea watoto sanjari na kuiangalia nyumba yake kiusafi na kiusalama. Mume naye anapata nafasi ya kutoka nje kwenda kutafuta maisha ya familia yake; chakula, mavazi, gharama za matibabu, elimu na baki ya mahitaji yao muhimu. Kwa msaada wa mkewe, mume hupata fursa ya kutekeleza wajibu wake kwa familia yake, jamii yake na taifa lake. Mume huchuma kwa taabu ili kupata tonge la familia yake kutokana na maumbile ya kupambana aliyo umbwa juu yake.
Na kugawana magumu na majukumu ya maisha baina ya mume na mke, jambo hilo lina msaada mkubwa katika kuyawepesisha maisha kimaada na kimaana baina yao. Ili upate kulidiriki na kulifahamu hilo vema, hebu sawirisha akilini na fikrani mwako maisha ya baba anaye ilea familia peke yake au mama anaye ilea familia peke yake. Ione dhiki na taabu inayo mpata, halafu tena uangalie mjengo, mtungo na uimara wa familia hiyo kimaadili, kiafya, kielimu na … na …. ila wachache mno walio wafikiwa na Allah.
Na huenda mke mwema anaye msaidia mume wake katika majukumu ya maisha ya familia yao, ndiye ule wema wa kidunia unaoombwa na mja kama ulivyo nukuliwa katika neno lake Allah Mtukufu: “Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe duniani mema, na akhera mema, na utulinde na adhabu ya moto”. Al-aqarah [02]:201
Hakika maana ya kusaidiana baina ya mke na mume, inajenga na kupanda roho na mshikamano wa kijamii na kumjali mwingine kunako ambukia kwa watoto na vizazi vitakavyo kuja baada yao. Huko kusaidiana basi, ni mtazamo kina uliomo ndani ya familia na wala haupatikani kwingineko; mume humpendelea na kumtanguliza zaidi mke wake na watoto wake katika kupata kila ambalo litawaletea furaha na amani katika maisha yao. Na hujiweka mbele yeye mwenyewe katika lile lenye madhara ili asalimike mke na watoto wake, kama liko hilo la kudhuru basi na limdhuru yeye kwanza kabla ya kuwapata wao. Na hupambana mpaka pumzi yake ya mwisho kwa ajili ya maslahi na manufaa yao. Na jambo hili ni nadra mno kupatikana nje ya wigo wa maisha ya familia.
- Wanandoa kutanua wigo wa ndugu:
Katika jumla ya faida za kusaidiana kwa sababu ya ndoa, ni mume kujiongezea ndugu kwa kuunganishwa na ndugu wa mke wake na hali kadhalika mke kuongeza ndugu kwa kuunganishwa na ndugu wa mume wake. Kwani ndoa huziunganisha familia na huimarisha si tu mahusiano baina ya familia hizo bali pia mahusiano ya nchi zao pale wanapo oana watu wa mataifa tofauti. Na jambo hili ndilo linalo dokezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika hutuba yake wakati alipo muozesha binti yake Faatima kwa Sayyidna Aliy-Allah awawiye radhi-pale alipo sema: “Hakika Allah limetukuka jina lake na umekuwa juu utukufu wake. Ameufanya ukwe kuwa ni sababu yenye kuwakutanisha watu na kuwa ni jambo lenye kufaradhishwa. Na akaunganisha kwa ajili/sababu yake matumbo (koo) na akawalazimisha watu jambo hilo…”.
Katika kulisukuma mbele gurudumu la maisha, watu wanahitaji kuungana na kuimarisha baina yao mizizi ya mapenzi na ndoa ndio kitu muhimu mno kinacho yaimarisha hayo. Na jambo hilo la kutanua wigo wa familia kutokana na kuoleana baina ya koo na koo, au baina ya taifa na taifa, ni sababu ya kupatikana kwa amani baina ya koo hizo au mataifa hayo. Kwani ukoo huu, huuona ukoo ule kuwa ni ndugu zao kutokana na kuoa/kuolewa kwao na hali kadhalika taifa hili na lile, na hivyo haliwi jambo rahisi ukoo huu au taifa hili kufanyiana uadui au jambo litakalo vunja amani baina yao na ukoo au taifa lile. Na hiyo ndio ilikuwa hekima/falsafa ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kuwaoa baadhi ya wake zake, aliwaoa ili kuimarisha nguzo za amani baina yake na wakwe zake na hali kadhalika kupata fursa ya kufikisha da’awa (mahubiri ya Uislamu) miongoni mwao kwa kutumia fursa ya amani na usalama iliyopo.
Naam, ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-hizo ndizo baadhi ya taswira za kusaidiana katika maisha ya ndoa, mtu anayashughulikia ya mwenzake kama anavyo yashughulikia ya kwake mwenyewe. Na ijulikane ya kwamba yule anaye yashughulikia ya mwenzake, huwa ndiye mwenye daraja ya juu zaidi. Na jambo hilo ni jihadi ya nafsi ambayo ni sawa sawa kiujira na ile jihadi ya kupigana katika njia (Dini) ya Allah kwenye medani ya vita. Na kwa yote haya tuliyo kuandikia, tunataraji kwa msaada wake Mola utakuwa umeyaona na kuyafahamu malengo matukufu ya ndoa, ambayo hiyo ndio tofali la ujenzi wa familia ambayo nayo ndio msingi wa jamii inayo zaa taifa.
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]
“Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74
Ewe Mola wa haki! Kwa fadhila na rehema zako, zifungamanishe familia zetu na twaa yako na uzijaalie kukushikamana na mafundisho ya Qur-ani na Sunna ili ziwe familia bora zenye kupigiwa mfano. Yaa Allah tutakabalie dua!
Jukwaa letu juma hili linaishia hapa ili kutoa nafasi kwa kila mwenye moyo wa kukumbuka, akumbuke na awaidhike na kisha achukue hatua kwa kuilea na kuijenga familia ya Kiislamu kwa mujibu wa mafundisho ya Allah na maelekezo ya Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-ili tuweze kuzalisha jamii bora ya Kiislamu.
Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allah ni huyo aliye mchaMngu zaidi katika nyinyi. Hakika Allah ni Mwenye kujua, Mwenye khabari”. Al-Hujuraat [49]:13
Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.