SOMO LA NNE-POSA

“KUTENGENEA KWA FAMILIA YAKO, NDIO KUTENGENEA KWA JAMII NA TAIFA LAKO”

Sifa zote njema zimuendee Mola Mlezi wetu kwa Hidaya zake za wazi na zilizo fichikana azitoazo wakati wote. Na Baraka na Amani zimuendee Nabii wake Muhammad, Aila yake na Maswahaba wake ambao walijitolea kwa mali na nafsi zao katika kuitumikia Dini hii ya Allah na hali kadhalika ziwaendee wote walio wafuata wao mpaka siku ya Kiyama.

Kwa juma jingine na kwa mara nyingine tena, na kwa uwezo wake Allah tunakutana katika jukwaa letu, jukwaa lenye dhima moja tu nayo si nyingine zaidi ya kumkumbusha mwana jukwaa kuhusiana na Familia ya Kiislamu.

Juma hili, jukwaa lako la Familia ya Kiislamu, litaanza kujifunza pamoja nawe kuhusiana na posa katika Uislamu. 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-baada ya kufanya uchaguzi wa mwenza wako katika maisha, kinacho fuatia ni kupeleka posa. Na posa maana yake ni mwanamume kutangaza nia ya kutaka kumuoa mwanamke maalumu kupitia kwa wazazi wake huyo mwanamke.

Lakini kabla ya kijana kumposa aliye mpenda, ni lazima amjue kwanza na aone kile kitakacho mpendeza na kumvutia kwa mwanamke huyo, hata akipeleka posa awe ameridhika na uchaguzi wake. Na hili la mwanamume kumuangalia mwanamke anaye mchumbia na kwa upande wa mwanamke naye kumuona huyo anaye chumbiwa naye kabla ya kufungwa kwa ndoa, ni suala lililo kokotezwa sana na Sharia.

Imekuwa hivyo, kwa sababu ndoa ni mafungamano ya muda mrefu na pengine maisha yote, mafungamano ambayo yanatarajiwa kuleta matunda muhimu katika ujenzi wa familia, jamii na hata taifa.

Mpendwa ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-hayo tuliyo yaeleza ndio, lakini itambulike na kila mmoja wetu ya kwamba lililo asili katika hukumu ya sheria ni kuharamishwa mwanamume ajinabiya kumuangalia mwanamke ajinabiya.

Ni wajibu kufumba jicho ili kutoangalia yaliyo haramishwa kwa wote; wanamume na wanawake, uwajibu huo unatokana na kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu: “Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Allah anazo khabari za wanayo yafanya. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika…”. An-Nuur [24]:30-31

Ama kutokana na umuhimu na nafasi ya ndoa, mposaji (mwanamume) kumuangalia anaye mposa na mposwaji (mwanamke) kumuangalia mposaji wake, hilo limevuliwa kutoka kwenye uharamu huo unao tajwa na aya tuliyo inukuu hapo juu. Uangaliaji huo ni jambo lililo ruhusiwa (jaaizi) na sheria, bali limesuniwa na kupendelewa na sheria. Lakini ruhusa hiyo imewekewa masharti, kuangalia huko kuwe ni kwa:

  1. Nia ya kuposa, na
  2. Kufanyike mbele ya maharimu; isiwe baina yao peke yao.

Na hadithi zinazo lizungumzia hili la wachumba kuangaliana, ni nyingi lakini sisi katika darsa hili tutazitaja baadhi yake tu. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia mtu mmoja anaye taka kumuoa mwanamke fulani: “Je, umemuona?”. Akajibu: Hapana. (Mtume) akamwambia: “Basi, nenda ukamuangalie”. Muslim-Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Abdillah-Allah awawiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakapo taka kuposa mmoja wenu, basi akiweza kuangalia kwake (mwanamke hiyo)kitakacho mpelekea kumuoa, basi na afanye hivyo”. Ahmad, Abu Daawoud & Al-Haakim-Allah awawiye radhi.

Na anacho takiwa kuangalia mposaji kwa anaye mposa ni uso na vitanga vya mikono tu, kwa sababu uso unatosha kabisa kuwakilisha uzuri alio nao mwanamke huyo na vitanga vya mikono vinatoa taswira ya urutuba wa mwili wake. Na ilivyo uzuri na bora, ni kwamba mposaji amuangalie binti anaye mposa kabla ya kupeleka posa ili kama hakumpenda anaachana nae pasina ya kusababisha kero/maudhi au chuki baina yao.

Na pia yatakikana ifahamike katika hili la kumuangalia anaye taka kumposa, sheria haikushurutisha kupatikana kwa radhi ya binti au kujua kwamba anachunguzwa. Bali kunamuelea mposaji kumuangalia pasina yeye kujua na tena kwa kumshtukiza na hilo ndilo bora zaidi.

Hayo ndiyo mafundisho yanayo fahamishwa na Hadithi iliyo pokewa na Abu Humeid As-saaidiy-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakapo taka mmoja wenu kumposa mwanamke, basi si makosa kumuangalia itakapo kuwa anamuangalia kwa lengo la kumposa na si vinginevyo, hata kama yeye (huyo mwanamke) hajui (kuwa anaangaliwa)”. Ahmad & Twabaraaniy-Allah awarehemu.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kwa mukhtasari kabisa hiyo ndio posa ya Kiislamu ambayo tunaizingatia kama utangulizi wa ndoa. Kwa anaye taka ufafanuzi na upambanuzi wa kina katika suala hili, basi tunamshauri aziangalie rejea za Fiq-hi ili apate kujua mas-ala kama:

  • Sharti za mwanamke ambaye kumeruhusiwa kumposa,
  • Nani anaye peleka posa,
  • Posa inatangazwa au inafichwa,
  • Tamko la posa,
  • Nini hukumu ya zawadi alizo pewa binti katika kipindi cha uchumba na kisha mposaji akaghairi. Na baki ya mas-ala mengine yanayo fungamana na posa.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe: 

﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]

“Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74

Ewe Mola Mlezi wa walimwengu wote! Ewe uliye umba ardhi na ukaibarikia! Tunakuomba utubarikie vizazi vyetu, zibariki nyumba zetu, zibariki kazi zetu, yabariki matendo na kauli zetu, yabariki maisha yetu yote na utubarikie katika dini yako. Hakika hakuna mwenye kubariki ila Wewe. Yaa Allah tutakabalie duaa!

Mpaka hapa ndugu mwana jukwaa letu tunatamatia juma hili, tunaamini kwa uwezo wake Allah ya kwamba jukwaa hili linazidi kukuongezea maarifa yako kuhusiana na Familia ya Kiislamu. Maarifa ambayo yatakusaidia katika ujenzi wa familia yako ili iwe kama vile anavyo taka Mola wetu na wala sio kama vile tunavyo taka sisi.

Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakapo kujieni (kuposa) yule ambaye mnairidhia dini na tabia yake, basi muozeni na kama hamkuozesha, basi itakuwa fitina na fisadi kubwa katika nchi”. 

Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.

2 thoughts on “SOMO LA NNE-POSA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *