SOMO LA NNE –01- MATUKIO MUHIMU KABLA YA KUZALIWA KWA BWANA MTUME-Rehema na Amani zimshukie.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Naam, ndugu mwana darsa-Allah akurehemu-juma hili tena kwa fadhila zake Allah Mtukufu tumekutana katika kuendelea na mfululizo wa darsa zetu za Sira ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Tumuombe Mola Mlezi wetu atusaidie tuweze kusomeshana, kufahamu na kuzingatia huku tukitambua ya kwamba Mtume wa Allah ndiye aliye tuletea dini hii na ili kuijua vilivyo dini ni lazima kwanza tumjue aliye tuletea hiyo dini. Haya sasa karibu darasani:

Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-elewa ya kwamba wakati Allah Mola Muumba alipo taka kuishushia rehema jamii ya wanaadamu na kuitukuza, na ukafika muda wa ukombozi wao dhidi ya dhambi ya ushirikina na adui Shetani.

Na ikawa ni zama munasaba za kuletwa kwao kipenzi cha Allah na waja wake; Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Lakini kabla hatujaingia kuyaeleza mazazi matukufu ya mkombozi huyo na makuzi yake mema na namna Allah alivyo muhifadhi na kumlinda katika kile kipindi cha kabla ya kushuka kwa wahyi (ufunuo).

Tumeona ni vema kwanza, tukaanza kuzizungumzia ishara/alama na matukio makubwa yaliyo tokea kabla ya kuzaliwa kwake. Kwani mazazi matukufu ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-yalitanguliwa na matukio na mambo makubwa, yaliyo ashiria kukurubia ujio wa Mtume wa mwisho kama ulivyo tajwa na vitabu vilivyo tangulia.

Ni wazi na kweli kwamba katika jumla ya taratibu na kanuni maumbile za Allah katika ulimwengu, ni kwamba faraja huja baada ya kutanguliwa na shida/dhiki, mwangaza/nuru huzagaza baada ya kutanguliwa na giza. Hali kadhalika, wepesi huuandamia uzito. Naam, miongoni mwa yaliyo muhimu mno katika matukio na mambo makubwa hayo yaliyo yaandamia mazazi matukufu, ni pamoja na:

  1. Kisa cha babu yake Mtume; Mzee Abdul-Mutwalib kukifukua kisima cha Zamzam:

Sheikh Ibrahim Al-Aliy-Allah amrehemu-ametaja katika kitabu chake kiitwacho [Sahih As-siiratin-nabawiyyah], riwaya sahihi katika kuelezea kisha cha Mzee Abdul-Mutwalib; babu yake Bwana Mtume, kukifukua kisima cha Zamzam baada ya kufunikwa na kupotea kwa miaka mingi. Kisa hicho kimetajwa katika hadithi iliyo pokewa na Sayyidna Aliy bin Abi Twaalib-Allah amuwiye radhi-amesema: “Alisema (babu yangu Mzee) Abdul-Mutwalib: Wakati nikiwa nimelala katika Hijri (Ismailiy), tahamaki akanijia mjaji akaniambia: Fukua Twaiba. Nikamuuliza: Twaiba ni nini? Akasema (Abdul-Mutwalib): Kisha akaondoka zake.

Anaendelea (kusimulia): Siku iliyo fuata, nikaenda (tena) uchagoni kwangu (pale kwenye Hijri Ismailiy), nikalala hapo. Akanijia (tena), akasema: Ifukue Burra. Nikamuuliza: (Hiyo) Burra ni nini? Akasema (Abdul-Mutwalib): Kisha akaondoka zake.

Siku iliyo fuata, nikaenda (tena) uchagoni kwangu (pale kwenye Hijri Ismailiy), nikalala hapo. Akanijia (tena), akasema: Ifukue Madhwnuuna. Anasema: Nikamuuliza: (Hiyo) Madhwnuuna ni nini? Akasema (Abdul-Mutwalib): Kisha akaondoka zake.

Siku iliyo fuata, nikaenda (tena) uchagoni kwangu (pale kwenye Hijri Ismailiy), nikalala hapo. Akanijia (tena), akasema: Ifukue Zamzam. Anasema: Nikamuuliza: (Hiyo) Zamzam ni nini? Akasema: (Hiyo ni ambayo) hayaishi maji yake na wala hakikauki kina chake kamwe, huwanywesheleza mahujaji watukufu. Nayo ipo baina ya donyoo za kunguru wenye weupe kwenye mbawa zao, katika makutano ya wadudu chungu.

Akasema (Abdul-Mutwalib):Basi alipo liweka wazi suala lake (hiyo Zamzam) na akafahamisha ilipo na akajua kwamba amesema kweli, akatwaa jembe akiwa na mwanawe (aitwaye) Al-Haarith bin Abdul-Mutwalib na huyo ndiye aliye kuwa mwanawe pekee wakati huo (hakuwa na mtoto zaidi yake). Akachimba (mahala) hapo (alipo julishwa), Abdul-Mutwalib alipo ziona kingo za kisima, akapiga Takbira. (Kuisikia Takbira hiyo) Makuraishi wakatambua ya kwamba yeye amekwisha ipata haja yake, wakamuendea na kumwambia: Ewe Abdul-Mutwalib! Bila ya shaka hicho ni kisima cha baba yetu Ismail, na sisi tuna haki nacho, basi tushirikishe nasi kwenye (kisima) hiki. Akawaambia: Mimi sifanyi hilo, hakika hili ni jambo nililo khusishwa nalo mimi tu na si nyinyi na nimechaguliwa kupewa mimi. Wakamwambia: Hebu tufanyie haki, kwani hatutakuacha mpaka tukigombee. Akasema: Basi mtafuteni hakimu mumtakaye ahukumu baina yangu na nyinyi. Wakasema: (Na awe) kuhani wa ukoo wa Sa’ad mwana wa Hudhaim. Akasema: Naam (nimekubali) na (ukoo huo) walikuwa wakiishi karibu na mpaka wa Shamu.

Basi (baada ya makubaliano hayo), Abdul-Mutwalib akapanda (kipando chake tayari kwa safari) akiambatana na kundi la ndugu zake katika watoto wa (Ami yake) Abdu Manaaf. Na likapanda kundi katika kila kabila la Makuraishi, wakaanza safari na wakati huo ardhi (nchi) ilikuwa ni mawanda kame. (Wakaenda) hata walipo kuwa mbali njiani, yakaisha maji ya Abdul-Mutwalib na waambata wake, wakapatwa na kiu kikali mno kiasi cha kuyaona mauti hayo yanawajongelea. Wakawaomba maji wale wenzao (wa upande wa pili), wakawakatalia na wakawaambia: Hakika sisi tuko kwenye ardhi kame, nasi tunachelea tusije kufikwa na hali iliyo kupateni nyinyi. Akasema (Mzee) Abdul-Mutwalib: (Basi kama ni hivyo), mimi naona kila mmoja ajichimbie mwenyewe kaburi lake kwa kuwa sasa bado mnazo nguvu. Ili kila atakapo kufa mtu, wenzake wamtumbukize kwenye kaburi lake kisha wamfukie, mpaka abakie mtu mmoja peke yake, kwani kupotea kwa mtu mmoja ni jambo jepesi kuliko kupotea kwa msafara mzima. Wakasema: Naam, (na iwe) hivyo ulivyo amrisha wewe.

Basi kila mtu akajichimbia kaburi lake yeye mwenyewe, kisha wakakaa kusubiri kufa kwa kiu. Halafu Abdul-Mutwalib akawaambia wenzake: Wallah! Hakika kujitupa kwetu kwenye mauti kwa mikono yetu, hatuchimbi ardhi (kutafuta maji), wala hatufanyi juhudi (ya kujiokoa) kwa sababu ya ajizi. Basi huenda Allah akaturuzuku maji kwenye ardhi fulani, tuondokeni. Wakaanza kuondoka hata Abdul-Mutwalib alipo agiza kuletewa mnyama wake, ikachimbuka chini ya kwato zake (mnyama huyo) chemchem ya maji tamu. Abdul-Mutwalib akapiga takibira na akafuatiwa na watu wake, kisha akashuka akanywa na wakanywa watu wake na wakateka maji mpaka wakajaza vyombo vyao. Kisha akayaita makabila mengine ya Makuraishi nao wakiwa wanawaangalia katika mchakato ule mzima, akawaambia: Njooni mnywe maji, hakika ametunywesha Allah. Basi wakaja, wakanywa na wote wakateka maji ya akiba. Kisha wakasema: Wallah! Hakika Allah amesha hukumu baina yetu. Wallah! Hatutazozana na wewe katika kadhia ya Zamzam, kamwe. Bila ya shaka Yule ambaye aliye kunywesha maji katika mbuga kame hii, ndiye huyo huyo aliye kunywesha Zamzam. Basi rejea kwenye kinyweshelezi chako (Zamzam) ukiwa mwongofu. Basi akarejea na wakarejea pamoja naye bila ya kufika kwa yule kuhani, na wakamuacha na Zamzam yake”.

Anasema Mwanasira; Ibn Is-haaq-Allah amrehemu: Hayo ndio yaliyo nifikia kutoka kwa Aliy bin Abi Twaalib kuhusiana na Zamzam.

Na zimepokewa hadithi nyingi katika kutaja fadhila za maji ya Zamzam, miongoni mwake ni ile iliyo pokewa na Imamu Muslim-Allah amrehemu-katika kutaja kisa cha kusilimu kwa Abu Dharri-Allah amuwiye radhi. “Hakikayo ni chakula kishibishacho”.

Na imepokewa riwaya kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Maji ya Zamzam ni kwa nia yatakayo nywewa, ikiwa utayanywa kwa kutaka ponyo, Allah atakuponya. Na ikiwa utayanywa ili kupata shibe, Allah atakushibisha na kama utayanywa ili kukata kiu, Allah atakikata (kiu chako). Nayo (maji ya Zamzam) ni athari (ya pigo la) Jibrilu (pale alipo ipiga ardhi kwa kisigino au ubawa wake) na ni kinywesho cha Ismail”. Daaruqutwniy & Al-Haakim-Allah awarehemu.

Naam,hiyo ndio dhima ya somo la Sira, kwani kupitia somo hili tumeweza kuijua ijapokuwa kwa mukhtasari historia ya maji matukufu ya Zamzam na hayo ndio tuliyo wezeshwa na Allah kudarisishana juma hili. Tulilo patia ni kwa taufiki yake Allah Mola Muwezeshi na tulilo kosea linatokana na mapungufu ya kibinaadamu, kwani ukamilifu ni wake Allah pekee.

Sote kwa pamoja tumuombe Mola wetu amruzuku kila mwana darsa hili elimu, maarifa, ufahamu na busara inayo ambatana na matendo. Mpaka juma lijalo kwa uwezo wake Allah, tunaagana nawe kwa kusema: Maa Salaama!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *