SOMO LA NNE-JOSHO/KUKOGA

i) MAANA YA JOSHO:

Neno JOSHO/KUKOGA ni matokeo ya tafsiri ya neno la kiarabu GHUSLU. Neno hili lina maana mbili; ya kilugha na kisheria. Kwa mtazamo wa kilugha josho/kukoga ni kuyatiririsha maji kwenye kitu chochote kile kiwacho. Josho kisheria ni kitendo cha kuyapitisha maji mwili mzima kwa nia maalum.

ii) HUKUMU NA DALILI YA JOSHO:

Josho kisheria ni WAJIBU/FARDHI kwa kila muislamu akipatwa na mojawapo wa mambo yatakayomlazimisha kukoga kama vile janaba kwa jimai au kukoga, hedhi, nifasi, uzazi na mengineyo kama tutakvyoeleza huko mbele.

Ulazima huu akipatwa na mambo haya ni juu ya kila muislamu, mwenye akili timamu na mwenye uwezo wa kulitekeleza josho hilo.

Dalili na ushahidi wa josho ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : “NA MKIWA NA JANABA BASI OGENI” [5:6].

Na amesema tena “NA WANAKUULIZA JUU YA HEDHI; WAAMBIE HUO NI UCHAFU. BASI JITENGENI NA WANAWAKE WAKATI WA HEDHI (zao). WALA MSIWAKARIBIE MPAKA WATWAHIRIKE” [2:222].

Josho ni jambo la kisheria, liwe ni josho la nadhafa au josho la faradhi/wajibu. Na dalili za usheria wa josho zinapatikana ndani ya Qur-ani Tukufu, Sunna ya Mtume (Hadithi) na Ijmaai.

Miongoni mwa dalili za josho katika Qur-ani Tukufu : “HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA ..” [2:222].

Yaani watu wanaojiepusha na kujilinda na hadathi/uchafu wa kimaada na kimaana/najisi za dhahiri na zile za batini. Katika jumla ya dalili za josho katika suna ni ile hadithi iliyopopkelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwie radhi – amesema, amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – “Ni haki ya kila muislamu kukoga siku moja katika juma, akaosha kichwa na mwili wake” Bukhariy na Muslim.

Mapendeleo na muradi wa neno haki ni kwamba haifai kwa muislamu kuacha, na wanazuoni wameichukulia siku hiyo kuwa ni siku ya ijumaa.

Ijmaa ya wanazuoni mujitahidi imekongomana na kukubaliana kwamba kukoga kwa ajili ya nadhafa ni jambo lililosuniwa na kukoga kwa ajili ya kusihi ibada ni wajibu na hakuna hata mwanachuoni mmoja aliyelipinga kongamano hili.

iii) FALSAFA/HEKIMA YA JOSHO:

Josho katika sheria lina hekima/falsafa na faida nyingi, miongoni mwa hizo ni kama zifuatazo:

  • Kupata thawabu – Hii ni kwa sababu josho kwa maana na mtazamo wa kisheria ni IBADA kwa kuwa ndani yake kuna kutekeleza amri ya sheria na kuitumia hukumu ya sheria. Kwa hivyo lina hili la utekelezaji amri na hukumu ya sheria ujira adhimu/mkubwa.
    • Ni kwa mantiki hii ndio Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – akatuambia: “Twahara ni nusu ya imani” Muslim. Ni vema ikaeleweka wazi kuwa twahara imekusanya udhu, josho, tayammum na mengineyo.
  • Kuwa nadhifu – Muislamu anapokoga, mwili wake hutakasika na kuwa msafi. Usafi huu ni kinga kubwa ya vijidudu vinavyoweza kusababisha maradhi kama vile upele na humfanya muislamu anukie vema, kitu ambacho humkurubisha na watu kwani watu humteta mtu mchafu anukaye.
    • Imepokelewa kutoka kwa Bi Aisha – Allah amuwie radhi – kwamba amesema : Watu (maswahaba) walikuwa wakifanya kazi na hawakuwa na watumishi/vibarua wakawa na harufu mbaya ya jasho. Wakaambiwa na Mtume “Lau mngalikuwa mnakoga siku ya Ijumaa”. Na katika upokezi mwingine Mtume – Rehema na Amani zimshukie – “Lau mngalikuwa mnajitwahirisha kwa ajili ya siku yenu hii (yaani Ijumaa)”. Bukhaariy na Muslim.
  • Kuwa mchangamfu na kupata nguvu. Mwili wa mwanadamu anapokoga huwa na nguvu mpya na kurudia kuwa katika hali ya uchangamfu baada ya ulegevu na uchovu ambao humsababisha uvivu na kutokujisikia kufanya jambo lolote zaidi ya kubweteka bwete! Hili la kujisikia kuchoka na mwili kunyong’onyea hupatikana zaidi mara tu baada ya tendo la kujamiiana.
  • Kwa maneno ya jumla, falsafa ya josho twahara na nadhafa ambavyo hivi humuandaa mtu/mja na kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwasiliana na kuzungumza na Mola Muumba wake ndani ya swala akiwa katika hali njema kabisa.
iv) AINA ZA JOSHO, YAWAJIBISHAYO JOSHO NA YALIYO HARAMU KWA MWENYE KUWAJIBIKIWA NA JOSHO:

Kuna aina mbili za josho kwa mtazamo wa kisheria (kifiq-hi): Josho la faradhi/wajibu na Josho la suna

JOSHO LA FARADHI:

Hili ni lile josho ambalo haitosihi ibada yenye kuhitajia twahara kama vile swala bila ya kupatikana kwanza josho hili wakati wa kuwepo sababu zake.

SABABU ZA JOSHO LA FARADHI:

Haya ni yale mambo ambayo yakimtokea muislamu yatamsababishia awajibikiwe kukoga josho hili la faradhi. Mambo hayo ni :

  • Janaba
  • Hedhi/Nifasi
  • Kuzaa/Kujifungua
  • Mauti (kifo)

Haya ndiyo mambo ambayo humpasia muislamu josho la faradhi yatakapomtokea. Hebu sasa tujaribu kuyafafanua moja baada ya jingine.

JANABA

Maana ya asili ya neno janaba ni umbali. Hivi ndivyo ilivyotumika ndani ya Qur-ani : “….BASI YEYE AKAMUANGALIA KWA MBALI BILA WAO KUJUA” [28:11].

Kadhalika neno janaba linachukua maana ya MANII yatokayo kwa mchupo kama libebavyo maana ya JIMAI (tendo la ndoa). Kwa maana tunaposema Fulani ni mwenye janaba/ana janaba tunamaanisha si twahara/hana twahara kutokana na kutokwa na manii au kujamiiana yaani kutokana na kufanya tendo la ndoa.

MAMBO YASABABISHAYO JANABA:

Janaba husababishwa na mambo mawili yafuatayo :

  1. Mwanamume/Mwanamke kutokwa na manii kwa sababu yeyote miongoni mwa sababu zake kama vile kujiotelea usingizini yaani mtu kuota usingizini kuwa anafanya tendo la ndoa. Au yakatoka kwa kuchezeana na kushikana baina ya mwanamume na mwanamke. Au yakatoka na athari ya kutazama/kufikiri kulikouathiri moyo.

Sasa ni vema tukajua manii ni nini? Manii kwa upande wa mwanamume ni maji meupe, mazito yachupayo ambayo hutoka wakati anapofikia kilele cha matamanio. Ama upande wa mwanamke ni maji ya manjano na ni mepesi.

Katika jumla ya dalili za kuthibitisha kuwa utokaji wa manii huwajibisha josho ni hadithi zifuatazo:
Imepokelewa na Ummu Salamah – Allah amuwie radhi – amesema: Ummu Sulaym alikuja kwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie akasema : Ewe Mtume wa Allah, bila shaka Allah haoni haya kusema haki, je, inampasa mwanamke kuoga atakapojiotelea ? Mtume akajibu : “Naam, atakapoyaona maji (manii)” Bukhariy na Muslim.

Imepokelewa na Mama Aysha –Allah amuwie radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – aliulizwa kuhusiana na mwanamume anayekuta ubichibichi/umajimaji (athari ya manii) na wala hakumbuki kujiotelea. Mtume akajibu “(Atapaswa) kukoga” Na aliulizwa pia juu ya mwanamume mwenye kuona kajiotelea lakini hakukuta ubichibichi. Akasema “Haimpasi kukoga”. Ummu Sulaym akasema : Mwanamke (pia) huona hivyo (hujiotelea), je, inampasa kukoga ? (Mtume) akajibu: “Naam, wanawake ni ndugu baba mmoja, mama mmoja na wanamume” Abu Dawoud.

Muradi wa kauli ya Mtume ni kuwa wao (wanamume na wanawake) ni sawa sawa katika nyenendo na tabia za kimaumbile.

  1. Jimai – Yaani kujamiiana hata kama manii hayakutoka. Mwanamume akiingiza sehemu tu ya dhakari yake katika tupu ya mwanamke, basi imewapasa wawili hao; mwanamume na mwanamke huyo kukoga josho la kisheria bila ya kuangalia wametokwa na manii au la.

Kinachozingatiwa hapa ni muingiliano na mvaano wa tupu mbili hizo, ya mwanamume na mwanamke na si utokaji wa manii. Imepokelewa na Abu Hurayrah –Allah amuwie radhi- kutoka kwa Mtume –Rehema na Amani zimshukie – amesema: ” Mwanamume akikaa baina ya mapaja na miundi yake (mwanamke), halafu akamuendesha mbio, hakika limekwishapasa josho” Bukhariy na Muslim. Na katika upokezi wa Imaam Muslim kuna ziada: “Hata kama hakutokwa na manii”.

Na katika hadithi nyingine iliyopokelewa na Mama Aysha – Allah amuwie radhi – “Na khitani ikiigusa khitani (dhakari ikaigusa tupu ya mwanamke) hakika limepasa josho (kwa wote wawili)” Muslim.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *