SOMO LA NNE –04 MATUKIO MUHIMU KABLA YA KUZALIWA KWA BWANA MTUME-Rehema na Amani zimshukie.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

MASOMO, MAZINGATIO NA FAIDA ZIPATIKANAZO KWENYE TUKIO LA NDOVU.

7. Kisa cha watu wa ndovu ni miongoni mwa dalili za utume:

Baadhi ya Wanazuoni wa Sira na Tarekhe-Allah awarehemu-wamesema: Hakika tukio la ndovu ni miongoni mwa shuhuda na dalili julishi za utume. Miongoni mwao hao Wanazuoni ni Imamu Al-Maawardiy-Allah amrehemu-yeye amesema: Ishara za ufalme ni angavu na shuhuda za utume zi wazi, misingi yake inashuhudia yanayo fuatia. Basi humo ukweli hautatatizwa na uwongo na wala haki haitatatizwa na batili. Na kwa kadiri ya nguvu zake na kuenea kwake, ndivyo zitakavyo kuwa bishara (habari njema) zake na indhari zake (habari za maonyo).

Na yalipo karibia mazazi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-zikanukia vema ishara za utume wake na zikadhihiri alama za baraka zake.

Na ikawa katika jumla ya alama kubwa kwa uzito, na iliyo maarufu mno kuonekanwa, ni watu wa tembo…

Mpaka akafikia kusema (Al-Maawardiy): Na alama/dalili/ishara ya Mtume iliyomo ndani ya kisa cha watu wa tembo, ni kwamba katika wakati huo yeye alikuwa ni mimba ndani ya tumbo la mama yake katika mji wa Makka. Kwani yeye alizaliwa siku hamsini baada ya kutokea kwa tukio hilo na baada ya kufariki kwa baba yake.

Alizaliwa mnamo siku ya Jumatatu, mwezi kumi na mbili, Mfunguo Sita (Rabiul-Awwal). Basi alama/dalili katika tukio hilo, ni kwa njia mbili:

  1. Kwamba lau jeshi la tembo lingelishinda, basi lingetwaa mateka na kumwaga damu. Ndipo Allah akaliangamiza ili kumlinda Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-asiangukie kuwa mateka akiwa tumboni na baada ya kuzaliwa.
  2. Kwamba Makuraishi hawakuwa na ustahiki wa kukingwa na shari ya watu wa ndovu, kwani wao hawakuwa watu wa kitabu, kwa sababu walikuwamo miongoni mwao wenye kuabudu masanamu, wengine wapagani. Lakini walinusuriwa kwa sababu Allah Mtukufu alitaka udhihiri Uislamu na iwe liwazo la utume na kuiadhimisha Al-Ka’aba.

Na ilipo tangaa kwa Waarabu habari ya namna Allah alivyo liangamiza jeshi la tembo, ukawaingia utisho na haiba ya Haram na wakaitukuza, na heshima yake ikarudufika ndani ya nafsi zao na wakawa watiifu kwa Makuraishi hata wakasema (kuhusiana nao): Watu wa Allah, amewapigania na kuwatoshea na vitimbi vya adui yao.

Basi kwa ajili hiyo, wakazidi kuwaheshimu na kuwatukuza na Makuraishi wakaikabili heshima na taadhima hiyo kwa kuwapa “Rifaada”, “Sadaana” na “Siqaaya”. Ama Rifaada ni lile fungu la mali iliyo kuwa ikitolewa na Makuraishi kila mwaka kutoka kwenye mali zao, kwa ajili ya kuwapikia watu chakula katika siku za Minaa.

Kwa sababu hiyo basi, Makuraishi wakawa maimamu wa wanadini na viongozi wenye kuwaongoza Waarabu wengine. Na kisa cha watu wa tembo kikawa ni mfano na onyo kwa wale walio salimika na adhabu. [Rejea: A’ALAAMUN-NUBUWWAH cha Imamu Al-Maawardiy sah. 185-189]

Na Imamu Ibn Taimiya-Allah amrehemu-amesema: Na lilikuwa (hilo tukio la watu wa tembo) katika mwaka alimo zaliwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na majirani wa Al-Ka’aba walikuwa washirikina wanao abudu masanamu na wanao fuata dini ya Kinaswara, ni bora kuliko wao. Ikajulikanwa kupitia hilo ya kwamba muujiza huo (wa kuangamizwa kwa jeshi la ndovu) haukuwa ni kwa ajili ya kuwanusuru majirani wa nyumba kongwe wa zama hizo, bali nusura hiyo ilikuwa ama ni kwa ajili ya dhati ya nyumba hiyo (Al-Ka’aba). Au ni kwa ajili ya Bwana Mtume ambaye alizaliwa ndani ya mwaka huo kwenye nyumba hiyo au ni yote mawili kwa pamoja (nyumba na Mtume). Na lolote lile liwalo, basi hilo ni miongoni mwa dalili/alama julishi za utume wake.

Na Imamu Ibn Kathiir-Allah amrehemu-alipo kuwa akilizungumzia tukio la jeshi la tembo, alisema: Hilo (tukio) lilikuwa ni katika mlango wa maashirio ya ujio wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwani yeye alizaliwa katika mwaka huo, kwa mujibu wa kauli zilizo mashuhuri. Na ulimi wa hali ya kudura unasema: Enyi kusanyiko la Makuraishi! Allah hakukunusuruni nyinyi kwa Wahabeshi, eti kwa ajili ya ubora wenu juu yao. Lakini amekunusuruni kwa ajili ya kuilinda ile nyumba kongwe, ambayo tutaipa utukufu na heshima kwa kumleta Mtume asiye jua kusoma wala kuandika. Naye ndiye Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-Mtume wa mwisho (hakuna tena baada yake mtume atakaye letwa).

8. Tukio la watu wa tembo likawa ni mahala pa kuanzia na kutajwa tarehe:

Waarabu walilitukuza mno tukio lililo litokea jeshi la tembo, kwa ajili hiyo basi wakalifanya kuwa ni kipimo cha tarehe na kianzio cha kuhesabia tarehe, wakawa wanasema: “Hili limetokea mwaka wa tembo” na “Fulani amezaliwa mwaka wa tembo” na “Hili lilitokea baada ya mwaka wa tembo kwa miaka kadhaa”. Na mwaka wa tembo ulisadifu kuwa sawa na mwaka 570 Miladia.

Ndugu mwana darsa-Allah akurehemu-mpaka hapa darsa letu hili limetamatia, kwa uwezo wake Allah tunatumai utakuwa umejifunza na kuielewa japo sehemu ndogo ya faida na mazingatio yanayo patikana kupitia kisa cha watu ndovu ambacho hicho kilitokea kabla ya kuzaliwa kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Haya na tumuombe Allah atupe uhai na uzima ili tupate kuungana nawe tena katika darsa zinazo fuatia. Hadi juma lijalo tunasema: Maa Salaamah!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *