SOMO LA NNE –03 MATUKIO MUHIMU KABLA YA KUZALIWA KWA BWANA MTUME-Rehema na Amani zimshukie.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

MASOMO, MAZINGATIO NA FAIDA ZIPATIKANAZO KWENYE TUKIO LA NDOVU.

Ni jambo jema, tena la wajibu, tuanze kwa kumshukuru Mola wetu Muweza wa kila kitu ambaye kwa uwezo na matashi yake, ametujaalia uhai na uzima hata tukaweza kukutana kwa mara nyingine tena katika darsa letu hili la Sira.

Mola wetu Mtukufu tunakuomba utuzawadie ufahamu utokao kwako ili tuzidi kusomeshana, masomo ambayo yatakuwa ni kani ya kutusukuma kumpenda Bwana Mtume na kisha tumfuate ili tupate kukutana naye peponi, nawe ukiwa radhi nasi.

Katika darsa letu la juma hili, tutajifunza pamoja masomo, mazingatio na faida zilizo sheheni ndani ya tukio la watu wa ndovu kama tulivyo kwisha lisoma. Kwa auni na taufiki yake Mola, tunasema miongoni mwa masomo hayo ni pamoja na:

1. Kubainisha utukufu wa Al-Ka’aba; nyumba ya mwanzo waliyo wekewa watu kwa ajili ya ibada:

Ndugu msomaji-Allah akurehemu-kisa cha watu wa tembo kimesheheni mafundisho na faida nyingi kwetu sisi Waislamu na wala si kisa cha kusomwa tu kama hadithi ya paukwa pakawa.

La hasha, bali ni kisa kinacho paswa kusomwa kwa mazingatio makubwa na kila mmoja wetu, ili afaidike na faida na masomo yaliyomo humo.

Naam, kisa hiki kinatuwekea wazi na kutujulisha utukufu wa Al-Ka’aba ambayo ilikuwa ikitukuzwa, kuenziwa na kuheshimiwa tangu zamani hata na wale washirikina wa Kiarabu.

Na daraja, hadhi na utukufu huo ulio pewa Al-Ka’aba, ulitokana na masalia ya dini ya Mtume Ibrahimu na mwanawe Ismaili-Amani iwashukie-yaliyo kuwemo mioyoni na fikrani mwa watu wa zama zile.

Na jengine linalo onyesha hadhi na utukufu wa nyumba hiyo kongwe ya ibada, ni kule mwenyewe Allah Mtukufu kutawalia ulinzi wake dhidi ya uadui wa Abraha, akawaangamiza wote walio ikusudia kwa ubaya.

Na hilo si kwa zama hizo tu, bali hata leo yeyote atakaye ivunjia heshima nyumba hiyo au kuifanyia uadui kwa namna yoyote ile, atapambana na mwenye nyumba yake.

2. Hasadi, chuki, uadui, na nia mbaya ya Manaswara kwa mji wa Makka na Waarabu:

Chuki, hasadi, roho ya kwanini na uadui wa Abraha kwa Waarabu walio kuwa wakiiadhimisha na kuitukuza Al-Ka’aba ndio iliyo msukuma kujenga kanisa la Qulaisi ili kuwafanya Waarabu waache kuitukuza Al-Ka’aba na badala yake wauhamishie utukufu na taadhima hiyo kwenye kanisa lake.

Pamoja na kutumia kwake njia za kuvutia sanjari na zile za vitisho, lakini bado haikusaidia, Waarabu walikataa na ili kumuonyesha kuwa hawataki, mmoja wa mabedui akaenda kukidhi haja ndani ya kanisa hilo.

Alifanya hivyo ili kumjulisha kivitendo ya kwamba kanisa lake hilo si chochote wala lolote mbele ya Al-Ka’aba; nyumba kongwe ya ibada.

Imamu Fakhru Raazi-Allah amrehemu-katika kuitafsiri kauli yake Allah: Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika?”. Amesema: “Jua ya kwamba (neno) vitimbi (maana yake ni) kukusudia madhara (yamfike) mtu mwingine kwa njia ya uficho. (Iwapo mtu atauliza) kwa nini (Allah) ameliita tukio hilo kitimbi (na maana ya kitimbi ndio hiyo tuliyo ambiwa) na suala (la Abraha) lilikuwa wazi, kwani yeye alisema wazi ya kwamba anakwenda kuivunja Al-Ka’aba? (Tunasema kumjibu): Naam (ni kweli hayo uyasemayo), lakini yale yaliyo kuwamo moyoni mwake yalikuwa mabaya mno kuliko hilo (la kuivunja Al-Ka’aba) alilo litaja wazi. Kwani yeye aliwadhamiria hasadi Waarabu na alikuwa anataka kuiondosha hadhi na heshima waliyo ipata kwa sababu ya uwepo wa Al-Ka’aba kwao. Alitaka kuwapokonya hilo kutoka kwenye nchi yao, aihamishie kwenye nchi yake”. [Rejea TAFSIIR RAAZIY]

3. Kujitoa muhanga katika kuyahami na kuyalinda matukufu ya Allah:

Katika kisa cha tembo tumeona mmojawapo wa wafalme wa kabila la Himyari alisimama kukabiliana na jeshi la Abraha, lakini akazidiwa nguvu na kuangukia mateka mikononi mwa Abraha.

Leo tarekhe (Historia) inamtaja kutokana na kitendo chake hicho cha kujitoa muhanga katika kuyahami matukufu yake Mola. Mwingine miongoni mwa wengi walio jitoa muhanga alikuwa ni Nufail bin Habiib wa ukoo wa Khath’am, huyu alitoka kupambana na Abraha akiwa na kundi la Waarabu wa makabila ya Yemen.

Wakapambana na Abraha ili kumzuia asiende kuivunja Al-Ka’aba, lakini kutokana na ukubwa wa jeshi la Abraha hawakufua dafu, wakasambaratishwa. Pamoja na kushindwa huko lakini tayari waliisajiri Historia kwa damu zao kwa ajili tu ya kuyatetea na kuyahami matukufu yao.

Naam, ikiwa wale walikuwa ni washirikina wenye masalia ya imani ya dini ya Nabii Ibrahimu-Amani imshukie-pamoja na udhaifu wao lakini walisimama kidete kuihami Al-Ka’aba.

Ni hali gani leo, kwa muislamu mkamilifu wa imani?! Si ndiye aula zaidi wa kuyahami, kuyatetea na kuyalinda matukufu ya Allah dhidi ya uchokozi na uadui wa maadui wa Allah na dini yake?! Leo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anachorwa katuni, anatengenezewa filamu za kumfedhehesha, anatukanwa, muislamu moyo haukupigi, ghera ya imani haikupandi, unashindwa hata kusema, basi hata kuchukia?! Msahafu unachanwa, unatemewa mate, unachomwa moto, unakojolewa, unakanyagwa kanyagwa na viatu, wewe unasema tutafanyaje sasa sisi wanyonge, kweli?!

4. Wasaliti wa umma watupwe mkono:

Wale watu wa Thaqiifu walio kuwa wakiongozwa na Masoud bin Mu’attab, ambao walimsaidia Abraha katika kuitekeleza dhamira yake mbaya, na wao wakawa ndio wapelelezi na majasusi wake. Si hivyo tu, bali wakamuongoza na kumjulisha njia ya kumfikisha ilipo ile nyumba kongwe ya Allah ili apate kuibomoa.

Hao wamelaaniwa duniani na akhera pia; wamelaaniwa na watu duniani na wamelaaniwa na Muumba wa watu juu mbinguni. Na kaburi la mjulisha njia; Abu Rughaal likawa ni alama na kielelezo cha khiyana na usaliti. Mtu huyo akawa ni mwenye kuchukiwa mioyoni mwa watu, na kila mtu alipo pita lilipo kaburi lake, alilipopoa kwa mawe.

Naam, khiyana na usaliti wa umma haukuanzia hapo kwa Thaqiifu, bali hilo ni jambo la tangu na tangu. Hali kadhalika khiyana na usaliti haukukomea kwa Bani Thaqiifu, bali hilo ni jambo linalo endelea kuishi hadi hii leo miongoni mwetu.

Tunao tele wasaliti misikitini mwetu, kwenye taasisi zetu na hata mitaani mwetu, mambo mengi ya umma leo yanakwama kwa sababu yao wao. Hao ni virusi hatari ndani ya jamii yetu, si watu wa kuungwa mkono kwa maana ya neno lenyewe, bali ni watu wa kupopolewa kwa mawe.

5. Kweli hakika ya vita baina ya Allah na adui zake:

Neno la kiongozi wa Makka; Mzee Abdul-Mutwalib: “Tutamuacha yeye na nyumba hiyo. Ikiwa Allah atamuacha yeye na nyumba hiyo (akaibomoe), sisi hatuna ubavu na hilo”. Ndani yake mna uthibitisho sahihi unao fahamisha kweli hakika ya vita baina ya Allah na adui zake, vyovyote itakavyo kuwa nguvu ya adui na ukubwa wa jeshi lake.

Basi ni ukweli usio pingika kwamba, nguvu kubwa hiyo na jeshi kubwa hilo, haliwezi kusimama hata kwa sekunde moja tu mbele ya nguvu, uwezo na adhabu yake Allah. Kwani Yeye Allah-utakasifu wa mawi ni wake-ndiye Mtunuku wa uhai huo unao mtia jeuri mwanaadamu hata akathubutu kupambana na Muumba wake na ndiye anaye weza kumpoka uhai wake wakati wowote autakao, mahala popote apatakapo na kwa namna yoyote aitakayo.

Amesema Al-Qaasimiy-Allah amrehemu: Amesema Al-Qaashaaniy-Allah amrehemu: “Kisa cha watu wa ndovu ni kisa mashuhuri (kumetangaa kujulikana kwake) na kilitokea karibu ya kuzaliwa kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Nacho ni mojawapo ya vielelezo (vinavyo onyesha na kujulisha) uwezo wa Allah na athari ya ghadhabu zake kwa yule anaye thubutu kuvunja nyumba yake tukufu (na baki ya matukufu yake mengine)”. [Rejea MAHAASIN TAFSIIR ya Al-Qaasimy 17/262]

6. Kuenziwa na kutukuzwa Al-Ka’aba na watu wake:

Tukio la watu wa ndovu, lilizidisha mara dufu heshima ya Waarabu katika kuitukuza na kuienzi nyumba ya Allah ambayo Yeye Mwenyewe amechukua dhamana ya kuihami na kuilinda dhidi ya vurugu na vitimbi vya mafisadi.

Kama ambavyo tukio hilo, liliipandisha heshima ya Makuraishi miongoni mwa Waarabu wengine kiasi cha wao kufikia kusema: Wao (Makuraishi) ni watu wa Allah, Allah amewapigania na kuwatoshea (shari ya) adui. Na tukio hilo likawa ishara/alama miongoni mwa alama za uwepo wa Allah na pia likawa ni utangulizi wa kutumwa kwa Mtume atakaye letwa kutokea Makka.

Naye ndiye atakaye itakasa Al-Ka’aba kwa kuiondoshea masanamu yaliyo wekwa humo yakiabudiwa, na pia atairejeshea heshima, daraja na hadhi yake.

Ndugu mwana darsa-Allah aukunjue ufahamu wako-kwa juma hili darsa letu linatamatia hapa, huku tukiamini kwa uwezo wake Allah, kwamba  masomo ya darsa letu hili, yatakuwa yanakuongezea maarifa, ufahamu na ujuzi wa Sira yake Mtume wetu.

Na yote hayo yatakuwa yanakusaidia kumuiga na kumfuata ili akufikishe salama kwa Mola Muumba wetu aliye mtuma kwetu kutuletea dini. Mpaka juma lijalo tunasema: Maa Salaama!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *