Tumuhimidi na tumtakase Allah Mola Muumba wa mbingu saba na ardhi saba na vyote vilivyomo humo. Tunamshukuru kwa kuturuzuku bure uhai na uzima hata tukaweza kukutana leo katika ukumbi wetu huu wa Familia ya Kiislamu. Tunazidi kumuomba atufikishie Sala na Salamu kwa kipenzi chetu Mtume Muhammad; aliye Mbora wa familia, ziende na ziwafikie pia Aali, Sahaba na umati wake jamia.
Ndugu msomaji na mshirika wetu katika jukwaa hili la Familia ya Kiislamu-Allah akurehemu. Baada ya Utangulizi wa makala hizi ulio kujia katika majuma mawili yaliyo pita, kwa msaada na uwezeshi wake Mola tumekutana tena katika ukumbi wetu huu wa kila juma. Leo ndio tunalianza somo letu la kwanza katika mfufulizo wa jukwaa hili la Familia, hebu na tuanze kwa kujiuliza sote:
- Familia ni nini.
Kwa kuwa Darasa na Makala zetu hizi zinabebwa na kuongozwa na anuani isemayo: “Familia ya Kiislamu; muundo, mjengo na mpango wake kwa jicho la Uislamu”. Sasa basi, ili tuweze kwenda na kufuatana pamoja, ni lazima kwanza tukaelewa Familia ni nini/Maana ya familia, ili kila tutakapo kuwa tunaitaja familia, akili, mawazo na fikra zetu zirejee kwenye maana hiyo.
Naam, Uislamu kama dini na mfumo kamili wa maisha ya mwanaadamu, unacho Kitabu chake ambacho hicho ndicho muongozo na dira ya Waislamu wote, pia unaye Mtume wake ambaye yeye huyo ndiye kiongozi wa umma mzima. Hali kadhaalika, Uislamu unayo lugha yake, ambayo hiyo ndio lugha inayo waunganisha Waislamu wote popote pale walipo pasina kujali tofauti ya rangi, utaifa na hali zao za kijamii. Ni lugha yao leo duniani, kaburini na kesho kule Akhera. Kwa kuwa tunakusudia kuizungumzia Familia ya Kiislamu, basi ni lugha hiyo ndiyo itakayo tuongoza kujua maana ya familia.
Katika lugha ya Waislamu; Kiarabu, neno “Familia” linabeba dhana ya jamaa na ndugu wa karibu wa mtu. Ndugu hao wanaunganishwa kupitia:
- Nasaba (uzawa), yaani ndugu wa kuzaliwa kwa upande wa baba, babu na kuendelea na kwa upande ule wa mama, bibi na kuendelea. Kwa upande wa nasaba ya baba, mtu anampata kaka/dada alio zaliwa nao kwa baba huyo na watoto wao, baba mkubwa/mdogo, shangazi walio zaliwa na babu yake (baba wa baba yake) na watoto wao. Pia anampata bibi aliye mzaa baba yake na ndugu zake bibi na babu aliye mzaa baba yake na ndugu zake na watoto wao. Hao ni ndugu na jamaa zake kwa upande wa baba yake.
Ama ndugu na jamaa zake kwa upande wa mama, ni pamoja na kaka/dada alio zaliwa nao kwa mama huyo na watoto wao, mama mkubwa/mdogo, wajomba walio zaliwa na bibi yake (mama wa mama yake) na watoto wao. Pia anampata bibi aliye mzaa mama yake na ndugu zake bibi na babu aliye mzaa mama yake na ndugu zake na watoto wao. Hao ni ndugu na jamaa zake kwa upande wa mama yake.
- Kunyonya, yaani ndugu walio nyonyeshwa na mama mmoja. Mtoto akinyonyeshwa na asiye mama yake mzazi, basi tayari wamesha kuwa ndugu kwa sababu ya kunyonya. Kwa hivyo basi, mama mnyonyeshaji anakuwa ni mama wa mtoto aliye mnyonyesha, mtoto wa mama huyo walio nyonyeshwa pamoja anakuwa ni ndugu yake wa kunyonya na mume wa mama huyo anakuwa ni baba yake.
- Ukwe, mtu kuoa/kuolewa katika familia fulani, tayari anakuwa ameshaunga udugu na familia ile kupitia ndoa. Katika huko kuoa, mume anakuwa amempata mke ambaye anakuwa ni ndugu yake wanaye rithiana. Pia anampata baba mkwe, mama mkwe na mtoto wa mke kama alipata kuzaa kabla ya kumuoa. Hali kadhalika katika kuolewa, mke anakuwa amempata mume wanaye rithiana, kama anavyo mpata baba mkwe, mama mkwe na mtoto wa mume kama alipata kuzaa kabla hajaolewa nae.
Tanbihi:
Udugu wote huo unao ingia chini ya dhana ya familia; ule wa nasaba, kunyonya na ukwe, kila mmoja una hukumu zake katika Sheria. Wako katika ndugu hao ambao ni haramu kuoana na wale walio halali kuoana, kama ambavyo wako miongoni mwao wanao rithiana na wale wasio rithiana. Lakini hapa si mahala pa kuzitaja hukumu hizo, hapa tunajaribu kuonyesha ndugu katika Familia ya Kiislamu. Ukipendezwa kuzijua hukumu hizo, angalia Rejea za Fiq-hi.
Naam, hiyo ndio familia katika jicho la Uislamu. Na dini nyingine, jamii zisizo za Kiislamu na mifumo mingine inayo tokana na fikra za kibinadaamu nayo ina mitazamo na dhana zao katika kuielezea familia. Lakini sisi katika masomo yetu haya, twende na maana hiyo ya familia kwa mujibu wa jicho la Uislamu. Haya sasa na tuangalie:
- Asili/chimbuko la familia:
Familia ya Kiislamu na ile isiyo ya Kiislamu, asili/chimbuko lake ni moja na asili hiyo inatajwa na kuelezwa na Mwenyewe Mola Muumba ulimwengu na walimwengu ndani ya Kitabu chake Kitukufu, tusome na tufahamu: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Allah ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Allah ni Mwenye kuwaangalieni“. An-nisaa [04]:01
Tukiitafakari vema aya hii tuliyo inukuu, tutafahamu ya kwamba Allah Mola Muumba wetu ndiye aliye uanzisha utaratibu huu wa familia kupitia kwa wale wanaadamu wa kwanza; Baba yetu Adam na Mama yetu Hawaa-Amani iwashukie. Baada ya kumuumba Nabii Adam-Amani imshukie-akamuumbia mke wake; Mama yetu Hawaa na kutokana na wawili hao akaumba wanaume na wanawake wengi. Hiyo ndio asili na chimbuko la familia na familia zetu zote zinafuata utaratibu huo ulio asisiwa na wazazi wetu hao wa awali. Kila familia leo; yangu, yako na ya yule imetokana na mwanamume mmoja na mwanamke mmoja walio funga ndoa, wakawa mke na mume na kisha wakawa baba na mama, halafu wakawa baba na mama mkwe na halafu tena wakawa babu na bibi.
Kwa mujibu wa aya, jamii yote ya wanaadamu ulimwenguni kote ni familia moja; familia ya Nabii Adam na Mama Hawaa. Familia yake ilipo ongezeka na kuwa kubwa, hapo sasa ndipo yakatokea matumbo (koo), makabila na hata mataifa na hilo ndilo analo lizungumzia Allah Mola Mtukufu kupitia kauli yake: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari“. Hujuraat [49]:13
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
﴿… رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا٧٤ [الفرقان: 74]
“Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachaMngu”. Al-Furqaan [25]:74
Ewe Mola Mlezi wetu! Kwa ulezi wako kwetu sisi, tunakuomba utuweke katika kundi la vipenzi wako na waja wako wa karibu yako ambao nuru yao iko mbele yao na kuliani mwao na wala hawatakuwa na khofu siku ya Kiyama na wala hawatahuzunika. Ewe Mola wetu Mlezi! Tuondolee mmomonyoko wa maadili katika familia na umma mzima wa kipenzi chako, Mtume wetu Muhammad. Yaa Rabbi tutakabalie dua!
Hapa ndipo linapo tamatia Jukwaa letu juma hili, tunamuomba Allah Mola Muumba wetu amnufaishe na jukwaa hili kila anaye lizengea na kulifuatilia kila juma. Atupe afya na nguvu waandaaji wa jukwaa ili tuweze kuendelea kukuletea jukwaa hili kila juma minajili ya kutuelimisha sote kuhusiana na Familia ya Kiislamu ili tuziasisi na kuzilea familia zetu kwa mujibu wa atakavyo Mola Muumba wetu. Na ni kwa njia hiyo tu ndio familia zetu, jamii zetu na hata ulimwengu wetu utasalimika na janga hili la dude liitwalo “Mmomonyoko wa maadili”.
Wakati tukiendelea kumuomba Allah atukutanishe tena juma lijalo tukiwa na afya ya mwili, roho na akili, si vibaya tukiizingatia na tukiitafakari kauli yake Allah Yeye aliye Mtukufu na Muumba wetu: “Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza”. Al-Furqaan [25]:54
Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa jukwaa letu hili la Familia ya Kiislamu.