i/ MAANA YA TWAHARA KATIKA LUGHA YA SHERIA
“Twahara” ni neno la Kiarabu lenye maana mbili; maana ya kilugha na maana ya kisheria. Twahara katika lugha ina maana ya unadhifu na kujilinda na kila kilicho kichafu.
Kwa mtazamo wa sheria twahara ni kuondosha 1. Hadathi na 2. Kuondosha najisi.
- Hadathi ni hali inayomzuilia mtu kufanya ibada kama vile swala na hali hii huondoka kwa kutawadha ikiwa hadathi ni ndogo, na kwa kuoga ikiwa hadathi ni kubwa.
- Najisi ni kama vile damu, usaha, matapishi, choo kikubwa na kidogo, mbwa, nguruwe na kadhalika.
ii/ UBORA WA TWAHARA
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasifia sana waja wake wanapenda kujitwaharisha na kujitakasa ndani ya Qur-ani aliposema: “HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA”. (2:222)
Utaona kutokana na aya hii kwamba twahara ni sababu ya kuyavuna mapenzi ya mola Mwenyezi. Mwenyezi Mungu anazidi kutuonyesha ubora wa twahara kwa kusema:
“MSIKITI ULIOJENGWA JUU YA MSINGI WA KUMCHA ALLAH TANGU SIKU YA KWANZA (ya kufika Mtume Madinah) UNASTAHIKI ZAIDI WEWE USIMAME HUMO. HUMO WAMO WATU WANAOPENDA KUJITAKASA NA ALLAH ANAWAPENDA WAJITAKASAO”. (9:108)
iii/ FALSAFA YA TWAHARA NA MAKUSUDIO YAKE
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameifanya twahara kuwa ni sheria na kuwafaradhishia waja wake kwa sababu twahara humfanya muislamu aishi maisha ya unadhifu na utakasifu. Humfanya awe mtakasifu wa mwili, nadhifu wa mavazi na mahala aishipo. Utakasifu na unadhifu huu humjengea afya njema na mwenendo mzuri kitabia. Usafi huu wa nje/dhahiri ni barabara na chombo cha kumfikisha katika usafi na utakasifu wa ndani/batini ambao humfanya kuwa ni mtakasifu wa moyo, mwenye kauli nzuri laini na nafsi iliyosalimika na husuda, udanganyifu na tabia mbaya zote kwa ujumla. Muislamu wa kweli ni yule aliyetakasika nje na ndani wakati wote khasa khasa wakati wa kutekeleza ibada, hii ndio sababu Bwana Mtume akatuambia: “Uislamu ni nadhifu, basi jinadhifisheni kwani hatoingia peponi ila aliye nadhifu”.
iv/VYA KUJITWAHARISHIA (VITWAHARISHIO)
Vitu vitumikavyo katika twahara ni hivi vinne vifuatavyo:-
i/ Maji
ii/ Mchanga
iii/ Dab-ghu na
iv/ Mawe.
i/ MAJI: Maji yakiwa miongoni mwa vitu vinne hivi ndiyo yatumikayo sana katika suala zima la twahara.
Maji yanayofaa kutumika katika twahara kwa mtazamo wa fiq-hi hujulikana kama MAJI MUTLAQ ambayo haya yana sifa ya kuwa yenyewe ni twahara na yanaweza kutwaharisha kitu kingine.
Maji haya ni :-
1:MAJI YA MVUA – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni. Mwenyezi Mungu anatuambia juu ya maji haya:.
“NA TUNAYATEREMSHA KUTOKA MAWINGUNI MAJI SAFI (kabisa) (25:48)
Na akasema tena:
“NA AKAKUTEREMSHIENI MAJI KUTOKA MAWINGUNI ILI KUKUTWAHIRISHENI KWAYO…”(8:11)
2: MAJI YA THELUJI – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni yakiwa katika hali ya kumiminika kisha yakaganda.
3: MAJI YA UMANDI – haya ni yale yateremkayo kutoka mawinguni yakiwa katika hali ya kuganda kisha yakayeyuka yanapofika ardhini. Mtume anatuambia katika kuonyesha utwahara wa aina hizi za maji:
“Ewe Mola wa haki nikoshe kutokana na makosa yangu kwa theluji, maji na (maji ya) umandi”
4:MAJI YA BAHARI – Yaani maji chumvi
5:MAJI YA MAZIWA NA MITO – Yaani maji tamu yasiyo ya chumvi.
Imepokelewa na Abu- Hurayrah- Allah amridhie- amesema: Mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu – Allah amrehemu na kumshushia amani – akasema:Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu sisi tunasafiri, na tunachukua maji kidogo tu, tukiyatumia kutawadhia tutashikwa na kiu, je, tutawadhe kwa maji ya bahari? Mtume akamjibu:”Hiyo (bahari) ni twahara maji yake, halali mfu wake” Bukhaariy na Muslim.
6:MAJI YA CHEMCHEM:Haya ni yale yachimbukayo yenyewe kutoka ndani ya ardhi bila ya kutumia zana kuyatoa.
7:MAJI YAVISIMA: Hayo ni yale yachimbuliwayo kutoka ardhini.
Aina zote hizi za maji tulizozitaja na ambazo zinazofanana na hizi inafaa kuyatumia katika twahara yakiwa peke yake au yakichanganywa pamoja baina aina moja na nyingine.
ii/ MCHANGA: Mchanga hutumika katika twahara badala ya maji ikiwa mtu amekosa maji au maji yapo lakini hawezi kuyatumia kwa sababu ya maradhi ambayo akitumia maji yatazidi au yatachelewa kupona.Twahara hii ya kutumia mchanga badala ya maji ndio hujulikana katika sheria kama TAYAMMAMU. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:- “NA KAMA MKIWA WAGONJWA (mmekatazwa kutumia maji) AU MMO SAFARINI AU MMOJA WENU AMETOKA MSALANI (chooni) AU MMEWAGUSA WANAWAKE NA MSIPATE MAJI BASI UKUSUDIENI (tayamamuni) UDONGO SAFI, MPAKE NYUSO ZENU NA MIKONO YENU…” (4:43)
iii/ DAB-GHU: Dab-ghu ni njia/utaratibu utumikao katika kuitwaharisha ngozi ya mnyama ili iweze kufaa kutumika katika matumizi mbalimbali ya binadamu. Hutumika vitu vikali kabisa vyenye muonjo wa tindikali kuondoa taka zilizo juu ya ngozi kama vile damu, mafuta na vipande vya nyama vilivyosalia wakati wa kuchuna. Baada ya hatua zote hizi ndipo ngozi hutiwa maji ikawa ni twahara inayoweza kutumiwa.
iv/ MAWE: Mawe au chochote chenye kufanana na mawe kama vile karatasi (toilet paper), na vinginevyo vinavyoweza kuondosha najisi hutumika katika kuchamba (kustanji) wakati yanapokosekana maji.
Aina hizi za vitu vitumikavyo katika twahara zinaonyesha wepesi wa dini hii ya kiislamu katika kuweka sheria na hukumu zake ambazo zinakwenda sambamba na tabia na mazingira ya mwanadamu. Haya yanathibitishwa na ruhusa tuliyopewa na sheria ya kujitwaharisha kwa kutumia aina zote za maji tulizozitaja na tukiyakosa maji au yakiwa yanatudhuru tumeruhusiwa kutumia mchanga.