SOMO LA KWANZA – ASILI NA CHIMBUKO LA WAARABU NA USTAARABU (MAENDELEO) WAO.

  1. Asili ya Waarabu.

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-fahamu na uelewe ya kwamba, Sira ya Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-haiandikiki na wala haielezeki bila ya kuwataja na kuwajua Waarabu na chimbuko (nasaba) lao, kwani yeye Bwana Mtume anatokana na kizazi chao. Kwa maana ya kwamba Mtume wa Allah ni mwanaadamu na ni Muarabu kiuzawa.

Naam, Wanahistoria wameigawa asili ya Waarabu katika vigawanyo/makundi matatu kwa kuzingatia machimbuko (nasaba) yao kama ifuatavyo:

  1. Waarabu “Baaida” – walio toweka kwenye uso wa ardhi:

Hawa ni wale Waarabu wa kale kabisa ambao wanajumuisha makabila ya Aadi, Thamuud, Amaaliqa, Twasmu, Jadiish, Umaimu, Jurhum, Hadharamout na wanao tungamana nao. Na walikuwa na falme zao zilizo anzia Shamu mpaka Misri. Na Waarabu wote hao na makabila yao walitoweka kabla ya Uislamu; kabla ya ujio wa Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie.

  1. Waarabu “Aariba” – wa asili.

Waarabu hawa wanatokana na kizazi cha Ya’arubu bin Yashjubu bin Qahtwaan na pia wanaitwa kwa jina la العرب القحطانية Al-‘Arabu Al-Qahtwaaniyya”. Na wanatambulika kwa jina jumla la “Waarabu wa Kusini” na falme/tawala za Yemen; Ma’iin, Sabai na Himyari zinatokana nao, ni katika kizazi chao.

  1. Waarabu “Adnaaniya” – watokanao na kizazi cha Adnaani.

Hawa wananasibika na Adnaani ambaye yeye nasaba yake inagota (inakomea) kwa Nabii Ismail mwana wa Nabii Ibraahimu-Amani iwashukie. Nao ndio wanao julikana kwa jina la العرب المستعربةAl-‘Arabu Al-Musta’araba” – yaani wale ambao ilichanganyika nao damu isiyo ya Waarabu na Kiarabu kikawa ndio lugha ya mchanganyiko huo mpya wa damu. Nao wanatambuliwa kwa jina jumla la “Waarabu wa Kaskazini”, na makaazi yao ya asili ni Makka. Nao ni mchanganyiko wa uzao wa Nabii Ismail na wanawe pamoja na Wajaraahimu; masalia ya kabila la Jurhum ambao Nabii Ismail alijifunza kwao lugha ya Kiarabu na akaoa kwao. Na watoto wake Nabii Ismail wakaishi na kukua wakiwa Waarabu kama wao hao Waarabu Wajaraahimu.

Na walio mashuhuri mno katika kizazi cha Nabii Ismail ni Adnaan; babu mkuu (progenitor) wa Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Na katika kizazi cha Adnaan ndio yakapatikana makabila ya Waarabu na koo zao, kwani Adnaan alifuatiwa na mwanawe Mu’ad, kisha Nizaar ambaye walikuja baada yake wanawe wawili; Mudhwar na Rabii’ah.

Ama huyu Rabii’ah mwana wa Nizaar, kizazi chake kilitawanyikia upande wa Mashariki, ukoo wa Abdul-Qaisi ukafanya maskani yake Bahrein na ule wa Haniifa maskani yao yakawa Yamaama. Na ukoo ule wa Bakri bin Waail ukafanya maskani kwenye eneo lililo baina ya Bahrein na Yamaama. Na ukoo wa Taghlabu ukavuka mto Furaat na kwenda kuishi kwenye kisiwa kilicho baina ya bonde na mto Furaat. Ama ukoo wa Tamimu wao walifanya maskani yao katika vitongoji vya mji wa Basra katika nchi ile ijulikanayo leo kwa jina la Iraq.

Ama tukija kwa kizazi cha Mudhwar, ukoo wa Suleim uliweka maskani yao karibu na mji wa Madina na ule ukoo wa Thaqiifu ukaishi Twaifu. Na koo nyingine za Hawaazin zikafanya maskani yao upande wa Kaskazini Mashariki mwa mji wa Makka. Na ukoo wa Asad ukawa na maskani Kaskazini Mashariki mwa mji wa Taimaa kuelekea Kusini Magharibi mwa mji wa Kuufa.

Na kizazi cha Mudhwar ndicho ambacho Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-amezawa kutokana nacho. Imepokewa kutoka kwa Kulaib bin Waail amesema: Alinihadithia binti mlelewa (mwanakambo) wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie; Zainab binti Abu Salamah. Anasema (mpokezi): “Nilimuuliza: Unaonaje, hivi Mtume wa Allah anatokana na ukoo wa Mudhwar? Akajibu: Basi anatokana na ukoo gani mwingine kama sio Mudhwar? Yeye anatokana na kizazi cha Nadhwri mtoto wa Kinaana”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ni Mkuraishi na ukoo wa Kuraishi unatokana na Kinaana ambao ni watoto wa Fihri bin Maalik bin Nadhwri bin Kinaana. Na ukoo wa Kuraishi unagawanyika katika makabila mbali mbali na yaliyo mashuhuri mno miongoni mwa hayo ni kabila la:

  • Jam-hu,
  • Sahmu,
  • Adiyu,
  • Makhzuumu,
  • Taimu,
  • Zuhrah, na
  • Koo za Quswayi mtoto wa Kilaabu, nao ni:
  • Abdud-Daari bin Quswayi,
  • Asad bin Abdul-Uzzaa bin Quswayi, na
  • Abdu Manaaf bin Quswayi. Na zilitokana na huyu Abdu Manaaf koo nne, ambazo ni:
  1. Abdu Shamshi,
  2. Naufal,
  3. Al-Mutwalib, na
  4. Haashimu.

Na kutoka kwenye tumbo (ukoo) hilo la Haashimu ndimo ambamo Allah Mtukufu alimteua Bwana wetu Muhammad mwana wa Abdillah bin Abdul-Mutwalib bin Haashimu. Na hivi ndivyo anavyo lisemea hilo mwenyewe Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika Allah alimteua Kinaana katika watoto wa (Nabii) Ismail, na akawateua Makuraishi kutoka kwenye (kizazi cha) Kinaana. Na akawateua Bani Haashimu miongoni mwa Makuraishi na akaniteua mimi kutoka kwa Bani Haashimu”. Muslim-Allah amrehemu.

Somo letu juma hili la kwanza linatamatia hapa, tunamuomba Allah Mola Mlezi wetu kwa fadhila na neema zake amnufaishe na somo hili kila aliye anza nasi juma hili. Atupe nguvu na atubarikie ufahamu wetu waandaaji wa somo hili la upande wa pili wa Sira, ili tuendelee kukuletea mfululizo wa darasa hizi kila juma. Tukutane juma lijalo kwa uweza wake Mola katika muendelezo wa somo hili, bakia salama mpaka muda huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *