SOMO LA KWANZA – ASILI NA CHIMBUKO LA WAARABU NA USTAARABU (MAENDELEO) WAO.

“SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Kwa auni na msaada wake Allah Mola wetu Mkarimu, leo tena tunaendelea na mfululizo wa darasa zetu za Sira. Juma lililo pita tulijifunza na kuangalia asili na chimbuko la Waarabu ili tupate kumjua vema Mtume wetu ambaye yeye ni Muarabu kwa utaifa. Juma hili tutaendelea kujifunza:

  • Staarabu na maendeleo ya Waarabu:

Ndugu msomaji wetu wa Sira ya Bwana Mtume-Allah akurehemu-fahamu na uelewe ya kwamba hiki kinacho semwa leo “Ustaarabu” na kile kinacho itwa “Maendeleo”, si kitu kipya, bali kimekuwepo dahari na dahari. Kinacho tofautiana ni ule mtizamo na tafsiri ya jamii husika kuielekea dhana hiyo ya ustaarabu na maendeleo kulingana na zama na pengine tuseme na teknolojia.

Naam, ustaarabu kwa maana ya neno lenyewe na maendeleo kama maendeleo yalikuwepo Bara Arabu tangu zama za kale mno. Na miongoni mwa staarabu za Waarabu zilizo kuwa mashuhuri mno, ni pamoja na:

  1. Ustaarabu wa jamii ya Sabai katika nchi ya Yemen:

Jamii hii ya Sabai imetajwa ndani ya Qur-ani Tukufu; sura nzima miongoni mwa sura za Qur-ani imeitwa kwa jina la watu hao. Watu hawa walijaaliwa neema ya mvua nyingi, mikondo na mito mingi ya maji ambayo sehemu kubwa ya maji hayo ilikuwa ikipotea bure kwa kutiririkia baharini. Ili kufaidika na maji hayo na kuyazuia yasipotee bure, watu hao wakajenga matenki na mabwawa makubwa kwa teknolojia ya hali ya juu kuweza kufikirika kuwa iliweza kufanywa na watu wa zama hizo za kale mno. Na bwawa maarufu zaidi miongoni mwa waliyo yajenga, lilikuwa bwawa lililo julikana kwa jina la “Sadu Ma’aribu” na walifaidika na maji yake katika kilimo cha mazao mbali mbali, na bustani zilizo sheheni miti mizuri na matunda matamu.

Kuhusiana na ustaarabu huo, tunaisoma kauli yake Allah Mtukufu: “Hakika ilikuwepo ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao – bustani mbili kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Allah, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu. Lakini wakaacha (kumshukuru kwa neema hizo na wakakufuru), tukawapelekea mafuriko makubwa na tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda makali machungu na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi kwani tunawaadhibu isipo kuwa anaye kufuru?”. Sabaa [34]:15-17

Na mahala pengine, Qur-ani Tukufu imefahamisha uwepo wa vitongoji vilivyo ambatana (pakana/shikamana) katika zama hizo za kale. Vitongoji hivyo vilikuwa kwenye njia inayo toka Yemen kuelekea Hijaazi (Saudi Arabia) mpaka miji ya Shamu (Syria, Jordan, Lebanon na Palestina). Na kwamba misafara ya biashara na wasafiri walikuwa wakitoka Yemen kwenda kwenye miji ya Shamu, hawakosi mahala pa kupumzika kabla ya kuendelea na safari, hawakosi maji wala chakula. Hilo linadokezwa na Mola kupitia kauli yake ndani ya Qur-ani Tukufu: “Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki, tuliweka miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana kwa amani. Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu baina ya safari zetu. Na wakadhulumu nafsi zao, basi tukawafanya ni masimulizi tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo ishara kwa kila mwenye kusubiri sana na akashukuru”. Sabaa [34]:18-19

  1. Ustaarabu wa jamii ya Aadi katika eneo la Ahqaafu nchini Yemen.

Jamii hii ya Aadi iliishi Kaskazini mwa mji wa Hadharamout, katika nchi ya Yemen. Jamii hiyo ndiyo ambayo Allah alimpeleka kwao Mtume Huudi-Amani imshukie. Jamii hiyo iliundwa na watu wenye umahiri mkubwa katika ujenzi wa majumba makubwa madhubuti na ya kifakhari, na walikuwa na mabustani yenye matunda kweche kweche. Hali kadhalika, Allah aliwaneemesha kwa kuwapa anuwai (aina mbali mbali) za mimea, mazao na mito mingi.

Jamii hiyo ndio inayo tajwa na Allah katika Qur-ani kwa kauli yake: “Kina Aadi waliwakanusha Mitume. Alipo waambia ndugu yao Huud: Je! hamchiMngu? Hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. Basi mcheni Allah na nitiini mimi. Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko ukumbusho wa kufanyia upuuzi? Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. Basi mcheni Allah na nitiini. Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. Na mabustani na chemchem”. As-shu’araa [26]:123-134

  1. Ustaarabu wa jamii ya Thamuud katika nchi ya Hijaazi (Saudi Arabia).

Qur-ani Tukufu inafahamisha juu ya uwepo wa ustaarabu na maendeleo katika eneo la “Hijri” na ikadokezea juu ya nguvu walizo kuwa nazo watu walio ishi kwenye eneo hilo. Watu hao walikuwa mahiri mno katika uchongaji wa majabali kwa ustadi mkubwa na kuyageuza kuwa nyumba zao za kuishi zilizo pendeza. Aidha, walikirimiwa na Allah kwa kuwa na mito mingi kwenye eneo lao hilo, jambo lililo pelekea wao kuwa na viunga adida (vingi) vya mitende na aina mbali mbali za nafaka na matunda.

Watu hao ndio anao wataja Allah kupitia kauli yake: “Kina Thamud waliwakanusha Mitume. Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! hamumchiMngu? Hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. Basi mcheni Allah na nitiini. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? Katika mabustani na chemchem? Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. Basi mcheni Allah na nitiini mimi”. As-shu’araa [26]:141-150

Pia Allah akawazungumzia katika kauli nyingine: “Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa Aadi na akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Allah wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi. Al-A’araaf [07]:74

Ustaarabu na maendeleo hayo yalitoweka kitambo mno na hayakusalia ila magofu na mabaki yanayo dokeza juu ya uwepo wao na utamaduni wao. Miji na vitongoji vyao vyote vimefutika juu ya uso wa ardhi, mito imekauka, viunga na makonde nayo yote yameangamia na kuiacha ardhi ikiwa kame isiyo otesha kitu.

Hilo ndilo somo letu juma hili, tunatumai kwa uwezo wake Allah, tutakuwa tunaendelea vizuri pamoja na utakuwa umeshapata maarifa na elimu juu ya asili, staarabu na maendeleo ya Waarabu. Tumuombe Allah atupe nguvu ili tuzidi kuelimishana kwa lengo la kumjua vema Mtume wetu ili tupate kumpenda na kisha kumfuata kama lilivyo agizo na amri yake. Allah atukutanishe tena juma lijalo, tukiwa na  siha njema. Maa Salaam!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *