SOMO LA KUMI NA SITA

MANDHARI NA VITISHO VYA SIKU YA KIYAMA

Ewe Mola wetu! Ni zako Wewe tu sifa njema zote na shukrani zote. Ni zako Wewe tu sifa njema zote kwa namna inayo lingana na utukufu wako na ukubwa wako. Ni zako Wewe tu sifa njema mpaka uridhike na pale unapo ridhika na baada ya kuridhika. Na Swala na Salamu zimfikie kipenzi chetu Mtume Muhammad, jamaa zake, maswahaba wake wote na kila aliye/anaye/atakaye iandama njia yao kwa wema mpaka siku ya jazaa na malipo kwa jinsi ya amali.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Kwa mara nyingine tena tunasema Himda na sifa zote njema ni stahiki yake Allah, ambaye ametuneemesha kukutana tena katika juma hili. Ewe Mola wa haki! Tujaalie kuwa miongoni mwa wenye kuzishukuru neema zako na wenye kuzikumbuka fadhila zako. Tusamehe dhambi zetu hali ya kuwa Wewe ndiye Mbora wa kusamehe.

Naam, jukwaa letu la leo, litaendelea kuongozwa na anuani mama kama inavyo someka mbele yetu:

Mandhari na vitisho vya siku ya Kiyama.

Naam, ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kuishi na kukiangalia kipengele kingine kinacho someka:

  • Siku ya Kiyama, eeh siku iliyoje hiyo!

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tumeitaja sana siku ya Kiyama katika darsa za jukwaa letu hili kwa kiasi ambacho huenda ukawa umekereka au umekimwa. Lakini je, pamoja na kuitaja kwa wingi siku hiyo, umekwisha jiuliza ni kwa nini tumefanya hivyo? Umekwisha ijua na kuitambua ni siku gani hiyo na ina uzito na nafasi gani kwako? Na je, umesha jaribu kuvuta hisia ukaiona mandhari ya siku hiyo, urefu, uzito, ugumu na utisho wake na hali yako itakavyo kuwa?

Ikiwa bado hujaijua au hujapata lau taswira inayo weza kubebwa na akili yako, basi sisi na wewe tujue na tutambue ya kwamba siku ya Kiyama:

  • Hakika hiyo ni siku Allah; Mfalme wa siku hiyo ataitia ardhi (ulimwengu mzima) mkononi mwake na atazikunja mbingu kwa mkono wake wa kuume. Hilo analisema Yeye aliye Mtukufu kwa kauli yake Mwenyewe: “Na wala hawakumuhishimu Allah kama anavyo stahiki kadiri yake. Na siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayo mshirikisha nayo”. Az-zumar [39]:67

Si hivyo tu, lakini Yeye aliye tukuka akaeleza namna zitakavyo kunjwa mbingu, akasema: “Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao”. Al-Anbiyaa [21]:104

Na Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Abdillah bin Masoud-Allah awawiye radhi-ya kwamba alikuja Muyahudi mmoja kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Ewe Muhammad! Hakika Allah atazikunja mbingu kwa kidole kimoja, na ardhi kwa kidole (cha pili), na majabali kwa kidole (cha tatu), na miti kwa kidole (cha nne) na wanaadamu kwa kidole (cha tano), kisha aseme: Mimi ndiye Mfalme. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akacheka mpaka yakaonekana magego yake, kisha akasoma: “Na wala hawakumuhishimu Allah kama anavyo stahiki kadiri yake. Na siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume. Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayo mshirikisha nayo”. Az-zumar [39]:67

Na imepokewa kutoka kwa Imamu Muslim-Allah amrehemu-kwa riwaya ya Abdillah bin Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Siku ya Kiyama, Allah atazikunja mbingu kisha atazikamata kwa mkono wake wa kuume, halafu atasema: Mimi ndiye Mfalme! Wako wapi wale walio kuwa majeuri? Wako wapi wale walio kuwa wajivuni? Kisha ataikunja ardhi kwa mkono wake wa kushoto”.

  • Hakika hiyo ni siku ambayo bahari zitapasuka pasuka na kuwaka moto “Na bahari zitakapo pasuliwa”. Al-Infitwaar [82]:03 “Na bahari zikawaka moto”. At-takwiir [81]:06

Hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya yake Mola huenda tukapata japo taswira ndogo inayo ingia akilini hata tukauona ugumu, uzito na utisho wa siku hiyo. Sote tunafahamu ya kwamba maji huzima moto, lakini kutokana na kishindo na kizaizai cha siku hiyo maji yenyewe ndio yatawaka moto, hayatakuwa na uwezo tena wa kuuzima moto, yatakuwa zaidi ya petroli – Sub-haanallah!

Si hivyo tu, bali hiyo ni siku ambayo milima iliyo kita na kuishikilia ardhi itavurugwa vurugwa na kupeperushwa itawanyike na kuwa kama vumbi litimkalo au sufi zilizo chambuliwa na ilhali ilikuwa ni miamba migumu kuvunjika kwake. Allah Ataadhamiaye anasema: “Siku ambayo ardhi itatikiswa na milima pia, na milima itakuwa kama tifutifu la mchanga”. Al-muzammil [73]:14

Na amesema Yeye aliye Mtukufu: “Na litapo pulizwa baragumu mpulizo mmoja tu. Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja. Siku hiyo ndio tukio litatukia. Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa”. Al-Haaqah [69]:13-16

Isitoshe, Allah Mtukufu atafanya zaidi ya hivyo, ataiondosha milima kutoka pale alipo iweka tangu ile siku aliyo iumba dunia, anasema Yeye aliye na utukufu: “Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivuruga vuruga. Na ataiacha tambarare, uwanda. Hutaona humo mdidimio (bonde) wala muinuko”. Twaaha [20]:105-107

Na akasema Yeye mwenye utukufu na enzi: “Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi”. An-Nabaa [78]:20

  • Ewe ndugu mwana jukwaa uliye mwema-Allah akurehemu-eeh ni siku iliyoje hiyo siku ya Kiyama! Tuseme nini hata tuujue ugumu, uzito, mshindo na kizaizai chake! Siku hiyo hata hizi mbingu iliyo nzuri mandhari yake kuitazama mchana pale jua linapo angaza hata usiku pale mwezi na nyota zinapo zagaza nuru. Mbingu ambazo nyoyo na macho yanaburudika kwa kuzitazama, hizo basi siku hiyo zitapasuka pasuka mpasuko mkubwa ambao haujapata kutokea tangu kuumbwa kwake, waidhika na upulike: “Itapo chanika mbingu. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa kumsikiliza”. Al-Inshiqaaq [84]:01-02

Basi zitakuwa nyonge na dhaifu: “Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa”.

Kama vile haitoshi, hata ile rangi nzuri ya bluu ya mbingu, hiyo nayo pia itaondoka na kutoweka kabisa na mbingu itaanza kubadilika rangi kama zinavyo badilika rangi zinazo pakwa vitu. Itabadilika na kuwa nyekundu na mara nyingine itakuwa manjano na wakati mwingine itakuwa ya kijani na tena ikarudi kuwa ya bluu, kama alivyo sema Allah aliye Mtukufu: “Itakapo pasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta”. Ar-Rahmaan [54]:37

  • Naam, ewe mwana jukwaa-Allah akurehemu-kutokana na uzito, ugumu na kishindo cha Kiyama hata hili jua ambalo Allah amelifanya kuwa ni mojawapo ya sababu za uhai, nalo litakusanywa na utatoweka mwangaza wake kama alivyo sema Allah Mtukufu: “Jua litakapo kunjwa”.

Lakini pia huu mwezi tunao uona katika sura angavu iliyo nzuri hata ikawaliwaza wasafiri, huo nao utapatwa na kutoweka mwangaza wake kama alivyo sema Yeye aliye Mtukufu: “Basi jicho litapo dawaa. Na mwezi utapo patwa”. Al-Qiyaamah [75]:07-08

Na hizi nyota pia zinazo ipamba mbingu nazo zitatawanyika na kupukutika kama ilivyo kwenye kauli yake Allah Mtukufu: “Na nyota zitapo tawanyika”. Na akasema Yeye aliye Mtukufu: “Na nyota zikazimwa”.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe Mola wa haki! Ewe ambaye hakuna mponyaji ila kwa idhini yako, tunakuomba kwa uwezo wako mkuu katika uponyaji na kila kitu, uwaponye walio wagonjwa miongoni mwetu. Wasamehe na uwarehemu wazazi wetu, waalimu na masheikh zetu, ndugu na jamaa zetu walio kwisha tangulia mbele yako. Nasi uturehemu kabla ya kuja kwako, turuzuku husnul-khaatima na tufishe hali ya kuwa ni Waislamu. Wanusuru ndugu zetu Waislamu wanao teseka kwa vita na njaa ulimwenguni kote kwa sababu ya fitina za makafiri. Hakika Wewe ni Msikivu na Mpaji. Yaa Rabbi tutakabalie dua!

Kwa uchache, hayo ndio tuliyo jaaliwa na Allah Mtukufu katika kukumbushana kwetu kupitia jukwaa letu hili la kila juma. Tuendelee kuyatafakari na kuyafanyia kazi mpaka hapo tutakapo jaaliwa kukutana tena juma lijalo.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ جَعَلَ اللَّهُ عَلَيْكُمُ اللَّيْلَ سَرْمَدًا إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَهٌ غَيْرُ اللَّهِ يَأْتِيكُمْ بِضِيَاءٍ أَفَلَا تَسْمَعُونَ٧١ قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ جَعَلَ اللَّهُ عَلَيْكُمُ النَّهَارَ سَرْمَدًا إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَهٌ غَيْرُ اللَّهِ يَأْتِيكُمْ بِلَيْلٍ تَسْكُنُونَ فِيهِ أَفَلَا تُبْصِرُونَ٧٢ [القصص: 71-72]

Sema: Mwaonaje, Allah angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Allah atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? Sema: Mwaonaje, Allah angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Allah atakaye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?” Al-Qaswas [28]:7172

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *