SOMO LA KUMI NA SABA

MANDHARI NA VITISHO VYA SIKU YA KIYAMA.

Mstahiki wa kuhimidiwa na kutukuzwa ni Allah; Mola Muumba wetu, nasi waja wake hatuwezi kumuhimidi na kumtukuza ila kwa kuwezeshwa naye. Ewe Mola Muumba wetu! Kwa rehema na fadhila zako tuwezeshe kukuhimidi na kukutukuza ili tupate radhi zako. Na tunakuomba umshushie rehema na amani mja na Mtume wako; Bwana wetu Muhammad, Aali na swahaba zake wote na wote walio muamini na kumfuata mpaka siku watakapo simamishwa viumbe wote mbele yako kwa ajili ya hisabu, hukumu na jazaa sawiya.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Yaa Rabbi! Kama ulivyo tujumuisha tena katika jukwaa letu juma hili kwa uweza na ukarimu wako, tunakuomba kwa uwezo na ukarimu wako huo uibariki milango yetu ya fahamu ili tuweze kuyafahamu na kukumbushika na haya utakayo tujaalia kukumbushana leo.

Naam, jukwaa letu la leo, litaendelea kuongozwa na anuani mama kama inavyo someka mbele yetu:

Mandhari na vitisho vya siku ya Kiyama.

Naam, ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kuishi na kukiangalia kipengele kingine kinacho someka:

  • Ewe masikini weeh! Jiandae na siku hiyo.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-nawe ujihurumie na ujiandae na siku hiyo ambayo ni kikubwa mno kishindo na kitisho chake, ni mrefu mno muda wake, Mtawala na Mfalme pekee wa siku hiyo wake ni Yule aliye Mtenza nguvu, ambaye ndiye atakaye uliza siku hiyo: “…Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Allah Mungu Mmoja Mtenza nguvu”. Jisikitikie na uihurumie nafsi yako kukutana na kufikiwa na siku hiyo ngumu, siku ambayo watu wataambiwa: “Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo yachuma (yatenda). Hapana dhulma leo. Hakika Allah ni Mwepesi wa kuhisabu”. Ehee, ewe ndugu yangu wee! Siku hiyo si ya mchezo, ni siku inayo hitaji maandalizi ya kukutana nayo na dunia ndio uwanja wa maandalizi hayo. Hebu uone ugumu na uujue uzito wa siku hiyo, hiyo ndio siku ambayo utaiona/utaziona:

  • Mbingu zikiwa zimekunjwa kunjwa mkunjo wa karatasi,
  • Nyota zikiwa zimepukutika na kuzimwa nuru yake,
  • Jua likiwa limekunjwa,
  • Milima ikiwa imeondolewa,
  • Ngamia wenye mimba wakiwa wametelekezwa,
  • Wanyama wa mwituni wakiwa wamekusanywa,
  • Bahari zikiwa zinawaka moto,
  • Nafsi zikaunganiswa,
  • Jahannamu ikiwa inachochewa,
  • Pepo ikiwa imesogezwa,
  • Ardhi ikiwa imetanuliwa,
  • Ardhi ikiwa imetetemeshwa kwa mtetemeko wake. Na ardhi ikatoa toa mizigo yake. Siku hiyo watu watatoka kwa mfarakano wakaonyweshwe vitendo vyao.
  • Ardhi na milima ikiondolewa na ikavunjwa mvunjo mmoja,
  • Tukio likiwa limetukia,
  • Mbingu zikiwa zimepasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu,
  • Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
  • Siku hiyo mtahudhurishwa – haitafichika siri yenu yoyote.
  • Siku tutakapo iondoa milima na ukaoina ardhi i wazi,
  • Siku milima itakapo sagwasagwa, iwe mavumbi yanayo peperushwa,
  • Siku ambayo watu watakuwa kama nondo walio tawanyika. Na milima itakuwa kama sufi zilizo chambuliwa,
  • Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataiharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Allah ni kali.
  • Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu pia. Nao watahudhuria mbele ya Allah Mmoja, Mwenye nguvu.
  • Siku milima itapo peperushwa mpeperusho na ikaachwa kuwa tambarare, uwanda. Hutaona humo mdidimio wala muinuko.
  • Siku utapo iona milima unaidhania imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu.
  • Siku utaiona mbingu imepasuka ikawa nyekundu kama mafuta.
  • Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini.
  • Siku hiyo watu aasi watazuiwa kuzungumza. Wala hawataulizwa siku hiyo juu ya kukosea kwao bali watashikwa kwa nywele zao za utosini na kwa miguu.
  • Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya iliyo ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye.
  • Siku ambayo kila nafsi itajua ilicho kitanguliza na ilicho kibakisha nyuma.
  • Siku ambayo ndimi zitatiwa ububu na vitazungumza viungo vyake mtu.
  • Siku ambayo utajo wake ulimtia mvi Bwana wa Mitume wote, pale yule msadikishaji; Abubakri alipo mwambia: Nakuona umeota mvi ewe Mtume wa Allah! Akajibu (Mtume): “Imenitoa mvi (Surat) Huud na ndugu zake”. Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 3720]-Allah amrehemu.

Na ndugu zake Surat Huud anao wakusudia Bwana Mtume, ni Surat Al-Waaqi’ah (56), Al-Mursalaat (77), Amma yatasaaluun (78), na Idhas-shamsu kuwwirat (81)

Ewe ndugu yangu-Allah akurehemu-ewe mtu wee! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu? Pale milango ya amali itakapo fungwa na pazia za mbingu zitakapo shushwa viumbe wasione yaliyoko mbinguni na hapo maovu yakachukiwa; watu wakaacha kutenda dhambi. Hebu fikiri sasa kabla hujafikiwa na siku hiyo, utafanya nini wakati ambapo viungo vyako vitatoa ushahidi dhidi yako kama anavyo sema Allah aliye tukukia: “Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma”. Yaasin [36]:65

Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda”. An-Nuur [24]:24

Basi eeeh ole wetu! Tena ole wetu sisi tulio ghafilika, hata tukaacha kumuabudu Mola wetu aliye tuumba! Mola wetu Mlezi, ambaye ametuletea Bwana wa Mitume na akamteremshia Kitabu ambacho hukumu zake ziko wazi ili atuongoze kwa muongozo wake, nasi tukakataa kumfuata mtume huyo na kitabu alicho kuja nacho. Ewe ndugu yangu, unafikiri Allah atatufanya nini kwa mghafala na ukaidi wetu huo?! Tutakuwa na udhuru gani tena baada ya yote hayo?!

Kisha Allah Mtukufu akatutajia wasifu wa siku ya malipo; siku ya Kiyama, halafu akatujulisha kughafilika kwetu, akasema: “IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza. Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo. Zimeghafilka nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong’onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binadaamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona?”. Al-Anbiyaa [21]:01-03

Halafu tena anatujuza kukaribia kwa Saa ya Kiyama, anasema: “Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!’. Al-Qamar [54]:01

Hakika wao wanaiona iko mbali. Na Sisi tunaiona iko karibu”. Al-Ma’aarij [70]:06-07

Sasa basi, baada ya maelezo yote hayo ya Allah ambaye ndiye ametuwekea hiyo siku ngumu na nzito mno ya Kiyama, ni jukumu letu sisi ambao tumeumbiwa hicho Kiyama, kulifanyia kazi somo la Qur’ani na tuyazingatie maana yake na wala tusiangalie sifa na majina ya siku hiyo…. Unasubiri nini kujiandaa na siku hiyo, anza leo kabla hujajuta na kusaga meno, tusome na tuwaidhike sote: “Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako Mlezi, au zifike baadhi ya ishara (aya) za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika baadhi ya ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake. Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja”. Al-An’aam [06]:158

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe ambaye unapo litaka lako, husema tu kuwa na likawa! Yaa Rabbi tuhifadhi na kila balaa litokalo mbinguni au ardhini, mashariki au magharibi, kaskazini au kusini, juu au chini. Ewe Mola wetu Mkarimu! Sisi ni waja wako dhaifu sana, hatuna pa kukimbilia ila kwako tu, tusamehe na utufutie madhambi yetu. Tuhifadhi na shari za wanaadamu wenziwetu, majini na baki ya makhuluku wako wengine. Ewe Mola Mwingi wa ukarimu na upaji, usiirejeshe patupu mikono yetu dhalili. Aamina yaa Rabbal-A’alaamiina!

Kwa juma hili, hayo ndio tuliyo jaaliwa na Allah; Mola Mlezi wa walimwengu wote kukumbushana katika jukwaa letu hili, tunatamatia hapa huku tukimuomba akili na utayari wa kuyakubali makumbusho haya na kisha kuyatia matendoni kwa maslahi na manufaa yetu wenyewe, leo hapa duniani na kesho kule Akhera.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine katika anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

مَثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ فِيهَا أَنْهَارٌ مِنْ مَاءٍ غَيْرِ آسِنٍ وَأَنْهَارٌ مِنْ لَبَنٍ لَمْ يَتَغَيَّرْ طَعْمُهُ وَأَنْهَارٌ مِنْ خَمْرٍ لَذَّةٍ لِلشَّارِبِينَ وَأَنْهَارٌ مِنْ عَسَلٍ مُصَفًّى وَلَهُمْ فِيهَا مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَمَغْفِرَةٌ مِنْ رَبِّهِمْ كَمَنْ هُوَ خَالِدٌ فِي النَّارِ وَسُقُوا مَاءً حَمِيمًا فَقَطَّعَ أَمْعَاءَهُمْ١٥ [محمد: 15]

Mfano wa pepo walio ahidiwa wachaMngu ina mito ya maji yasiyo vunda, na mito ya maziwa isiyo haribika ladha yake, na mito ya mvinyo yenye ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyo safishwa. Na wao humo watakuwa na kila aina ya matunda, na maghfira kutoka kwa Mola wao Mlezi. Basi hao ni kama watakao dumu motoni na wakinyweshwa maji yanayo chemka ya kuwakata matumbo yao?” Muhammad [47]:15

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *