MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.
Atakaswe na adhukuriwe Allah asemaye: “Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa haki. Na anapo sema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni haki. Na ufalme wote ni wake siku litapo pulizwa baragumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari”. Mola wetu Mtukufu tunakuomba umfikishie Sala na Salamu Bwana wetu Muhammad, Aali, Sahaba na jamia ummati wake.
Ama baad,
Mpendwa mwana-jukwaa letu.
Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!
Naam, ndugu mwana jukwaa mwenzetu-Allah akurehemu-juma hili tena kwa fadhila zake Allah Mtukufu tumekutana katika kuendelea na mfululizo wa makala zetu za kukumbushana kuhusiana na siku ngumu na nzito iliyo mbele yetu, siku ambayo tumependa au hatukupenda ni lazima tutakutana nayo tu. Tumuombe Mola Mlezi wetu atusaidie tuweze kukumbushana, kuzingatia na kujiandaa na siku hiyo kwa kutenda amali njema zinazo mridhi na kuacha kabisa matendo maovu yanayo mchukiza.
Mandhari ya wakanushaji na makafiri.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele tulicho kianza juma lililo pita, kipengele kisomekacho:
- Fitina ya wafuataji (wafuasi) na wafuatwa (viongozi).
Naam, bado tunaendelea kuitazama filamu yetu inayo itwa “Fitina ya wafuasi na wafuatwa”, filamu inayo letwa kwako kila juma na Televesheni Qur’ani, leo tuendelee kuitazama sehemu ya pili ya filamu hiyo. Na ili tupate kuendelea vema na sehemu hii ya pili, basi na tuanzie na pale tulipo ishia juma lililo pita:
Maneno/swali lao hilo kwa walio kuwa wafuasi wao, ni kukiri kwao ya kwamba wao waliwapambia kutenda dhambi na ukafiri na kwamba wao hawakuwatenza nguvu katika hilo. Bali wafuasi wao wanyonge ndio walio kuwa tayari kukubali na kupokea ukafiri na utenda dhambi huo. Hapo sasa, ndio zinakuja radi (jawabu jibishi/rejeshi) mkataa kutoka kwa wale wanyonge ambao duniani hawakuwa na uwezo hata wa kutamka neno moja. Lakini baada ya kuondoka kwa utawala wa wakubwa wale kwa kuondoka kwa dunia na haki ikadhihiri wazi kama ulivyo uwazi wa jua la mchana, wakasema: “… Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha kumkufuru Allah, na tumfanyie washirika…”. Sabai [34]:33
Yaani: Vitimbi vyenu havikukoma usiku wala mchana katika kutuzuia na uwongofu, kwani nyinyi ndio mlio tupambia upotofu na mkatushajiisha kufanya ufisadi na mkisema kwamba hiyo ndio haki. Kisha leo mnaitia dosari haki ile na mnadai kwamba hiyo ni batili, na vitimbi vyenu havikutuacha mpaka mkatupoteza na kutufitinisha!!
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-vitimbi viko aina nyingi na vinabadilika badilika kulingana na zama, katika zama za kuteremka kwa Qur’ani vitimbi vya makafiri wa Kikuraishi vilikuwa ni kutunga kwenye baraza (vijiwe) zao anuwai za mashairi. Watu wa zama hizo walikuwa mahiri mno katika fani hii ya ushairi, na ushairi ulikuwa ni mojawapo ya njia kuu za kufikisha ujumbe kwa hadhira. Mashairi yakatungwa na kusomwa mbele ya kadamnasi, lengo likiwa ni kumchafua, kumbomoa, kumpaka matope ya tuhuma batili, kumtukana na kumvunjia heshima Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na mashairi hayo ya matusi hayakuwasaza pia wale wote walio kuwa pamoja na Bwana Mtume. Na hali kadhalika mashairi hayo yalilenga kuwazuia watu kuisikiliza haki au kuchochea fitina ya gonjwa la ukabila na umajimbo/ukanda na kujifakharisha kwa nasaba.
Ama fitina na vitimbi vya makafiri kwa Waumini wa zama hizi vinatofautiana na vile vya zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Vitimbi na fitina kubwa ya zama zetu hizi ni tekinolojia hususan ile ya habari, simu hizi na televisheni hizi pamoja na faida zake lakini zimekuwa na maafa makubwa kwa jamii zetu. Leo watoto wetu wamekuwa waraibu wakubwa wa hizo zinazo itwa “game”, muda wote ni wao na game kiasi cha kufikia kutopenda chochote zaidi ya game. Na wako tayari hata kuiba kitu majumbani mwao na kwenda kukiuza ili tu wapate pesa za kwenda kucheza game kwenye mabanda au hata kununua game zao wenyewe. Watoto hawakai majumbani mwao, sababu ni game, watoto hawana muda wa kudurusu/kutwalii masomo yao, kisa ni game, watoto wanasinzia madarasani, chanzo ni hizo game. Matokeo ya uraibu huo wa game kwa watoto wetu, ni kuporomoka vibaya mno kwa maendeleo yao ya kitaaluma sanjari na kuporomoka kwao kimaadili. Game ni fitina na vitimbi vya zama zetu za leo, wakubwa wametutengenezea kwa malengo maalumu na la mbele yao likiwa ni kutuzuilia na njia ya Allah nasi tumeangukia kuwa mateka wa tekinolojia hiyo.
Haya na simu zetu hatupingi kuwa zimerahisisha mambo mengi, lakini pia zimeleta balaa na maafa makubwa kuliko faida zake. Leo watoto wadogo wanayajua mambo ya kikubwa kuliko hata hao watu wakubwa wenyewe, mwalimu wao ni simu, simu tunawanunulia sisi wenyewe kisha wakajifungia vyumbani mwao usiku ndani ya nyumba zetu wenyewe, wazazi tukijua wamelala, kumbe wanakesha na simu katika kutazama mambo ya kikubwa. Baada ya hapo ni nini, ni wao kuyaiga hayo waliyo kesha wakiyaona kisha asubuhi wakawa ni wenye kusinzia shuleni. Simu zetu hazipungui kuwa ni fitina na vitimbi vya zama zetu hizi, tutahadhari na tuchunge matumizi yetu ya tekinolojia hizi. Simu hizo! Leo mume yuko chumbani anamsubiri mke wake, lakini mke yuko ukumbini akiangalia tamthilia mpaka usiku wa saa sita, akiingia chumbani tayari mumewe amekwisha lala kutokana na uchovu wa mchana kutwa katika kutafuta mkate wa familia yake. Tabia hiyo haiko kwa wanawake peke yao, bali pia wanamume nao hukesha katika kuangalia mechi za mpira za timu za Ulaya mpaka usiku wa manane wakiwaacha vitandani wake zao peke yao. Jambo hili limefikia kiasi cha kupelekea kuvunjika kwa baadhi ya ndoa. Haya niambie hapo televisheni haijawa fitina ya zama zetu hizi?! Wakubwa wanatengeneza, sisi tunatumia. Uislamu haukutukataza kutumia tekinolojia, laa hasha! Lakini unacho taka Uislamu kwetu sisi ni kutokuwa muhanga, mateka na watawaliwa wa tekinolojia hizo, bali sisi ndio tuwe watawala wake tukizitumikisha katika maendeleo yetu katika dunia na dini yetu kwa maslahi ya akhera yetu. Tekinolojia isiwe ndio sababu ya kukosa swala, isiwe ndio chanzo cha kuvunjika kwa ndoa zetu, isiwe ndio sababu ya kuanguka kitaaluma kwa watoto wetu na kuporomoka kwao kimaadili. Hivyo ndivyo “vitimbi vya usiku na mchana” watakavyo vitaja wale wafuasi wanyonge wa mabwana wakubwa siku ya Kiyama kama inavyo nukuliwa na Qur’ani tukufu: “… Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha kumkufuru Allah, na tumfanyie washirika…”. Sabai [34]:33
Haya sasa, ewe ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-sisi na wewe na tujiulize swali hili: Je, muislamu atakuwa na udhuru wa kujitetea mbele za Allah kwa kuishi kwake na vitimbi na fitina hizi za zama zetu? Tuwe wakweli kama inavyo kiri mioyo yetu ingawa ndimi na nafsi zetu zinataka kupiga chenga, muislamu kabisa hatakuwa na la kujitetea mbele za Allah, kwani ni yeye ndiye aliye inunua tekinolojia na akaitia nyumbani mwake pasina kuelekeza na kusimamia matumizi yake. Na natija ikawa badala ya tekinolojia hiyo kunufaisha na kufaa, ikawa ni balaa na maafa yanayo ambukia; yanaangamiza dunia na akhera yake. Na ndio maana pale watakapo walaumu wale mabwana wakubwa, nao watawajibu kama inavyo nukuu Qur’ani Tukufu kupitia filamu yetu: “… Kwani sisi ndio tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ndio wakosefu”. Sabai [34]:32
Na hapa ndipo tunajua na kufahamu ya kwamba mdahalo huo baina ya walio kuwa wanyonge wafuasi na wale walio takabari wafuatwa, hautawanufaisha hawa wala wale zaidi ya hawa kuwakataa wale. Hivyo ni kwa sababu siku hiyo ya Kiyama kila mmoja kati ya makundi mawili hayo atajua kwa yakini kwamba yeye ni dhaalimu wa nafsi yake anaye stahiki adhabu. Akajuta katika wakati ambao majuto hayatamnufaisha kwa chochote na atatamani lau angeliifuata haki na akawa muumini: “… Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa wakiyatenda?”. Sabai [34]:33
Hapo tena jambo likahukumiwa, mdahalo ukafungwa na mjadala ukaisha. Na katika Suratil-Baqarah, Allah Ataadhamiaye anasema: “Na katika watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa Allah. Wanawapenda kama kumpenda Allah. Lakini walio amini wanampenda Allah zaidi sana…”. Al-Baqarah [02]:165
Yaani: Pamoja na dalili/hoja hizi zilizo wazi, zenye kuonyesha utawala/mamlaka ya Allah, ukubwa wa nguvu na uwezo wake, bado wamepatikana miongoni mwa watu wanao mpa Allah washirika. Wakawaabudu washirika hao wa Allah na wakawapenda kama waumini wanavyo mpenda Allah. Au kama ambavyo washirikina hao wanavyo mpenda Allah ndivyo kwa kadiri hiyo hiyo wanavyo ipenda miungu yao hiyo waliyo ifanya kuwa ni washirika wa Allah katika ibada. Lakini waumini wanampenda mno Allah kuliko ambavyo wao washirikina wanavyo ipenda miungu yao hiyo kinyume cha Allah: “… Na laiti walio dhulumu wakajua watakapo iona adhabu kuwa nguvu zote ni za Allah na kuwa Allah ni mkali wa kuadhibu”. Al-Baqarah [02]:165
Yaani: Lau kuwa wale walio dhulumu (washirikina na makafiri) kwa namna walivyo kuwa wakiipenda miungu yao kama wanavyo mpenda Allah, laiti wataiona hali yao wakati watakapo iona adhabu siku ya Kiyama. Na watakapo iona nguvu ya Allah na utisho wake na wakaona ushindwa wa miungu yao katika kuwaondoshea japo sehemu ndogo tu ya adhabu ya Allah “Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio wafuata, na hali ya kuwa wamekwisha iona adhabu; na yatakatika mafungamano yao. Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyo tukataa sisi! Hivyo ndivyo Allah atakavyo waonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka motoni”. Al-Baqarah [02]:166-167
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-katika kitatange hicho, ndio watatamani wale walio kuwa wafuasi wa mabwana wakubwa, watatamani kurudi tena duniani kwenye ulingo wa amali (matendo) ili watende amali njema. Na wawakatae wadau wa ukafiri na upotofu kama ambavyo wao wanavyo wakataa leo akhera kwenye uwanja wa hisabu na jazaa ya amali walizo tenda duniani. Lakini wapi eeeh, litapatikanaje hilo! Eeeh! Majuto yaliyoje watakayo kuwa nayo!
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele hiki hiki cha fitina ya wafuasi na wafuatwa chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.
Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:
“Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na moto na akatiwa peponi, basi huyo amefuzu. Na maisha ya Dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu”. Aali Imraan [03]:185