MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.
“MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI”
Shukrani na sifa zote njema ni milki na stahiki yake Allah Mola Muumba wa mbingu saba na ardhi saba na vyote vilivyomo baina ya mbingu na ardhi. Tunamshukuru kwa neema zake nyingi zisizo dhibitika na kubwa kuliko zote ni hii neema ya Uislamu. Na hatuchoki kumbembeleza na kumuomba atufikishie Sala na Salamu kwa kipenzi chetu Mtume Muhammad; aliye Mbora wa wakumbushaji, ziende na ziwafikie pia Aali, Sahaba na umati wake jamia.
Ama baad,
Mpendwa mwana-jukwaa letu.
Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!
Naam, ni juma jingine ambalo kwa uwezo wake Mola ametukutanisha tena katika jukwaa letu hili la ukumbusho. Ndugu mwana jukwaa letu-Allah akurehemu-tuanze kwa kumshukuru Allah Mtukufu ambaye kwa mapenzi yake makuu kwetu ametukutanisha katika ukumbi huu wa kukumbushana ili tupate kuuona ukaribu wa siku ile iliyo ahidiwa; siku yenye vituko na vishindo vikuu. Lengo letu likiwa ni kutanabahishana ili tufanye maandalizi mema mazuri yatakayo kuwa nusra kwetu katika siku hiyo isiyo kwepeka wala kimbilika. Hivyo basi tunakusihi uendelee kuwa nasi, hasaa huenda uokovu wetu ukapatikana kwa njia hii ya kukumbushana juu ya siku ngumu iliyo karibu mno kuwadia. Haya turuhusu tukukaribishe kwa kusema: Karibu katika somo letu linalo endelea kwa majuma kadhaa sasa, ambalo anuani yake inasomeka:
Mandhari ya wakanushaji na makafiri.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele tulicho kianza juma lililo pita, kipengele kisomekacho:
- Fitina ya wafuataji (wafuasi) na wafuatwa (viongozi).
Na mandhari yanaendelea na kufuatana:
Naam, kupitia Televisheni Qur’ani tunaendelea kutazama filamu inayo tuonyesha mandhari ya fitina ya wafuataji na wafuatwa. Mandhari yanaendelea ili kuzidi kutuwekea wazi magomvi na makataano ya watu wanyonge wafuataji na wale mabwana wakubwa; viongozi, wafalme na matajiri wafuatwa. Allah Mwenye utukufu na ukarimu anatuambia: “Na wote watahudhuria mbele ya Allah. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Allah? Watasema: Lau Allah angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri, hatuna pa kukimbilia”. Ibraahim [14]:21
- “Na wote watahudhuria mbele ya Allah”.
Wote; wale watu walio kuwa waasi wakanushaji na wafuasi wao katika wale walio kuwa watu wanyonge wakipokea na kutekeleza kila walicho pewa na kuambiwa na mabwana wakubwa, tena wakiwa na kiongozi wao mkuu; shetani-mrujumiwa mawe. Kisha wale walio waamini mitume walio tumwa na Mola wao kwao na baada ya kuwaamini wakatenda amali njema kusuhubiana na imani yao hiyo, wote hao watahudhuria waonekane na daima wao wanaonekana mbele ya Allah. Lakini wao wakati huo watajua fika na watahisi hasa kwamba wao wamewekwa wazi; hawana kinacho waficha yasijulikane mambo yao, hawana kinacho wasitiri wala kinacho wakinga kama walivyo kuwa wakidhani huko duniani. Wote watahudhuria na uwanja utajaa na pazia litaondoshwa, hapo sasa mambo yote yako hadharani, ndipo mdahalo utaanza: “Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Allah?”
Na wanyonge ndio wanyonge, hao ndio wale walio litupa jambo tukufu kuliko yote aliyo pewa mwanaadamu tu; uhuru wao wa kibinaadamu katika kufikiri, kuamini na kuelekea. Wakautupa uhuru wao huo kwa thamani duni, wakawafuata wale walio takabari, walio waasi. Wakawanyenyekea wasio Allah miongoni mwa waja wake, na huo unyonge wao walio jivika wenyewe hautakuwa udhuru wa kutoadhibiwa mbele za Allah, bali huo ni kosa/uhalifu. Kwani Allah hataki yeyote awe mnyonge na ni Yeye ndiye anaye waita waja wake wote kuingia kwenye ngome yake ili wapate utukufu kwake na utukufu wote ni wa Allah tu. Na wala hataki kwa yeyote kuliachia kwa hiari yake au kwa kutenzwa nguvu, fungu lake katika uhuru; uhuru ambao ndio sifa ya upekee na muhimili wa utukufu wake.
Na nguvu ya kimaada iwe itakavyo kuwa, haimiliki katu kumfanya mtu anaye utaka uhuru kuwa mtumwa, bali mtu atashikamana na ule utukufu wake wa kibinaadamu. La mwisho kabisa ambalo inamiliki nguvu hiyo ya kimaada ni kuumiliki mwili wa mtu; inaweza kuufanyia makero/maudhi, kuuadhibu na kuufunga. Ama dhamira, roho na akili, hivyo hawezi mtu yeyote awaye kuvifungia kama anavyo utia mahabusu mwili na wala hawezi kuvidhalilisha kama anavyo weza kuudhalilisha mwili kwa anuwai za adhabu. Ila tu kama atataka huyo mwenye dhamira yake, roho yake na akili yake kuvitoa vitu vyake ghali hivyo vidhalilishwe na vifungiwe hata akose uhuru wake wa kuamua kufuata au kutokufuata, kufanya au kutokufanya.
Eeeh! Ni nani huyo anaye miliki kuwafanya hao wanyonge:
- Kuwafuata wale walio takabari katika imani/itikadi na katika kufikiri na mwenendo/desturi/ tamaduni/ada zao?!
- Kumuabudu asiye Allah na ilhali Allah ndiye Muumba wao, Mruzuku wao na Mlezi wao?!
Hakuna yeyote anaye limiliki hilo, ila tu nafsi zao ndizo dhaifu. Wao ni wanyonge si kwa sababu kwamba wao ni wachache zaidi wa nguvu za kimaada kuliko hao waasi wanao wafuata, wala si kwa sababu wao ni wachache kwa cheo, utukufu au mali kuliko hao mabwana wakubwa. La hasha! Si hivyo kabisa. Hakika mambo yote hayo ni vitu vya nje (vya kimwili) ambavyo kwa dhati yake havihesabiki wala kuchukuliwa kuwa ni udhaifu unao ambatishwa na sifa ya unyonge walio nao hao watu wanyonge. Na kwa hakika si kwa jenginelo, wao wamekuwa wanyonge walio kosa uhuru wa kuamua kutenda/kutokutenda, kwa sababu huo unyonge umo ndani ya roho zao, mvunguni mwa mioyo yao, mabongoni mwao na katika kujitukuza kwao kwenye kitu makhususi alicho pewa mwanaadamu tu miongoni mwa viumbe vyote.
Hakika hao watu wanyonge wafuasi wa mabwana wakubwa ni wengi, na hao miungu watu wanao jivika madaraka ya kuwapangia wenzao sheria na kuwalazimisha kuzifuata na wakikataa huwaadhibu kwa kuwawekea vikwazo, hao ni wachache. Basi hebu jiulize, ni nani anaye weza kuwalazimisha hao wengi kuwanyenyekea na kuwafuata wale walio wachache?! Na ni kitu/jambo gani linalo watiisha amri na kuwanyenyekesha hao walio wengi kwa wale walio wachache?! Hakika si kwa kinginecho, kinacho wanyenyekesha na kuwatiisha amri ni udhaifu/unyonge wa roho, kuporomoka kwa hima, uchache wa murua na uachiliaji wa utukufu wa ndani ambao Allah amewatunukia wanaadamu. Ni jambo lisilo kubali mjadala, hakika hao miungu watu hawamiliki kulidhalilisha kundi kubwa la walio wengi ila tu ni kwa kupenda kwa hilo kundi kubwa. Kwani hilo kundi kubwa siku zote lau likitaka, lina uwezo wa kusimama na kundi la hao walio wachache, basi tufahamu ya kwamba kule kutaka ndiko kunako ipunguza nguvu ya wale walio wengi.
Ni kweli, tena ni kweli kabisa ya kwamba udhalili hautokani ila na ile hali ya kuukubali udhalili iliyomo ndani ya nafsi za wale walio madhalili, na hiyo hali ya kuukubali udhalili ndio inayo tegemewa na hao miungu watu katika kulinyenyekesha na kulitiisha amri kwao hilo kundi kubwa. Na hao madhalili hapa katika muonekano na mandhari ya akhera katika unyonge wao na kuwafuata kwao hao walio takabari, wanawauliza hao mabwana wakubwa walio jivika uungu: “… Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Allah?” … Na hakika sisi tulikufuateni huko duniani, ndio leo tukaishia kwenye mafikio haya yatiayo uchungu mkubwa?!
Au huenda wao wakiwa tayari wamekwisha iona adhabu inayo wakabili ndipo wanaanza kuwakaripia/kuwalaumu wale mabwana wakubwa wao walio takabari ulimwenguni, kwa kuwaongoza vibaya na kuwapelekea kwenye adhabu hiyo? Hakika mlolongo wa maneno unayaelezea maneno hayo yakiwa na muhuri wa udhalili kwa hali zote. Na wale walio takabari wanalijibu swali lao hilo: “… Watasema: Lau Allah angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri, hatuna pa kukimbilia”. Hili ni jawabu jibishi ambalo linaonyesha kukimwa na kuona dhiki: “Lau Allah angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni”.
Basi ni kwa lipi hasa mnatulaumu na ilhali sisi na nyinyi sote tuko katika njia moja kuelekea kwenye hatima moja?! Hakika sisi hatukuongoka na tukakupotezeni nyinyi, lau Allah angeli tuongoa basi nasi tungeli kuongozeeni kwenye huo uwongofu pamoja nasi kama ambavyo tulivyo kuongozeeni kwenye upotofu pale tulipo potoka! Kwa maneno yao hayo wao wanaunasibisha uwongofu na upotofu wao kwa Allah, wakati huo sasa ndio wanaukiri uwezo wake na ilhali hapo kabla walikuwa wakimkufuru na kuukanusha uwezo huo. Na wakijikweza kwa wale wanyonge kujikweza kwa mtu ambaye asiye uona uwezo wa Yule aliye Mtenza nguvu, Mwenye nguvu zisizo wezwa. Hakika wao wanasema hivyo si kwa jenginelo, wanacho kikimbia ni ule mzigo wa upotevu na upotoshaji kwa kulirejesha jambo hilo kwa Allah. Na ilhali Allah haamrishi upotofu kama alivyo sema Yeye ambaye utakati wa mawi ni wake: “… Hakika Allah haamrishi mambo machafu…”. Al-A’araaf [07]:28
Kisha tena wao ndio wanawakaripia na kuwalaumu wale walio kuwa wafuasi wao wanyonge kwa mtazamo wa uficho na wanatangaza ya kwamba hapana faida ya kupapatika kama ambavyo kusivyo na faida ya kusubiri. Kwani bila ya shaka adhabu imekwisha thibiti na wala huko kupapatika au kusubiri katu hakuwezi kuizuia adhabu hiyo ya Mola iliyo kwisha thibiti juu yetu. Aah wapi, tayari umekwisha pita ule wakati ambao kupapatika kwa sababu ya adhabu kulikuwa kunanufaisha na kukawa ni sababu ya kuwarejesha wapotofu kwenye uwongofu walio takiwa na Mola Muumba wao. Na wakati huo kusubiria shida/matatizo kulikuwa kunanufaisha, kukawa ni sababu ya kupatwa na rehema ya Allah. Kila kitu na mambo yote yamekwisha na kufikia ukomo wake, na hapana tena makimbilio wala pa kuokokea: “Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri, hatuna pa kukimbilia”.
Pamekwisha hukumiwa, mjadala umefungwa na mdahalo umekoma. Hapo ndipo tunaona ajabu kwenye onyesho letu kupitia Televisheni Qur’ani, tunamuona shetani; mlinganiaji wa upotofu na mtumbukiza shimoni. Tunamuona wakati huo sasa amevaa uhalisia wa kuhani au uhalisia wa shetani mwenyewe hasa kwa sifa zake zote. Anafanya ushetani wake kwa wale wafuasi wanyonge na wale wafuatwa walio takabari kwa maneno ambayo huenda yakawa makali na machungu zaidi kwao kuliko hata hiyo adhabu ya Mola wao: “Na shetani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Allah alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Allah. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu”. Ibraahim [14]:22
Allah! Allah hakika shetani kweli ni shetani! Na hakika uhalisia wake kabisa unaonekana hapa katika sura yake kamili kama ulivyo onekana uhalisia wa wale wafuasi wanyonge na wafuatwa walio takabari katika majibizano haya. Hakika huyo ndiye shetani aliye zitia wasiwasi nyoyo, akawaghuri watu kumuasi Mola wao, akaupamba ukafiri ukapendwa na kufuatwa na akawazuia watu kusikiliza mahubiri. Ni huyo huyo ndiye anaye waambia na kuwachoma mchomo mkali unao penya moyoni wakati ambao hawawezi kumjibisha na ilhali hukumu ya Mungu imekwisha pitishwa. Huyo ndiye anaye waambia sasa, tena baada ya kupita muda: “Hakika Allah alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni”!
Kisha anawafedhehesha kwa mchomo mwingine kwa kumuitika kwao wakamfuata na ilhali yeye hakuwa na mamlaka juu yao, akawalazimisha isipo kuwa ni wao ndio walio uvua murua wao na wakausahau ule uadui wa tangu na tangu uliopo baina yao na shetani. Basi wakauitika wito wake wa batili na wakauacha ule wito wa haki kutoka kwa Allah; Mola wao Mlezi: “Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia”. Kisha anawalaumu na anawataka wajilaumu wao wenyewe kwa kumuitika pale alipo waita: “Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe”. Kisha huyoo anawaacha na kukung’uta mikono yake na ilhali ni yeye ndiye aliye waahidi na kuwatamanisha hapo kabla na akawatia wasiwasi pale alipo washinda. Na ama wakati huo sasa, hawaitikii wao pale wanapo piga ukelele kutokana na adhabu iliyo mbele yao kama ambavyo wao hawawezi kumsaidia atapo papatika kutafuta kuokoka na adhabu ya Mola: “Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu”. Na wala hapana leo baina yetu mafungamano/mahusiano wala urafiki. Kisha anajitenga mbali na kumshirikisha kwao na anaukana ushirika huo: “Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Allah”. Kisha anaimalizia khutba yake hiyo ya kishetani kwa rungu linalo wapata marafiki zake: “Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu”.
Heeh! Ole wake shetani na ole wao wale walio mfanya kuwa rafiki yao aliye waita kwenye upotofu na wao wakamtii. Mitume wa Allah waliwaitia kwa Allah, wakawakadhibisha na wakawapinga. Na kabla halijakunjwa pazia la onyesho la filamu yetu inayo kujia kupitia Televisheni yako pendwa “Qur’ani”, tuangalie kwa upande mwingine, upande wa wale watu waumini; watu walio fuzu, watu walio okoka: “Na walio amini na wakatenda mema, wataingizwa katika mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam!”. Ibraahim [14]:23
Hapa sasa linafungwa onyesho letu. Heeh! Onyesho lilioje! Heeh! Mwisho ulioje wa kisa cha da’awa (ulinganiaji/uhubiri dini) na hao wadau wa da’awa pamoja na hao wakadhibishaji wapingaji na miungu watu wanao taka kutiiwa amri/kauli zao huku wakizipinga amri za Mola Muumba wao.
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
Ewe Mola wetu Mlezi! Ewe ambaye uliye wausia walio tutangulia, kukucha wewe, ukatuusia nasi pia! Kwa kuwa sisi waja wako ni dhaifu, hatuna uwezo wa kutenda twaa wala nguvu ya kuyaepuka maasi ila tu kwa kuwezeshwa na Wewe. Tunakuomba utuvike na kutupamba na vazi la uchaMngu, litupendezeshe mbele yako, Mtume wako na waja wako jamia. Vazi hilo liwe ni ngome yetu dhidi ya shari zote tuzijuazo na tusizo zijua, liwe ni hirizi yetu dhidi ya adui shetani na liwe kinga yetu dhidi ya adhabu yako iliyo kali. Ewe Mola wetu Mlezi, tutakabalie dua yetu!
Hapa ndio tamati ya Jukwaa letu juma hili, tamati hii inatusukuma kuamini kwamba filamu hii “Fitina ya wafuasi na wafuatwa” inayo onyeshwa na Televisheni Qur’ani inakusogeza karibu zaidi na Imani na kuhepa kila kiingiacho mjini, jambo ambalo litakusukuma kufanya amali njema zitakazo kuwa nusura na muokozi wako katika siku hiyo yenye vituko, vishindo na misukosuko.
Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele hiki hiki cha fitina ya wafuasi na wafuatwa chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.
Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:
“Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allah, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa”. Al-Baqarah [02]:281