SOMO LA KUMI NA SABA SEHEMU YA SABA

MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.

Shukrani zote ni stahiki na milki yake Allah Mtukufu; aliye uumba ulimwengu kuwa ni nyumba na uwanja wa matendo na akaiumba Akhera kuwa ni uwanja wa hisabu na nyumba ya jazaa sawiya kwa jinsi ya matendo yaliyo tendwa na waja duniani. Sala na salamu zimuendee mbora wa walio tenda matendo mema duniani kwa ajili ya nyumba ya milele ya akhera. Ziwaendee kadhalika Aali, Sahaba na umati wake wote.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Ni jambo jema, tena la wajibu, tuanze kwa kumshukuru Mola wetu Muweza wa kila kitu ambaye kwa uwezo na matashi yake, ametujaalia uhai na uzima hata tukaweza kukutana kwa mara nyingine tena katika ukumbi wetu huu wa kukumbushana. Mola wetu Mtukufu tunakuomba utuzawadie ufahamu utokao kwako ili tuzidi kukumbushana, ukumbusho ambao utakuwa ni kani ya kutusukuma kutenda amali njema ili tupate kukutana nawe katika siku ngumu ya Kiyama, nawe ukiwa radhi nasi.

Mandhari ya wakanushaji na makafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele tulicho kianza majuma kadhaa yaliyo pita, kipengele kisomekacho:

  • Fitina ya wafuataji (wafuasi) na wafuatwa (viongozi).

Na hii hapa ni sura nyingine ya kuhasimiana (kuzozana) kwa wafuasi na wale walio kuwa viongozi wa upotofu miongoni mwa wenye misingi inayo kinzana na Uislamu:

Allah Atukukiaye anasema: “Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu – Badala ya Allah. Waongozeni njia ya Jahannamu! Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: Mna nini? Mbona hamsaidiani? Bali hii leo, watasalimu amri. Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa waumini. Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. Wao walipo kuwa wakiambiwa {Laa Ilaaha illal-laah} Hapana mungu ila ni Allah tu, wakijivuna”. Asw-Swafaat [37]:22-35

Na hii hali kadhalika ni sura nyingine ya kuhasimiana (kuzozana) waabudu na waabudiwa:

Allah Ataadhamiaye anasema: “Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu. Badala ya Allah? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu. Na majeshi ya Ibilisi yote. Watasema na hali ya kuwa wanazozana humo: Wallah! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. Na hawakutupoteza ila wale wakosefu”. As-Shu’araa [26]:91-99

Hao waabudu watawasemeza miungu watu wao ambao walikuwa wakiwaabudu kwa kuwatii na kuwafuata kwa kila walilo waambia na kuwaamrisha pasina kuhoji wala kubisha, bali wakisema kwa mioyo, vinywa na vitendo vyao: “Tumesikia na tumetii”. Watasema hivyo hali ya kuwa wanakiri upotofu wao kwa kuwa walikuwa wakiwaabudu na wakiwalinganisha na Mola Muumba wao na ameruka patupu na kula hasara yule aliye mnyanyua kiumbe mwenzake hata akamfikisha kwenye daraja ya uungu. Na kila aliye muabudu mungu asiye Allah, huyo bila shaka atakuwa amemlinganisha Muumbaji na kiumbe (muumbwa) na kufanya hivyo ndio dhulma kubwa kama alivyo sema Bwana Luqmaan kumwambia mwanawe: “…Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allah. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa”. Luqmaan [31]:13

Ama tukienda kwa wale watu wema wabora (Swaalihiina) walio abudiwa hali ya kuwa hawajui kama wanaabudiwa kinyume na Allah, au wale walio abudiwa pasina wao kuliridhia hilo kama vile Malaika wa Allah. Hakika bila ya shaka wao watawaruka mbali wale walio kuwa wakiwaabudu na watayakanusha madai ya waabudu wao na uzushi wao, kwani Malaika hawakutaka kuabudiwa na wala hawakuridhia wao kuabudiwa. Lakini wale walio taka kuabudiwa ni majini waovu ili wapate kuipotosha jamii ya wanaadamu na kuitumbukiza kwenye lindi la Jahannamu, kwa hivyo hao walio potea ni waabudu majini na sio Malaika: “Na siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je! Hawa walikuwa wakikuabuduni? Waseme: Subhaanaka! Umetakasika. Wewe ndiye kipenzi chetu si hao. Bali wao walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao”. Sabai [34]40-41

Si hivyo tu, bali siku hiyo ya Kiyama kutakuwa na mzozo na majibizano baina ya kafiri na rafiki/mwenza wake shetani. Allah Mwenye utukufu na ukarimu anasema: “Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda. Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka. Aliye weka mungu mwengine pamoja na Allah. Basi mtupeni katika adhabu kali. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali. (Allah) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu”. Qaaf [50]:23-29

Jambo halitakomea hapo, bali siku hiyo ya Kiayama hata mwili utagombana na kuzozana na roho.

Imamu Ibnu Kathiir-Allah amrehemu-amesema: “Amepokea Ibnu Mandah katika kitabu {AR-RUUHU} kutoka kwa Ibnu Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Watu watahasimiana (watagombana) siku ya Kiyama mpaka roho nayo itagombana na mwili, basi roho itasema kuuambia mwili: Wewe ndiye uliye tenda. Na mwili nao utaiambia roho: Wewe ndiye uliye amuru na wewe ndiye uliye nipambia (hata nikatenda). Basi Allah atampeleka Malaika kuamua baina yao (Roho na mwili), awaambie: Hakika mfano wenu wawili nyie, ni kama mtu kiwete aonaye na mwingine ni kipofu walio ingia kwenye bustani. Basi yule kiwete akamwambia aliye kipofu: Mimi ninayaona hapa matunda, lakini hayana shina. Na yule kipofu akamwambia: Nipande uyachume. Basi (kiwete) akampanda na kuyachuma. Basi ni yupi kati ya wawili hao aliye fanya uadui (kwa mwenzake)? Basi watajibu: Ni wote wawili. Basi hapo ndipo yule Malaika atawaambia: Hakika nyinyi mmekwisha jihukumu wenyewe. Yaani mwili kwa roho ni kama kipando chake ambacho (roho) inakipanda (katika kuyafikia hayo ya kutendwa)”. [TAFSIIR IBNU KATHIIR 06/96]-Allah amrehemu.

Katika hali hiyo ya mzozo, watajichukia wenyewe: “Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka kukuchukieni Allah ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye imani nanyi mnakataa”. Ghaafir [40]:10

Watajichukia wao wenyewe na watawachukia wale wote walio kuwa waunga mkono na wasaidizi wao na vipenzi vyao duniani, watawaombea maangamizi na kutaka wapewe adhabu zaidi: “Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika moto. Watasema: Laiti tungeli mtii Allah na tungeli mtii Mtume! Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwatii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia. Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa”. Al-Ahzaab [33]:36-38

Na kutokana na kufura kwao hasira kwa wale walio wapoteza, watamuomba Allah awaonyeshe wale walio wapoteza duniani ili wawakanyage kwa miguu yao na kuwadidimizia motoni: “Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa”. Fus-swilat [41]:29

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe Mola Muumba wetu! Ewe ambaye uliye mtahini baba yetu Ibrahimu na ukampa ufaulu wa mitihani yako hiyo. Na kwa kuwa ni Wewe ambaye unaye tutahini kila leo katika maisha na imani yetu, tunakuomba utunusuru na balaa za Dunia na utuwezeshe kufaulu mitihani ya ulimwengu huu, ile ya barzakhi na ile ya siku ngumu; siku ya kisimamo cha hisabu na jazaa. Tujaalie kuzikumbuka na kuzishukuru neema zako. Ewe Mola wetu uliye Msikivu mno, itakabali dua yetu!

Kwa juma hili, hilo ndilo jukwaa letu na hayo ndio tuliyo wafikiwa kukumbushana, tumuombe Mola wetu Mkarimu kupitia ukarimu wake huo ulio kienea kila kiumbe chake, atubarikie ufahamu wetu ili tupate kufahamu na kukumbuka na wala asitujaalie kuwa kama wale ambao: “…wana nyoyo lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo…”.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

Jueni ya kwamba maisha ya Dunia ni mchezo, na pumbao na pambo, na kujifakharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Allah na radhi. Na maisha ya Dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu”. Al-Hadiid [57]:20

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *