“MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI”
Sifa njema zote ni haki ya Allah; Mola wa viumbe wote. Yeye pekee ndiye wa kuabudiwa na kuombwa. Rehema na Amani zishuke juu ya Bwana wetu Muhammad bin Abdillah, maswahaba wake na kila aliye itika mwito wake na kufuata maagizo yake.
Ama baad,
Mpendwa mwana-jukwaa letu.
Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!
Tuzidi kumshukuru Allah Mola Muumba wetu kwa kuturuzuku bure uhai na uzima hata tukaweza kukutana leo katika ukumbi wetu huu wa kukumbushana kuhusiana na ile siku ngumu na nzito tutakayo ipitia wanaadamu. Siku ambayo sote tutahudhurishwa mbele ya Mola Muumba wetu kwa ajili ya kuhisabiwa kwa matendo yetu tuliyo yatenda duniani na kisha kulipwa jazaa sawiya yenye uadilifu mtupu; isiyo na dhulma wala upendeleo kwa yeyote. Juma hili pia bado tunaendelea na jukwaa letu lililo beba anuani isomekayo:
Mandhari ya wakanushaji na makafiri.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele tulicho kianza majuma kadhaa yaliyo pita, kipengele kisomekacho:
- Viungo vitakiri na kutoa ushahidi wa makosa ya mwanaadamu.
Siku ya Kiyama, kwa idhini yake Allah viungo vya mwanaadamu vitatamka kwa lugha fasaha inayo eleweka na kila mtu, vitakiri na kutoa ushahidi wa kosa la kila aliye mkufuru Allah Mtukufu na dhambi ya kila aliye muasi Allah. Tusome na tuzingatie: “Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda”. An-Nuur [24]:24
Tuendelee kusoma na kuzingatia: “Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma”. Yaasin [36]:65
“Na siku watakapo kusanywa maadui wa Allah kwenye moto, nao wakigawanywa kwa makundi. Hata watakapo ufikia moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Allah ambaye amekitamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Allah hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda. Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi, imekuangamizeni na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri. Basi wakisubiri moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi hawakubaliwi”. Fusswilat [41]:19-24
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Je, nyinyi mnadhurika mkiliangalia jua katika mchana wa adhuhuri usio na mawingu? Wakajibu (Maswahaba): Hapana. Je, nyinyi mnadhurika mkiuangalia mwezi wa usiku angavu usio na mawingu? Wakajibu: Hapana. Basi (ikiwa hivyo ndivyo), nyinyi hamtadhurika katika kumuona Mola wenu Mlezi Mwenye utukufu na nguvu ila kama ambavyo mnadhurika katika kukiona kimojawapo cha viwili hivyo (jua au mwezi). (Allah) akutane na mja (wake) amwambie: Ewe fulani! Hivi sikukutukuza, nikakupa ukubwa/uongozi/utawala na nikakuozesha, na nikakudhalilishia (vikutumikie) farasi (kipando) na ngamia (kubeba mizigo) na nikakuacha uongoze na kukaa katika utawala? Ajibu (mja): Kwani, ewe Mola wangu Mlezi (ulinifanyia yote hayo). (Allah) amuulize: Hivi wewe ulikuwa na yakini ya kukutana nami? Ajibu: Hapana. Allah amwambie: Basi hakika Mimi (leo) nakusahau (nakuacha) kama wewe ulivyo nisahau (ulivyo puuza ujumbe wangu ulio letewa na Mitume wangu).
Kisha akutane na (mja) wa pili, amuulize: Ewe fulani! Hivi sikukutukuza, nikakupa ukubwa/uongozi/utawala na nikakuozesha, na nikakudhalilishia (vikutumikie) farasi (kipando) na ngamia (kubeba mizigo) na nikakuacha uongoze na kukaa katika utawala? Ajibu (mja): Kwani, ewe Mola wangu Mlezi (ulinifanyia yote hayo). (Allah) amuulize: Hivi wewe ulikuwa na yakini ya kukutana nami? Ajibu: Hapana. Allah amwambie: Basi hakika Mimi (leo) nakusahau (nakuacha) kama wewe ulivyo nisahau.
Kisha akutane na wa tatu na amwambie kama alivyo waambia wale wengine. Huyo amwambie: Mola wangu Mlezi! Mimi nilikuamini Wewe, Kitabu chako na Mitume wako. Na niliswali, nilifunga na nikatoa sadaka. Na amsifie kheri kiasi awezacho. Allah (amwambie): Hapa hapa kwa hiyo. Kisha pasemwe: Sasa hivi, tunakuletea shahidi wa kushuhudia dhidi yako. Afikirie nafsini mwake (ajiambie): Ni nani atakaye toa ushahidi dhidi yangu? Basi kizibwe kinywa chake na liambiwe paja lake: Tamka. Basi litatamka paja lake, nyama zake na mifupa yake (vitaje) matendo yake ili asiwe na udhuru. Na huyo ni yule mnafiki ambaye Allah anamchukia”. Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 7032]-Allah amrehemu.
Eeeh, ewe masikini wee! Hebu piga picha yako kisha ujiangalie ukiwa umekamatwa mikono na malaika kulia na kushoto, mbele ya Allah Mtukufu akikuuliza ana kwa ana; wewe na Yeye. Akuulize:
- Hivi sikukupa neema ya ujana, basi uliuchakaza katika nini?
- Hivi sikukurefushia umri, basi uliumaliza katika nini?
- Hivi sikukuruzuku mali, basi uliichuma na kuitumiaje?
- Hivi sikukukirimu elimu, basi ulikitendea nini kile ulicho kijua?
Katika hali hiyo na mazingira hayo, haya na aibu yako itakuwaje wakati Allah akikutajia neema alizo kutunuku na upande mwingine akikutajia maasi na madhambi yako?! Ukikanusha, vinatoa ushahidi viungo vya mwili wako mwenyewe. Anasema Anas-Allah amuwiye radhi: Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akacheka, kisha akatuuliza: “Mnajua ni nini kinacho nichekesha?” Tukajibu: Allah na Mtume wake ndio wajuao mno. Akasema: “Kinacho nichekesha ni maongezi ya mja na Mola wake Mlezi, atasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Je, hukuniokoa na dhulma?” Akasema: “Atasema kwani (nimekuokoa). Akaendelea kusema: “Basi atasema (Allah): Hakika Mimi simruhusu mbele yangu ila shahidi atokaye kwangu, aseme: Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu na waandishi watukufu wanatosha kuwa mashahidi”. Akasema: “Basi kitazibwa kinywa chake na viambiwe viungo vyake tamkeni”. Akasema: “Basi navyo vitatamka kuyataja matendo yake kisha kitafunguliwa kinywa chake na ataviambia viungo vyake: Mtokomee mbali na muangamie! Kwani ni nyinyi ndio nilio kuwa nikikuteteeni”. Muslim [SAHIH AL-JAAMI’I 8134]-Allah amrehemu.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-sote kwa unyenyekevu mkubwa tumuombe Allah atukinge na atuepushe na fedheha kubwa hiyo mbele ya kadamnasi kubwa ya watu ambayo haikuwahi kutokea wala haitatokea tena baada ya siku hiyo. Fedheha ya kutolewa ushahidi wa kuangamizwa na viungo vya mtu mwenyewe. Allah amsitiri kila muumini, mambo yake yasichomozewe na; yasionwe wala kusikilizwa na yeyote kama alivyo ahidi.
Ewe ndugu mwema weeh! Hebu mche na umuogope Allah kupitia viungo vyako hivyo; usivipeleke kwenye maasi na madhambi na badala yake vielekeze katika kumtii Allah. Kumbuka ya kwamba viungo vyako hivyo kwa idhini na amri ya Mola Muumba wako vitatamka, vitazungumza na vitaeleza yale yote uliyo yatenda. Na hilo la kutamka na kusema viungo vyako si jambo la ajabu ikiwa utajua ya kwamba ardhi inayo tokana na mawe na miamba itazungumza na kueleza yale yote yaliyo tokea juu ya mgongo wake, kama anavyo tuambia hilo Mwenye ardhi yake: “Siku hiyo itahadithia khabari zake. Kwa sababu Mola wake Mlezi ameifunulia”. Az-Zalzalah [99]:04-05
Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:
رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41
Yaa Rabbana! Ewe uyajuaye ya siri na ya dhaahiri! Kwa ujuzi wako huo ulio kienea kila kitokeacho mbinguni na ardhini, tunakuomba uturuzuku ukweli katika kauli zetu, subira katika hasira zetu, busara katika maamuzi yetu. Tena tupe mahaba katika udugu wetu, masikilizano katika aila zetu, ikhlasi katika amali zetu. Tutunuku wema katika nyoyo zetu, baraka katika riziki zetu, utulivu katika nafsi zetu. Tunakuomba utupe amani na salama katika maisha yetu, shifaa katika maradhi yetu, shahada katika mauti yetu, nuru katika makaburi yetu na makaazi katika Jannatil-Firdaus. Aamina yaa Rabbal-A’alaamiina!
Hapa tulipo fikia, ndio tamati ya tuliyo jaaliwa kukuletea katika jukwaa letu la juma hili. Tumuombe Allah; Mola Mlezi wetu alidaimishe jukwaa letu hili ili tupate kuongeza yakini yetu juu ya siku ya Kiyama. Kwani ni kwa kuwa na yakini hiyo tu, ndio tutaweza kufikiri kabla ya ama kutenda au kutokutenda na kwa nini kutenda au kutokutenda. Tufanye hivyo kwa faida, maslahi na manufaa yetu wenyewe.
Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaanza kukiangalia kipengele kingine chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.
Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.
Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:
“Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Allah na Mitume wake. Hiyo ndio fadhila ya Allah, humpa amtakaye. Na Allah ni Mwenye fadhila kuu”. Al-Hadiid [57]:21