SOMO LA KUMI NA SABA

MANDHARI NA MUONEKANO WA WAKANUSHAJI NA MAKAFIRI.

Sifa zote njema ni zake Mola Muumba wa viumbe vyote ambaye: “…Yeye ndiye Allah mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma”. Sala na salamu zimuendee mbora wa walio iamini siku ya Kiyama na mbora wa walio jiandaa nayo. Ziwaendee kadhalika Aali, Sahaba na umati wake wote.

Ama baad,

Mpendwa mwana-jukwaa letu.

Assalaamu Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Kwa auni na msaada wake Allah Mola wetu Mkarimu, leo tena tunaendelea na mfululizo wa makala za jukwaa letu, makala zihusianazo na kukumbushana siku iliyo karibia mno, siku ya Kiyama. Tunasema huku tukimtegemea Mola wetu atuongoze katika jukwaa letu hili ili lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwake yapate kutimia.

Mandhari ya wakanushaji na makafiri.

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-juma hili chini ya anuani mama hiyo hapo juu, kwa uwezeshi wake Mola wetu Mlezi tutaendelea kukiangalia kipengele kingine kisomekacho:

  • Fitina ya wafuataji (wafuasi) na wafuatwa (viongozi).

Kwa uwezeshi wake Allah na kwa kupitia Televisheni Qur’ani tunaendelea kukitazama kipindi cha Mandhari ya wakanushaji na makafiri. Na kipindi chetu cha leo tutaingalia filamu ya kweli na wala si ya kubuni; filamu itakayo tuonyesha namna watakavyo jitenga mbali wale wafuataji wa kibubusa walio kuwa wakifuata kila wanalo ambiwa au kuletewa pasina kuhoji wala kujali. Wakiambiwa na wakubwa sasa mwanaume amuoe mwanamume mwenzake na mwanamke aolewe na mwanamke mwenzake, wao husema “Ewallah! Tumesikia na tumetii”. Wakiambiwa kukopeshana sasa ni kwa riba, hukubali. Wakubwa wale wajiitao watu wa ulimwengu wa kwanza, wanamume wakivaa hereni na mikufu na wakasuka na nywele kama wanawake, nao huiga na kufuata. Na …. Na …. Wakawafuata katika anuwai za machafu, madhambi na maovu wakubwa wao hao, wenye mamlaka miongoni mwao na wale walio kuwa matajiri katika wao.

Aah! Hakika filamu yetu ya leo inatuonyesha mandhari ya fedheha inayo zichana chana nyoyo za waumini kutokana na kuiangalia. Hakika mandhari hiyo ni kipindi cha mtengano ambacho watajitenga mbali wale wafuasi walio tenda dhambi kwa kuwafuata wakubwa wao pasina kumuonea haya Mola Muumba wao. Watajitenga mbali na wale walio kuwa wakiwafuata katika ukafiri na upotevu wao. Na mwanzo wa fitina hiyo ulianzia katika uhai wa dunia kama anavyo tuambia Allah Mwenye utukufu na ukarimu ndani ya Kitabu chake kitukufu: “Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo”. Al-Ankabuut [29]:12

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tuiangalie Televisheni Qur’ani huku tukizingatia kupitia filamu tunayo ingalia. Naam, huo ndio mwanzo wa fitina na hiyo ndio ada na mbinu inayo tumiwa na wapotofu katika vitimbi vyao wanavyo wafanyia waumini, huwataka na huwapa ahadi na maagano waumini ili wawafuate katika ukafiri wao. Tena huwaambia ya kwamba watayabeba madhambi yao siku ya Kiyama, husema hivyo “kwa njia ya vitimbi na udanganyifu”. Basi muumini yeyote atakaye wafuata duniani, huyo bila ya shaka akhera ataonja majuto ya milele; yasiyo katika. Ni kwa ajili hiyo basi, ndio Allah akasema kuwarudi makafiri hao: “… Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua”. Al-Ankabuut [29]:12-13

Na ili tupate kuifahamu vema filamu hii, hakika Allah Atukukiaye anatusawirishia mandhari hiyo ilhali akitutahadharisha dhidi ya kuwafuata wadau wa batili na majuto ya siku ya Kiyama, akasema: “Na wote watahudhuria mbele ya Allah. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Allah? Watasema: Lau Allah angeli tuongoa basi basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri, hatuna pa kukimbilia”. Ibraahim [14]:21

Yaani: Watasema wale wafuasi (wafuataji) walio madhaifu wa imani, kuwaambia wale viongozi na makafiri, hakika sisi tulifuata nyayo zenu katika kila lililo mghadhibisha Allah na hatukupata kuiasi amri yenu kamwe. Bali tulimuasi Allah ili tukuridhisheni nyinyi, basi tulivyo kutiini na kukufuateni katika maisha ya dunia, je leo hamtusaidii tukapata japo kupunguziwa adhabu hii chungu?!

Eheeh! Majuto makubwa yaliyoje!

Filamu yetu bado inaendelea kutuletea mandhari na muonekano wa wakanushaji na makafiri namna watakavyo kuwa katika ile siku yenye mshindo mkuu, Allah Mwenye utukufu na ukarimu anatuambia: “Na watapo hojiana huko motoni, wanyonge watawaambia walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi hamtuondolei sehemu ya huu moto? Watasema walio jitukuza: Hakika sote sisi tumo humo humo! Kwani Allah kesha hukumu baina ya waja!”. Ghaafir [40]:48

Yaani: Wale wanyonge walio kuwa bendera fuata upepo, wakifuata kila wanalo ambiwa au kuletewa na mabwana wakubwa, watapo ionja adhabu ya Allah siku ya Kiyama, watawaomba msaada mabwana wao hao walio kuwa wakiwatii na ihali wakimuasi Mola Muumba wao, wapate ahueni ya adhabu chungu hiyo. Tahamaki wale mabwana watiiwa wamekuwa wanyonge, nyuso zao zimedhalilika mbele ya Yule aliye hai milele, hawana wakimilikicho chochote na wala hawawezi lolote. Hapo ndipo kwa udhalili na unyonge mkubwa watawaambia walio kuwa wafuasi wao: “Hakika sote sisi tumo humo humo! Kwani Allah kesha hukumu baina ya waja!”

Na akthari ya (wengi wa) madhaalimu kama si wote haya ndiyo maneno yao wanayo waambia watu wanyonge wanao wafuata pasina kuwahoji, maneno hayo tumenukuliwa na Qur’ani Tukufu, tusome na tuzingatie: “Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua”. Al-Ankabuut [29]:12-13

Basi wale wenye akili pevu miongoni mwa waja wa Allah, hawaghuriki na maneno hayo ya mabwana wakubwa na wala hawawafuati wao ilhali wanajua ya kwamba wanamghadhibisha Mola Muumba wao. Na watakao ghurika na maneno yao hayo na wakawafuata, basi wao hao watashirikiana na wakubwa hao katika adhabu, fedheha na majuto katika siku hiyo ya Kiyama. Hebu basi ewe ndugu mwema, tusawirishe pamoja ili tupate kuiona picha ya fedheha na majuto watakayo kuwa nayo wale wanyonge wafuasi na wale mabwana wakubwa walio kuwa wakifuatwa. Wale wafuasi wanyonge wanawatuhumu viongozi wao kwa kuwa kikwazo baina yao na Imani. Na wale mabwana wakubwa wanawaambia wafuasi wao nyinyi ni watu wahalifu (wakosefu), sisi tulikuiteni tu nanyi mkatuitika (mkatufuata). Basi lau utawaona pale watakapo simamishwa mbele ya Mola Mlezi wao pasina kutaka kwao wala kupenda, yatawafika na kuwafunika madhila hayana kifani chake nao wakisubiria jazaa yao sawiya.

Hapo watarejesheana maneno wenyewe kwa wenyewe; huyu akimlaumu yule na yule akimkosoa huyu. Wale wafuasi wa upotofu ambao walikuwa wanyonge watawaambia wale mabwana wakubwa walio kuwa wakiwafuata: “… Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa waumini sisi”. Sabai [34]:31

Hao wafuasi wanyonge watawaambia maneno hayo mabwana wakubwa siku hiyo ya Kiyama wakati ambapo hawakuweza kuthubutu kuwaambia hivyo katika maisha ya dunia. Lililo kuwa likiwazuia kuwaambia au kuwahoji, ni ule udhalili, unyonge, unyenyekevu, kuuza uhuru wao wa kibinadaamu walio tunukiwa na Allah kwa thamani duni na kuiuza heshima na utukufu walio pewa na Allah. Hayo ndio yaliyo wafunga mdomo hata wakashindwa kuhojiana na mabwana wakubwa hao walio kuwa wakiwafuata kwa wa kila lao. Sasa leo katika siku ya Kiyama, wakiwa kwenye majuto yasiyo nufaisha na tayari wakiwa wamesha ielekea adhabu chungu, hapo sasa ndio wanapata ujasiri wa kuwaambia mabwana wakubwa pasina kuogopa kama walivyo kuwa katika uhai wa dunia: “… Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa waumini sisi”.

Yaani: Nyinyi ndio mlio kuwa kizuizi baina yetu na Imani, hakika mlitupambia ufasiki na ukafiri, basi nyinyi ni wahalifu/wakosefu mnao stahiki kupata adhabu kali. Na katika kipindi hicho wale walio takabari katika ardhi itawapata huzuni kuu, kwa kuwa wao wako sawa katika adhabu na washirika (wafuasi) wao. Na hapo sasa ndio watawarudi washirika wao kwa udhalili ulio sheheni ufedhuli na ubaya wa maneno: “… Kwani sisi ndio tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ndio wakosefu”. Allaahu Akbar! Hao ndio duniani walikuwa hawawathamini hata kidogo wanyonge wale, hawayazingatii maoni na rai zao na wala hawakuweza kustahamili kupingwa au kuhojiwa nao. Ama leo katika majuto yale, wakubwa wale wanawauliza wanyonge na wafuasi wao, na si kuwauliza tu bali kuwauliza kwa udhalili na uduni: “… Kwani sisi ndio tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ndio wakosefu”. Sabai [34]:32

Maneno/swali lao hilo kwa walio kuwa wafuasi wao, ni kukiri kwao ya kwamba wao waliwapambia kutenda dhambi na ukafiri na kwamba wao hawakuwatenza nguvu katika hilo. Bali wafuasi wao wanyonge ndio walio kuwa tayari kukubali na kupokea ukafiri na utenda dhambi huo. Hapo sasa, ndio zinakuja radi (jawabu jibishi/rejeshi) mkataa kutoka kwa wale wanyonge ambao duniani hawakuwa na uwezo hata wa kutamka neno moja. Lakini baada ya kuondoka kwa utawala wa wakubwa wale kwa kuondoka kwa dunia na haki ikadhihiri wazi kama ulivyo uwazi wa jua la mchana, wakasema: “… Bali ni vitimbi vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha kumkufuru Allah, na tumfanyie washirika…”. Sabai [34]:33

Yaani: Vitimbi vyenu havikukomo usiku wala mchana katika kutuzuia na uwongofu, kwani nyinyi ndio mlio tupambia upotofu na mkatushajiisha kufanya ufisadi na mkisema kwamba hiyo ndio haki. Kisha leo mnaitia dosari haki ile na mnadai kwamba hiyo ni batili, na vitimbi vyenu havikutuacha mpaka mkatupoteza na kutufitinisha!!

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe Mola wetu Mwema, ulio kienea kila kiumbe wema wako! Kwa wema wako huo usio na kifani, turuzuku maisha mema yaliyo sheheni mafanikio mema duniani na akhera. Kwa wema wako huo ulio juu ya wema wa kila kiumbe, turehemu leo katika mgongo wa ardhi, kesho tutakapo kuwa chini ya ardhi na siku tutakapo hudhurishwa mbele yako kwa ajili ya hisabu ya matendo yetu na jazaa yako sawia juu yake. Kwa wema wako usio bagua, tunakuomba ijaaba ya maombi yetu haya. Aamina!

Hapa ndipo linapo tamatia Jukwaa letu juma hili ili kumpa fursa ya kutafakari kila mwenye moyo wa kukumbuka, akumbuke na awaidhike na kisha achukue hatua kwa kujiandaa na siku iliyo ahidiwa ya Kiyama.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kukiangalia kipengele hiki hiki ili tupate kukimalizia chini ya anuani yetu mama ambayo inatupeleka na kutukumbusha yale yanayo fungamana na kuhusiana na ile siku nzito na ngumu ya Kiyama kwa kupitia maneno ya Allah na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie.

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

Enyi mlio amini! Tubuni kwa Allah toba iliyo ya kweli. Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Allah hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu”. At-Tahreem [66]:08

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *